Mama Salma Awataka Ruangwa Kutunza Ardhi

Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akihutubia mamia ya wanachama wa CCM na wananchi wa Lindi Vijijini wakati akizindua rasmi sherehe za kutimiza miaka 37 ya Chama Cha Mapinduzi katika mkoa wa Lindi. Shughuli hiyo ilifanyika katika kata ya Kiwalala iliyoko Lindi Vijijini. Sherehe hiyo ilienda sambamba na kumnadi mgombea wa udiwani kupitia Chama Cha Mapinduzi  katika kata hiyo Bwana Shineni Hamis Zahoro katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika tarehe 9.2.2014.

Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akihutubia mamia ya wanachama wa CCM na wananchi wa Lindi Vijijini wakati akizindua rasmi sherehe za kutimiza miaka 37 ya Chama Cha Mapinduzi katika mkoa wa Lindi. Shughuli hiyo ilifanyika katika kata ya Kiwalala iliyoko Lindi Vijijini. Sherehe hiyo ilienda sambamba na kumnadi mgombea wa udiwani kupitia Chama Cha Mapinduzi katika kata hiyo Bwana Shineni Hamis Zahoro katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika tarehe 9.2.2014.

Mke wa Rais na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, Mama Salma Kikwete akimpongeza aliyekuwa Mwenyekiti wa Mkoa wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo, CHADEMA, Mkoa wa Lindi Bwana Ali Omar Chitanda, ambaye amekihama chama hicho na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi. Mama Salma baada ya kumpongeza alimtambulisha kwa wananchi akiwa pamoja na Bi. Asha Chadenje wakati wa sherehe za uzinduzi wa miaka y37 ya CCM mkoani Lindi tarehe 1.2.2014.

Mke wa Rais na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, Mama Salma Kikwete akimpongeza aliyekuwa Mwenyekiti wa Mkoa wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo, CHADEMA, Mkoa wa Lindi Bwana Ali Omar Chitanda, ambaye amekihama chama hicho na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi. Mama Salma baada ya kumpongeza alimtambulisha kwa wananchi akiwa pamoja na Bi. Asha Chadenje wakati wa sherehe za uzinduzi wa miaka y37 ya CCM mkoani Lindi tarehe 1.2.2014.PICHA NA JOHN LUKUWI


Na Anna Nkinda – Maelezo, Ruangwa

MKE wa Rais Mama Salma Kikwete amewataka wakazi wa Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi kuitunza ardhi nzuri na ya rutuba waliyonayo na kutokubali kuiuza kwa wageni bali waitumie katika kilimo kwa kufanya hivyo watajipatia chakula cha kutosha na hivyo kuepukana na tabia ya kuomba chakula.

Mama Kikwete ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu Taifa aliutoa wito huo jana wakati wa kilele za sherehe za kutimiza miaka 37 ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) zilizofanyika katika kata ya Likunja wilayani humo.

Mjumbe huyo wa NEC alisema wilaya hiyo imejaliwa kuwa na ardhi nzuri na rutuba ambayo mazao mengi yanastawi kwa wingi kama wananchi hao watumia ardhi hiyo kulima mazao ya vyakula kwa wingi wataepukana na tatizo la njaa.

“Ardhi ni mali na ikitunzwa vizuri itawatunza hapo baadaye itumieni kulima mazao ya chakula kama mahindi, mihogo na mtu aone aibu kwenda kuomba chakula kwa jirani kwani hata watoto wenu wakila chakula kizuri na kushiba wataweza kuwa na afya njema na kusoma vizuri wawapo shuleni”, alisema Mama Kikwete.

Akizungumzia kuhusu CCM kutimiza miaka 37 Mjumbe huyo wa NEC aliwataka wakazi wa Mkoa wa Lindi kutembea kifua mbele na kujivuna kwani Serikali ya chama chao imefanya mambo mengi ya maana ikiwa ni pamoja na ujenzi wa barabara, shule, hospitali na kuboresha hali ya maisha ya wananchi wake ukilinganisha na miaka ya nyuma.

