*Ni kujadili namna ya kupunguza vifo vya wajawazito
Na Mwandishi Wetu
MUUNGANO wa Utepe Mweupe (White Ribbon Allience for Safe Motherhood Tanzania) wiki hii walikutana na Waziri Mkuu wa Tanzania, Mizengo Pinda na kujadiliana namna ya Serikali inavyoweza kuokoa maisha ya wajawazito hasa wakati wa kujifungua. Pia mkutano huo ulirejea ahadi ambazo zilishatolewa na serikali kwamba kufikia mwaka 2015 asilimia 50 ya vituo vyote vya afya nchini Tanzania vitakuwa vinatoa huduma za dharura zikiwemo upasuaji na damu salama kwa ajili ya kusaidia wajawazito nyakati za kujifungua.
Kupitia kampeni ya ‘Wajibika Mama Aishi’ iliyochini ya Muungano wa Utepe Mweupe inayolenga kuikumbusha Serikali ahadi yake ya kuhakikisha asilimia 50 ya vituo vya afya vinatoa huduma za dharura; walimuomba Waziri Pinda atoe agizo kwa Serikali kuweka kipengere cha huduma za dharura katika vituo vya afya na kutengewa bajeti mahususi kwenye bajeti ya Serikali ya mwaka 2014/15.
Takwimu zinaonesha kwa Tanzania kila siku wanawake 24 hupoteza maisha kutokana na matatizo ya uzazi. Lakini wanawake wengi wanaopata matatizo yanayosababisha kupoteza maisha, wangeweza kuokolewa pale tu wanapopata huduma za uzazi za dharura. Njia pekee ya kuepusha vifo visivyo vya lazima vitokanavyo na matatizo ya uzazi ni wanawake kupata kwa wakati huduma za dharura kama vile upasuaji na damu salama katika vituo vya afya wanakojifungulia pale inapobidi.
Katika Mkutano huo, Mkurugenzi wa Shirika la Evidence For Action Tanzania, Craig Ferrah alisema vifo 24 vya akina mama vinavyotokea kila siku nchini haina tofauti na ajali za kila siku za ndege na kuongeza kuwa ipo haja ya Serikali kuweka kuweka mkakati wa kukomesha ajali hizo ndani ya saa 48. Hata hivyo ombi kuu kutoka muungano huo kwa Waziri Mkuu lilikuwa Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa iagize kuwepo wa kipengele mahususi cha bajeti ya huduma za uzazi za dharura zikiwemo upasuaji na damu salama katika vituo vya afya kwenye bajeti ya mwaka 2014/2015.
Kwa upande wake Waziri Mkuu Pinda aliguswa na ukubwa wa tatizo hilo la vifo vya wajawazito nchini na kuelezea umuhimu wa kutafutia namna ya kukabiliana na tatizo ambalo linaelekea kuwa la kudumu. Waziri Pinda aliridhia moja kwa moja ombi kutokana na kuguswa na takwimu zilizotolewa juu ya vifo vya wajawazito na kukubali kuwa Serikali itatenga bajeti mahususi ambayo itaelekezwa kuhimarisha vituo vya afya nchini ili viweze kutoa huduma ya dharura yaani damu salama, upasuaji pamoja na wataalamu na vifaa kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi.
Mkutano huo pia ulihudhuriwa na wawakilishi kutoka mashirika ya; Jhpiego, CARE, Plan International (Wazazi na Mwana), Evidence4Action, Medical Women Association of Tanzania na Chama cha Wakunga Tanzania walihudhuria kama sehemu ya Muungano wa Utepe Mweupe (White Ribbon Allience for Safe Motherhood Tanzania).