Nchi Zaidi za Afrika Kujiunga na APRM

Bw. Hassan Abbas, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano katika APRM Tanzani.

Bw. Hassan Abbas, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano katika APRM Tanzani.

Na Mwandishi Wetu

WAKATI viongozi wan chi za Umoja wa Afrika wanachama wa Mpango wa Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM) wakikutana mjini Addis Ababa, Ethiopia Januari 29, 2014, nchi nne zinatarajiwa kujiunga. Kwa mujibu wa taarifa ya APRM Tanzania iliyotolewa jana, nchi hizo zinazotarajiwa kujiunga katika mkutano huo wa 20 wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa APRM ni Cape Verde, Ivory Coast na Guinea ya Ikweta.

“Kujiunga kwa nchi hizi ni hatua nzuri katika kuifanya APRM kuzidi kuwa chombo muhimu cha kuziunganisha Serikali za Afrika na wananchi wao,” alisema Bw. Hassan Abbas, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano katika APRM Tanzani.

Aliongeza kuwa nchi inaposaini mkataba wa kujiunga na APRM hutakiwa kuanza mara moja mchakato wa kuanzisha taasisi huru katika nchi husika, kuelemisha wananchi kuhusu ushiriki wao katika tathmini ya utawala bora na kisha kufanyika kwa tathmini husika. Mbali ya tukio la kujiunga kwa nchi hizo mkutano huo wa 20 wa Wakuu wa Nchi za APRM utajadili pia masuala mbalimbali juu ya utekelezaji wa utawala bora Barani Afrika.
 
“Mkutano huu ni muhimu pia kwa sababu msingi mkuu wa APRM ni kuhamasisha na kuchagiza uboreshaji wa utawala bora katika nchi mbalimbali. Katika mkutano huu viongozi wa nchi za APRM watajadili namna baadhi ya nchi zilivyotekeleza changamoto zilizobainishwa huko nyuma,” alisema.
 
Alizitaja nchi za Afrika Kusini, Benin, Sierra Leone, Msumbiji na Burkina Faso kuwa zimepangiwa kuwasilisha ripoti zao za utekelezaji ili kuwaeleza viongozi wenza juu ya hatua walizochukua kutokana na mapendekezo waliyopewa awali na changamoto walizokumbana nazo.
 
“Mikutano hii huhusisha wakuu wenyewe wa nchi zote 34 za APRM ambapo hushiriki katika kubaini changamoto zinazozikabili nchi wenza na hivyo kushauriana juu ya namna ya kuzikabili lakini pia kubaini mambo ya kuigwa kutoka nchi wenza ili kujifunza na kuyachukua kuboresha utawala bora katika nchi zao,” alisema Bw. Abbas.
 
Tanzania ni miongoni mwa nchi 34 za Umoja wa Afrika zinazoshiriki katika Mpango wa APRM na tayari ilikwishakamilisha ripoti yake ya kwanza ambayo imeanza kufanyiwakazi kwa Serikali kutekeleza Mpango wa kuondoa mapungufu ya kiutawala bora yaliyobainishwa.