WATU 22 wamefariki dunia wakiwemo watoto 3 na zaidi ya 30 kujeruhiwa baada ya magari waliyokuwa wakisafiria kupata ajali katika mikoa ya Singida na Lindi. Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete ametuma salamu za rambirambi akionesha kusikitika kwa ajali hizo.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo mtandao huu umezipata ajali ya kwanza imetokea Mkoani Singida eneo la la Isuna ambapo imehusisha gari aina ya Toyota Noah na lori kugongana uso kwa uso na kuua watu 13 akiwemo mtoto wa miezi mine. Taarifa zinasema gari hilo Toyota Noah lililokuwa limebeba abiria likitokea Itogi kwenda Singida.
Ajali nyingine imetokea Mkoani Lindi katika Kijiji cha Mambulu ambapo basi linalofanya safari zake kutoka Dar es Salaam kuelekea Mtwara lilianguka na kuuwa watu 9 wakiwemo watoto wadogo wawili. Taarifa za awali zinasema ajali hiyo ilitokea baada ya basi hilo kupishana na lori la mizigo kisha kuyumba na kupoteza uelekeo kabla ya kupinduka. Mashuhuda walisema hata hivyo ajali imechangiwa na mvua iliyokuwa ikinyesha.
Katika salamu za rambirambi za Rais Kikwete kwa Mkuu wa Mkoa wa Singida, Perseko Kone kutokana na vifo vya watu wazima 13 akiwemo mtoto wa miezi minne iliyotokea katika eneo la Isuna Mkoani Singida; amesema.
“Nimeshtushwa, nimesikitishwa na kuhuzunishwa mno na taarifa za vifo vya watu 13 akiwemo mtoto wa miezi minne waliofariki papo hapo katika eneo la ajali tarehe 20 Januari, 2014 baada ya gari aina ya Toyota Noah walilokuwa wakisafiria kutoka Itigi kwenda Singida kugongana uso kwa uso na lori katika eneo la Isuna”.
Rais Kikwete amesema inatia simanzi kuona ajali zikiendelea kutokea na kupoteza maisha ya watu wasio na hatia na hususan mtoto mdogo kama huyu wa miezi minne, kusababisha ulemavu wa kudumu kwa baadhi ya watu na uharibifu wa mali kutokana na makosa ya binadamu katika uendeshaji wa vyombo vya moto.
“Kufuatia ajali hiyo ya kusikitisha, ninakutumia wewe Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mheshimiwa Perseko Kone salamu zangu za rambirambi kutokana na msiba huo, na kupitia kwako, naomba unifikishie salamu zangu za rambirambi na pole nyingi kwa familia zote zilizopoteza wapendwa wao katika ajali hiyo. Nawaomba wanafamilia wawe na moyo wa uvumilivu, subira na ujasiri hivi sasa wanapougulia machungu ya kupotelewa na ndugu zao”, amesema Rais Kikwete kwa masikitiko.
Aidha Rais Kikwete amesema anamuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema azipokee na kuzilaza Mahala Pema Peponi Roho za Marehemu wote, na amewahakikishia wafiwa kuwa yuko pamoja nao katika kuomboleza msiba huu mkubwa.
Vilevile amemtakia ahueni kijana mmoja majeruhi wa ajali hiyo na aweze kupona haraka na kurejea katika hali yake ya kawaida na kuungana tena na ndugu na jamaa zake.