Na Eliphace Marwa-Maelezo
UBALOZI wa China nchini Tanzania kwa kushirikiana na makampuni ya watu wa China nchini wametoa msaada wa vitu mbalimbali kwa waathirika wa mafuriko mkoani Morogoro toka kwa, Lu Youqing, vyenye thamani ya sh. milioni 30.
Msaada huo umetolewa na Balozi wa China nchini Tanzania, Lu Youqing na ulikabidhiwa kwa Mkurugenzi wa Idara ya Maafa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Luteni Jenerali Sylivester Rioba akipokea msaada huo kwa niaba ya serikali amesema kuwa anaishukuru Serikali ya China kwani imekuwa mstari wa mbele pale Tanzania inapopata maafa mbalimbali.
Aidha Luteni Jenerali Rioba aliongeza kuwa mafuriko hayo ya aina yake hayajawi kutokea yalianzia milima ya Kilosa na Mvomero na kupelekea kufurika kwa mto Mkundi.
“Mheshimiwa Balozi mvua hizi zilikuwa kubwa ambazo hazijawahi kutokea wilayani Mvomero na kupelekea kuharibu daraja la Dumila ambalo ndiyo kiunganishi cha Mkoa wa Morogoro na Dodoma,” alisema Luteni Jenerali Rioba.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Antony Mtaka akiongea kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro amesema kuwa mamia ya nyumba ikijumuisha madarasa, majengo ya mahakama ya mwanzo, mashamba na barabara zimeharibiwa vibaya na mafuriko hayo.
“Kwa niaba ya Serikali napenda kushukuru Serikali ya China kupitia, Balozi Lu kwa msaada huu na ningependa kuahidi kuwa msaada huu utawafikia walengwa kama ilivyokusudiwa,” alisema Mtaka.
Kwa upande wake Balozi wa china ametoa pole kwa waathirika wa mafuriko na kusema kuwa watu wa Jamhuri ya China wako pamoja nao katika kipindi hiki kigumu.
“China na Tanzania ni marafiki wa muda mrefu hivyo kampuni ya ujenzi ya CCECC ilichukua hatua za haraka katika kushiriki ujenzi wa daraja hilo kwa kushirikiana bega kwa bega na ndugu zao Watanzania kwa kufanya kazi usiku na mchana na kumaliza ujenzi huo kwa muda wa siku mbili,” alisema Balozi Youqing.
Ubalozi wa China kwa kushirikiana na makampuni ya China nchini umetoa vitu mbalimbali ikiwemo Chakula, mashuka, madawa na maturubahi ikiwa ni sehemu ya mchango wao kwa waathirika hao wa mafuriko mkoani Morogoro.