MAZUNGUMZO ya amani nchini Syria ambayo yanatarajiwa kufanyika baadaye wiki hii yamekumbwa na sintofahamu, baada ya Umoja wa Mataifa (UN) kuialika Iran kushiriki katika mazungumzo huku upande wa upinzani ukitishia kuyasusia kutokana na mwaliko huo.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ameialika Iran kwenye mazungumzo ya Montreux. Mwaliko huo kwa Iran umetangazwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon katika mkutano na waandishi wa habari mjini New York. Katibu Mkuu Ban alisema amefikia uamuzi huo baada ya mazungumzo ya kina na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Iran, Javad Zarif.
“Waziri wa mambo ya nchi za nje Javad Zarif ameahidi kuwa nchi yake itatoa mchango wa maana katika mazungumzo mjini Montreux. Kwa hiyo, kama mwandaaji na mwenyeji wa mazungumzo hayo, nimeamua kuialika Iran kuwa mmoja wa washiriki.” Alisema katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa.
Ban Ki-moon alisema amekubaliana na waziri Zarif kuwa lengo la mazungumzo ya Montreux ni kuunda serikali ya mpito nchini Syria, ambayo itakubaliwa na wote, na itakuwa na madaraka kamili ya uongozi wa nchi.
Muungano wa upinzani Syria ulikuwa umeafikiana kuhudhuria mazungumzo lakini mara baada ya tangazo la Umoja wa Mataifa kuialika Iran, muungano wa upinzani nchini Syria umetishia kuyasusia mazungumzo hayo hadi pale Umoja wa Mataifa utakapobatilisha mwaliko huo kwa Iran. Kauli hiyo ya muungano wa upinzani nchini Syria imetolewa na msemaji wa muungano huo Louay Safi kupitia mtandao wa kijamii, Twitter.
Marekani pia imeingilia kati, ikiitaka Iran kukubaliana na msimamo uliowekwa katika mkutano wa awali, kuwa rais Bashar al-Assad asishirikishwe katika serikali ya mpito kama sharti la kupata nafasi katika mkutano ujao. Ikiwa Iran itakwenda katika mkutano huo, sherehe za ufunguzi wake zitazileta pamoja nchi 40 na jumuiya za kikanda, na itakuwa hatua kubwa zaidi katika juhudi za kidiplomasia kutaka kuvimaliza vita vya Syria.
Mwaliko wa Umoja wa Mataifa kwa Iran umetolewa siku moja baada ya muungano wa waasi kuthibitisha ushiriki wao katika mazungumzo ya amani ambayo yamepachikwa jina la Geneva II, uamuzi ambao ulisifiwa na viongozi mbalimbali wa dunia.
Marekani na nchi nyingine za magharibi zimekuwa zikipinga kushiriki kwa Iran katika mazungumzo ya kutafuta amani nchini Syria, wakati wote itakapokuwa haijatia saini yake kwenye makubaliano ya mkutano wa kwanza wa Geneva, ambao ulifanyika tarehe 30 Juni mwaka 2012, ambayo yalitaka kuwepo kwa serikali ya mpito nchini Syria.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje ya Marekani, Jen Psaki, amesema nchi hiyo inauchukulia mwaliko wa katibu mkuu Ban Ki-moon, kama sharti kwa nchi hiyo kuunga mkono kikamilifu na wazi wazi, makubaliano hayo ya mwaka 2012 mjini Geneva.
Hata hivyo, hadi mwaliko wa Umoja wa Mataifa ulipotolewa, Iran imekuwa ikisisitiza kuwa itashiriki kwenye mazungumzo hayo iwapo itaalikwa bila kuwekewa masharti. Ban Ki-moon ambaye ameungana na Urusi kutaka Iran iwepo katika mazungumzo ya baadaye wiki hii, amesema anatarajia baadaye Iran itatoa tamko. Nchi nyingine ambazo zimepokea mwaliko wa dakika ya mwisho kutoka Umoja wa Mataifa ni Australia, Bahrain, Ubelgiji, Ugiriki, Luxembourg, Mexico, Uholanzi, Korea Kusini na Vatican.
-DW