VITA ya urais kupitia CCM inazidi kushika kasi baada ya Makamu Mwenyekiti Mstaafu wa chama hicho, John Malecela kuutaka uongozi kumchukulia hatua Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kwa kuanza mapema kampeni. Kauli hiyo imekuja siku chache baada ya Katibu wa Uhamasishaji na Chipukizi wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Paul Makonda kumtuhumu Lowassa kuwa anakiyumbisha chama hicho kutokana na kampeni za kutaka kuwania urais wa 2015.
Katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika nyumbani kwake mjini Dodoma jana, Malecela alisema Sekretarieti ya CCM inapaswa kuwachukulia hatua kali makada wanaojipitisha maeneo mbalimbali nchini kwa nia ya kusaka urais, kabla ya chama hicho kupanga muda.
Aliwafananisha walioanza mbio za urais kupitia CCM na watu wanaowahi kukimbia kabla ya kipenga kupigwa na kusema hawawezi kupimwa sawa na wale wanaosubiri kuanza rasmi kwa kampeni. Alimpongeza Makonda kwa ujasiri wa kukemea hatua hiyo ya Lowassa bila woga.
Alipoulizwa juu ya suala hilo, Lowassa alijibu kupitia msaidizi wake kuwa hana la kusema. “Nimezungumza na Mheshimiwa Lowassa juu ya suala hilo lakini amenituma niwaambie kuwa hana ‘comment’ (hana la kusema),” alisema msaidizi wake huyo.
Fulana hadharani
Alipoulizwa swali la kwa nini ameamua kumtaja Lowassa pekee huku kukiwa na makada wengi wanaojipitisha kupiga kampeni za urais, kabla ya kujibu, Malecela ambaye aliwahi kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais na Waziri Mkuu, aliingia ndani ya nyumba yake na kutoka akiwa ameshikilia mfuko uliokuwa fulana mbili.
Alitoa fulana hizo, moja ikiwa na rangi nyeusi na kahawia na nyingine yenye rangi nyekundu na nyeupe zikiwa zimeandikwa ‘Friends of Edward Lowassa’ (Marafiki wa Edward Lowassa).
“Hivi kuna mwingine aliyefanya hivi? Na hizi zimegawiwa nchi nzima. Ehhh! Hivi kuna mwingine kafanya hivi? Sijui, niongezee nini tena zaidi ya hapo,” alisema Malecela huku akionyesha fulana hizo.
Malecela ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza la Ushauri la Taifa la CCM, alisisitiza kuchukuliwa kwa hatua haraka kwa vitendo hivyo akisema harakati za Lowassa kuwania urais kupitia chama hicho zimesababisha mgawanyiko.
“Jinsi tunavyochelewa kuchukua hatua ndivyo tunavyoweza kuleta mpasuko ndani ya chama. Hapa najiuliza, ile misingi imara ya uongozi ndani ya Chama Cha Mapinduzi iko wapi? Mpaka tumwachie mtoto (Makonda) akemee haya? Je, hapa chama kiko wapi?” alisema.
Alitahadharisha kuwa chama kisipotoa karipio au tamko kuhusu suala hilo, wanaotumia fedha kwa lengo la kutafuta umaarufu na ushawishi ili kupata madaraka wataharibu misingi bora ya uongozi iliyowekwa na waasisi wa CCM.
“Kinachonisikitisha zaidi ni kuona juhudi za uongozi wa sasa wa chama ngazi ya juu ikiwa ni pamoja na sekretarieti inayoongozwa na Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana na Katibu Mwenezi Nape Nnauye za kutetea chama hiki zinatiwa mchanga,” alisema na kuongeza kuwa juhudi hizo zisibezwe.
Malecela aliishauri Sekretarieti ya CCM kuchukua hatua mara moja, kwa maelezo kuwa Makonda asingesema hayo yote kama hana uhakika wa ushahidi.
Alisema waasisi wa chama hicho walikijenga kwa tabu na hakuna aliyediriki kutumia fedha kutaka madaraka… “Nidhamu, busara na uchungu wa rasilimali za taifa hili kwa masilahi ya wananchi ndivyo vilivyotuongoza kufuata misingi na maadili ya uongozi ndani ya chama na Serikali.”
Alisema vijana na wanachama wa CCM wanataka kujua msimamo wa chama chao. Akizungumzia kauli hiyo ya Malecela, Nnauye alisema: Tumemsikia, ushauri wake tutaufanyia kazi.” Hakutaka kuzungumzia zaidi suala hilo.
Tangu Lowassa ambaye pia ni Mbunge wa Monduli kuandaa hafla kubwa kusherehekea Mwaka Mpya nyumbani kwake Monduli ambako alitangaza kuanza rasmi safari aliyoiita ya matumani ya ndoto zake, ambayo pia itatimiza ndoto za Watanzania za kupata elimu bure, majisafi na maendeleo ya uhakika, makada wa chama hicho wameingia katika malumbano makubwa.
Malumbano hayo ambayo Malecela amesema hayana tija kwa chama na hayaleti umoja na mshikamano ambao umekuwapo kwa miaka mingi, yalipamba moto baada ya hivi karibuni baadhi ya wenyeviti wa mikoa wa chama hicho, wakiongozwa na Mwenyekiti wa Geita, Joseph Kasheku ‘Msukuma’ kumjia juu Mwenyekiti wa Singida, Mgana Msindai kwa kudai wenyeviti wote walikuwa wanamuunga mkono Lowassa.
Hata hivyo, Msindai ambaye pia ni Mwenyekiti wa wenyeviti wa CCM wa mikoa, alikanusha kutoa kauli hiyo kwa maelezo kwamba alikuwa akiwazungumzia wenyeviti aliokuwa amefuatana nao Monduli katika hafla hiyo.
CHANZO: Mwananchi