Obama Aapa Kuizunguka Congress

Rais Obama akitoa hotuba yake kuhusu hali ya taifa.

Rais Obama akitoa hotuba yake kuhusu hali ya taifa.

RAIS wa Marekani, Barack Obama ameapa kulizunguka bunge na kuchukua hatua kivyake ili kuwaimarisha watu wa tabaka la kati, akionyesha kukatishwa kwake tamaa na kasi ndogo ya kutunga sheria kwa upande wa bunge hilo.

Katika ujumbe wake kwa Bunge la Congress kupitia hotuba yake ya kila mwaka kwa taifa, Obama aliahidi kuchukua hatua kukabiliana na ongezeko la ukosefu wa usawa, hata ikimbidi kufanya hivyo bila uungwaji mkono wa bunge, huku akiwataka wabunge kuweka pembeni tofauti za kisiasa na kufanya kazi kwa maslahi ya raia na kulipeleka mbele taifa hilo.

Rais Obama alisema nchi hiyo laazima iondokane na mawazo ya kupigana vita mara kwa mara ili kutoa fursa kwa diplomasia kutatua matatizo sugu ya ulimwengu, kama vile mgogoro wa nyukilia wa Iran. Obama pia alitoa wito wa kuchukuliwa hatua za dhati kuufufua uchumi wa Marekani, na kukabiliana na ukosefu wa usawa na kupanua fursa kwa raia wote wa taifa hilo.

“Tuufanye mwaka huu kuwa mwaka wa kuchukuwa hatua. Hilo ndilo Wamarekani wengi wanalolitaka. Kwetu sote katika jumba hili, kuyajali maisha, matumaini na matarajio yao, na ninachoamini kinawaunganisha watu wa taifa hili bila kujali rangi, dini au chama wanakotoka, wadogo kwa wakubwa, matajiri na maskini, ni imani yao ya juu katika fursa kwa wote,” alisema rais Obama aliekuwa akishangiliwa mara kwa mara na hadhira yake.

Hotuba ya Obama ilijikita hasa juu ya uchumi, mabadiliko ya tabianchi, mageuzi katika sera ya uhamiaji, Afghanistan na gereza la Guantanamo, Iran na kima cha chini cha mshahara. Hatua za Obama, ingawa zilionekana za kawaida, kwa pamoja ziliashiria kukatishwa tamaa kutokana na kasi ndogo ya kutunga sheria katika baraza la wawakilishi “Congress” linalodhibitiwa na chama cha Republicans, walio na uwezo wa kupunguza kasi ya ajenda ya rais.

Alilitaka bunge kupandisha kima cha chini cha mshahara kutoka kiwango cha sasa cha dola 7.25 kwa saa hadi dola 10.10, huku akiyatolea wito makampuni pia kupandisha viwango vya mishahara na kuwalipa wanawake zaidi ya centi 77 wanazolipwa sasa kwa kila dola moja anayopata mwanaume, jambo aliloliita “fedheha.”

Baadhi ya amri alizotangaza Obama katika hotuba hiyo ni pamoja na kupandisha kima cha chini cha mshahara kwa wafanyakazi wapya wa mikataba wa serikali ya shirikisho, na kuanzisha kwa akaunti za akiba kuwasaidia mamilioni ya watu kujiwekea akiba kwa ajili ya kustafu kwao, na mipango ya kuanzisha viwango vipya vya ufanisi wa mafuta kwa magari makubwa.

Alilitolea wito bunge kuruhusu majadiliano ya biashara kupitia kile kinachojulikana kama sheria ya kuharakisha, akisema ushirikiano mpya wa kibiashara kati ya Ulaya na Asia utasaidia kuunda nafasi zaidi za ajira. Obama alisema mageuzi katika sheria ya uhamiaji ni muhimu kwa uchumi, na kuongeza kuwa mageuzi hayo yanaweza kusaidia bajeti kwa kupunguza matumizi na kuongeza mapato yatokanayo na kodi.

Alisema pamoja na ukweli kwamba Marekani inaendelea kukabiliana na mitandao ya kigaidi kupita juhudi zinazolenga shabaha makhsusi na kujenga uwezo wa mataifa washirika, taifa hilo halipaswi kufikiria mara zote katika vita. Obama alizungumzia mafanikio ya kidiplomasia ya hivi karibuni chini ya waziri wa mambo ya nchi za kigeni, John Kerry, kuiondolea Syria silaha za kemikali, na kuanzisha tena mazungumzo kati ya Israel na Wapalestina.

Aliwataka wabunge kutoiwekea vikwazo zaidi Iran, ili kutoa muda kwa mazungumzo kati ya taifa hilo la Kiislamu na mataifa makubwa sita. Akijibu ukosoaji wa wabunge juu ya kuzungumza na Iran, Obama alisema Marekani iko makini, na kwamba makubaliano yoyote hayatajengwa kwa misingi ya kuaminiana tu, bali kwa hatua zinazothibitika kwamba Iran hailengi kutengeneza bomu la nyuklia.

Rais huyo alizungumzia kwa muhtasari hali nchini Syria, na kusema utawala wake utaendelea kufanyia kazi mustakabali wanaostahiki watu wa Syria, usio na udikteta, vitisho wala hofu. Alisema wakati vita vya Afghanistan vikikaribia mwisho, huu unapaswa kuwa mwaka wa kuondoa vikwazo vilivyosalia kuhusu uhamishaji wa wafungwa, na kulifunga gereza la Marekani la Guantanamo lililoko katika ardhi ya Cuba.