Mwenyekiti wa CCM Taifa Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiongoza matembezi ya mshikamano kutoka Soweto, Mwanjelwa, hadi Uwanja wa Sokoine, ikiwa ni moja ya shughuli za maadhimisho ya miaka 37 ya kuzaliwa kwa chama hicho tawala. PICHA ZOTE NA IKULU.
Mwenyekiti wa CCM Taifa Rais Jakaya Mrisho Kikwete akizungumza na wana CCM na wananchi waliojitokeza kwenye shughuli za maadhimisho ya miaka 37 ya kuzaliwa kwa chama hicho tawala katika Uwanja wa Sokoine.
Na Joachim Mushi
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete amewataka viongozi wa chama hicho kwenda kwa wanachama wakakisemee chama, kuwasikiliza wananchi na kutatua hoja na matatizo yao. Aliwataka pia wawe na utaratibu wa kufanya vikao vya chama mara kwa mara ili mambo yazungumzwe na maamuzi yafanye kiutekelezaji.
Mwenyekiti huyo ametoa kauli hiyo alipo kuwa akizungumza na wanachama wa CCM, wananchi na wapenzi wa chama hicho walioshiriki katika kilele cha maadhimisho ya Miaka 37 ya Chama Cha Mapinduzi yaliofanyika leo mkoani Mbeya katika Uwanja wa Sokonne uliopo jijini Mbeya. Alisema awali baadhi ya viongozi wa CCM walilalamikia suala la usafiri kuwafikia wanachama jambo ambalo tayari limetatuliwa kwa chama kununua magari kwa viongozi hao. “Mwanzoni baadhi ya viongozi walilalamikia hawana magari, sasa magari tumenunua nendeni kwa wanachama muwasikilize hoja zao kwani uhimara na uzima wa chama ni wanachama,” alisema Kikwete katika hotuba yake.
Aidha aliwataka viongozi kuziimarisha jumuiya anuai za chama, ikiwa ni pamoja na kudumisha umoja na mshikamano kama ilivyo kauli mbiu ya chama hicho kwa sasa ‘umoja ni ushindi’. Alisema uwezo na sifa za chama cha CCM kupata ushindi ni tashura za viongozi na ili taasisi hiyo iweze kufanya vizuri ina kila sababu viongozi na wanachama kufanya kazi ya ziada, alisema kinyume na juhudi hizo chama kitatumia nguvu kubwa kupata ushindi na pengine ushindi unaopatikana kuwa mwembamba.
Pamoja na hayo aliwataka viongozi kusimamia mapato ya chama vizuri ili mapato hayo yaweze kukiingizia chama fedha na kuepukana na fedha za kusaidiwa ambazo wakati mwingine waovu wachache hutumia mwanya huo na kuingiza fedha chafu.
“Siku hizi hata wanaotoa rushwa nao tunawapokea kishujaa…tusipokee tu bali waulizeni wanataka nini ndani ya chama tusimamie mapato na si kutegemea michango, ambayo wakati mwingine hata fedha chafu za michango hujikuta zinaingia, tuna vyanzo vya mapato ndani ya chama katika ngazi mbalimbali viongozi tuvisimamie kuongeza mapato ya chama,” alisema JK.
Aliongeza kuwa sera nzuri na utekelezaji wake ndio unakijenga chama na kuungwa mkono zaidi kwa wananchi, hivyo kuwataka viongozi kulipa uzito unaostahili suala la uadilifu na uaminifu wa viongozi na wanachama wake. Alisema kinyume na hapo chama hakiwezi kukubalika katika jamii, hivyo kuwataka viongozi kuondokana na tabia ya kutoa na kupokea rushwa ndani ya chama.
“Tusiache ikajengeka dhana potofu kwamba uongozi ndani ya chama ni kununua kama suruali, yaani ili kupata ushindi ndani ya chama ni kukusanya maburungutu ya fedha na kutumia katika uchaguzi. Kuimarisha chama ni pamoja na kufanya kazi za umma ndani ya chama kushirikiana na wananchi katika masuala mbalimbali,” alisema Kikwete.
Hata hivyo alimpongeza Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana pamoja na wajumbe wa sekretarieti ya chama hicho kwa juhudi za kukijenga na kuimarisha chama kupitia ziara zao mbalimbali nchini. “Ziara zinazofanywa na Katibu Mkuu kwa kweli zinakiletea sifa chama…anashiriki shughuli za wananchi na hata kutatua matatizo ya wananchi moja kwa moja,” alisema. Aidha aliongeza kuwa juhudi zao ndiyo zilisababisha mawaziri wanne wakaitwa na KamatiKkuu ya CCM kujibu hoja zilizoibuliwa. Hata hivyo kuitwa ndani ya chama kwa mawaziri hao si lazima wafukuzwe kazi kwani kinachotakiwa ni kusikiliza na kutatua tatizo lililopo.
“…Kwa kusimamia na kutekeleza maamuzi na ilani za chama, tufuatilie ahadi zilizotolewa na viongozi na kuhakikisha zinatekelezwa kwa wananchi ili kuepuka kuja kusutwa baadaye na wananchi. Tufanye kazi za chama. Utekelezaji wa ilani ya chama ndani ya serikali unaenda vizuri, huwenda machache yasifanye lakini haitakuwa kwa makusudi bali ni ufinyu wa bajeti haya tutaendelea kuyafanyia kazi,” alisema Kikwete.
Alisema Serikali imefanya kazi nzuri kwenye sekta ya elimu kama vifaa na nguvu kazi ya elimu, tumefanya vizuri pia kwenye sekta ya maji idadi kubwa inapata maji maeneo anuai. Alisema sekta ya afya napo serikali imejitahidi, vituo vya afya, zahanati na hospitali zimejengwa na kuboreshwa zaidi, wataalamu na upatikanaji wa dawa imeendelea kuboreshwa. Pia katika sekta ya miundombinu tumefanya vizuri, barabara, viwanja vya ndege zimejengwa kiasi kikubwa na kazi hii inaendelea.
Aliwapombeza wananchi na viongozi wa Mkoa wa Mbeya kuwa wanafanya vizuri kwenye sekta za elimu, afya, maji na miundombinu kama barabara na uwanja wa ndege sasa upo hapa, tena wa kimataifa tuutumie kwa biashara ili uweze kuwa na manufaa zaidi kwetu na taifa.
Aidha aliwataka viongozi wa upinzani hasa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuacha kuzua ugomvi bungeni kwani vitendo hivyo si suluhisho la utatuzi wa mambo. “…wala siamini kwamba mambo yakivurugika chama cha Chadema kitakuwa na maslahi zaidi.” Alisema Kikwete akihutubia.
Katika hotuba yake Mwenyekiti huyo wa Chama cha Mapinduzi, alizungumzia maandalizi ya Bunge la Katiba ambalo alisema wajumbe wake watakutana wiki tatu zijazo za Februari na wanatarajia kufanya majadiliano kwa siku 90 kuchambua Rasimu ya Katiba kabla ya kuipitisha ili iendelee na mchakato mwingine. Alisema majadiliano hayo ya wabunge watakuwa huru kujadiliana na kukubaliana kila hoja kwa mwongonzo wa rasimu iliyokabidhiwa kwao hivyo hakuna hujuma zozote zinaweza kupandikizwa kwa wajumbe wa katiba na mtu yoyote kwa maslahi yake.