“Leo hii kuna baadhi ya watu wanapita na kusema kuwa Serikali haijafanya jambo la maana kitu ambacho si kweli kwani ukilinganisha na miaka ya nyuma hivi sasa watoto wetu wanaomaliza darasa la saba wanajiunga na elimu ya Sekondari kwa wingi kwani shule zipo.

Hivi sasa barabara ni nzuri na ni rahisi kwa mtu kusafiri kutoka eneo moja hadi lingine tofauti na miaka ya nyuma pia huduma ya afya imeimarika. Nawaomba msiwe wanyonge tembeeni kifua mbele na pale mpakapoulizwa jibuni hoja kwani majibu mnayo”, alisema Mama Kikwete.

Mama Kikwete pia aliwataka wananchi hao kutunza amani, upendo na mshikamano uliopo ili waweze kufika mbali kimaendeleo kwani vitu hivyo wakivipoteza ni sawa na kupoteza lulu waliyonayo.

Amani ikitoweka hakuna jambo lolote litakalofanyika zaidi ya watu kukimbia huku na kule kunusuru roho zao, nchi zisizo na amani watu hawawezi kukusanyika kwa pamoja na kufanya mambo yao pamoja na demokrasia iliyopo nawashauri mjitahidi kuchagua vitu ambavyo vinamaslahi ya Taifa.

Alisema, “Hao wanaowashawishi ninyi mfanye vurugu mbona kwao kuna aman?, ni ukweli kuwa mikoa ya Kusini ilikuwa nyuma kimaendeleo lakini sasa neema imepatikana baada ya kuendelea mnataka kurudi nyuma jitahidini kuwa wazalendo na kutengeneza mazingira ya kujali kwenu kwa kufanya shughuli za maendeleo angalieni msiwe chanzo cha matatizo katika maeneo mnayotoka”.

Kwa upande wake Mlezi wa Chama hicho katika mkoa wa Lindi Dk. Maua Daftari aliwapongeza wanachama hao kwa kuweza kutekeleza ilani yao ambayo imeweza kuwasaidia kufika miaka 37 na kusema kuwa wasisikitike na maneno ya kashfa yanayotolewa na wapinzani kwani ndiyo siasa ya vyama vingi ilivyo nao kama vyama vingine wamepata mdomo wa kusemea.

“Serikali iliamua kuanzisha mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 ingawa katika kura zilizopigwa na wananchi asilimia 80 walikataa na asilimi 20 ya wananchi walikubali lakini ilifanyika hivi ili wananchi wengine waweze wafanye kazi kwa pamoja na Serikali kupitia vyama vyao vya siasa na hii ndiyo demokrasia ya kweli”, alisema Dk. Daftari.

Naye Mwenyekiti wa CCM wa mkoa huo Mzee Ali Mtopa aliwataka wapinzani waache tabia ya kukichafua chama hicho bali wakubali kuwa Serikali imefanya mambo mengi ya maendeleo na siyo kutukana viongozi waliopo madarakani bali kila mtu amwage sera za chama chake na siyo kashfa.

Wakati huohuo Katibu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wilaya ya Ruangwa Saidi Nng’umbanga ambaye alialikwa katika sherehe hizo aliipongeza CCM kwa kufikisha miaka 37 na kuwa chama cha Demokrasia kwa kuvishirikisha vyama vingine vya siasa katika mambo mbalimbali.

Nng’umbanga alisema mikusanyiko ya wana Lindi na Mtwara ni ishara kuwa katika mikoa hiyo kuna amani ya kutosha na hakuna uhasama miongoni mwa watu kwani wanakutana katika mambo mbalimbali ikiwemo sherehe, misiba na mikutano ya siasa .

Jumla ya wanachama waliojiunga katika wiki ya kilele cha sherehe hizo ni 1534 kati ya hao kutoka chama cha upinzani cha CHADEMA ni 29 na Civic United Front (CUF) 21 pia Chama hicho kimefanikiwa kuongeza idadi ya ofisi za kata hadi kufikia 142, matawi 1120 na mashina 11100 lengo likiwa ni kusogeza huduma karibu na wananchi.