SERIKALI na waasi wa Sudan Kusini wamesaini makubaliano ya kusitisha mapigano, japokuwa wachambuzi wa mambo wanasema bado kuna kazi kubwa ya kuwadhibiti wapiganaji na kutekelezwa kwa makubaliano ya mkataba huo.
Makubaliano hayo yaliyosainiwa Mjini Addis Ababa, Ethiopia, Januari 23, 2014 na pande zote za mzozo kwa kukubaliana kumaliza mapigano yaliodumu takribani kwa wiki tano ambayo yamesababisha vifo vya maelfu ya watu. Mkuu wa ujumbe wa waasi kwenye mazungumzo hayo, Taban Deng, ameyaita makubaliano hayo kuwa ni chachu “itakayoandaa mazingira ya mdahalo wa kisiasa na ambao utafungua njia ya amani ya kudumu.”
Mkuu wa ujumbe wa serikali, Nhial Deng Nhial, alisema mazungumzo hayo yaliyokuwa yakisuasua kwenye hoteli moja ya kifahari mjini Addis Ababa hayakuwa rahisi.
“Tunatarajia kuwa tutaweza kupiga hatua kuelekea makubaliano kamili ambayo yatamaliza umwagaji damu,” alisema Nhial, lakini akaonesha wasiwasi wake juu ya uwezo wa waasi, ambao miongoni mwao ni vikosi vya kijeshi, wanamgambo wa kikabila na watu wa kawaida, kuweza kusimamisha ghasia.
Hatua ya wawakilishi wa Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini na wale wa hasimu na makamu wake wa zamani, Riek Machar, kuweka saini zao kwenye hati hiyo ilipokewa fursa na wapatanishi, wanadiplomasia na jumuiya ya kimataifa.
Rais Barack Obama wa Marekani, ambaye nchi yake iliwahi kuunga mkono kwa hali na mali juhudi za Sudan Kusini kuwa huru, ameyaelezea makubaliano hayo kama “hatua muhimu ya kwanza kuelekea utafutaji wa amani ya kudumu.”
Rais Obama alisisitiza kwamba “Viongozi wa Sudan Kusini wanapaswa kuyatekeleza kikamilifu na haraka makubaliano hayo na kuanza mdahalo wa kisiasa unaowajumuisha wote ili kutatua chanzo cha mgogoro.”
Wapatanishi kutoka Jumuiya ya Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki na Pembe ya Afrika (IGAD) walisema makubaliano hayo yataweka chombo cha usimamizi na ufuatiliaji wa utekelezwaji na kuwaruhusu wafanyakazi wa misaada kufanya kazi zao kwa uhuru.
Vile vile, serikali ya Sudan Kusini imekubali kuwaachia wanasiasa 11, washirika wa Machar, ambao waliwekwa kizuizini baada ya mapigano kati ya makundi hasimu ya wanajeshi kuanza siku ya Disemba 15, ingawa hakukutolewa tarehe rasmi ya kuachiwa kwao.
Suala la mahabusu hao ilikuwa mada iliyoleta mkwamo kwenye mazungumzo hayo na Obama alisisitiza kwamba ushirikia wao ungelikuwa “muhimu” sana kwenye utafutaji wa makubaliano katika siku zijazo. Katika wiki tano za mapigano haya, wachambuzi na wafanyakazi wa misaada wanaamini kwamba zaidi ya watu 10,000 wameuawa na wamezilaumu pande zote mbili za mzozo huo kwa kuhusika na utesaji na mauaji ya makusudi.
Zaidi ya watu 500,000 wamelazimika kuyahama makaazi yao wakati wa wimbi la ghasia za kikabila kwenye taifa hilo jipya na fukara. Baada ya mapigano ya awali kuzuka kwenye mji mkuu Juba zaidi ya mwezi mmoja uliopita, mgogoro ulisambaa haraka na kuwa vita kamili kati ya jeshi lililoungwa na wanajeshi wa Uganda na wanajeshi walioasi wakishirikiana na makundi ya wanamgambo.
Ghasia hizo zilichukua sura ya kikabila pale watu wa jamii ya Dinka, ambalo ni kabila la Kiir, walipopambana na jamii ya Nuer, kabila la Machar, hali iliyopelekea maelfu kusaka hifadhi kwenye vituo vya walinda amani vya Umoja wa Mataifa nchini humo.
-DW