RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa kampeni za kugombea kuteuliwa kuwa mgombea urais wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) hazijaanza rasmi.
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa vitendo vya baadhi ya watu kuanza kampeni kabla ya wakati wake ni moja ya mambo yanayosikitisha. Hata hivyo, Rais Kikwete amesema kuwa suala hilo limekabidhiwa kwa Makamu wa Mwenyekiti wa CCM (Tanzania Bara), Philip Mangula ambaye atalisimamia jambo hilo na kulishughulikia.
“Kuhusu kama kampeni za kuwania Urais zimeanza ni kwamba kampeni hazijaanza rasmi. Hili ni moja ya mambo yanayosikitisha. Lakini suala zima tumelikabidhi kwa Mzee Mangula ambaye atalisimamia na kulishughulikia,” Rais Kikwete alisema jana, Jumamosi, Februari Mosi, 2014.
Rais na Mwenyekiti wa CCM alikuwa anazunguza na wajumbe wa Halmashauri ya CCM ya Mkoa wa Mbeya kwenye Ukumbi wa CCM mjini Mbeya. Rais Kikwete yuko katika ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani Mbeya. Rais Kikwete alilizungumzia suala hilo baada ya kuwa ameulizwa moja kwa moja na Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Mbeya, Ndugu Godfrey Zambi ambaye alimtaka Mheshimiwa Rais na Mwenyekiti wa chama chake kufafanua kama kampeni zimeanza ama bado.