Pinda Aridhishwa na Ukarabati Jengo la Bunge la Katiba

Waziri Mkuu Mizengo Pinda akikagua sehemu ya ukumbu wa Bunge la Katiba.

Waziri Mkuu Mizengo Pinda akikagua sehemu ya ukumbu wa Bunge la Katiba.


WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amesema ameridhishwa na kazi ya ukarabati inayoendelea kwenye maeneo mbalimbali ya jengo la Bunge ikiwa ni maandalizi kwa ajili ya Bunge la Katiba.

“Maendeleo ni mazuri na kazi inayofanywa ni nzuri, kikubwa ni kuhakikisha mnaikamilisha hii kazi katika muda uliopangwa,” alisisitiza.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo Januari 18, 2014, wakati akipokea maelezo ya ukarabati kutoka kwa Mhandisi Mkuu wa Ofisi Bunge, Eng. Dk. Philemon Mzee ambaye alikuwa akimtembeza kwenye maeneo mbalimbali yanayofanyiwa ukarabati. Kwa mujibu wa Dk. Mzee, kazi hiyo inatarajiwa kukamilika Januari 30, mwaka huu. Ndani ya ukumbi wa Bunge, Waziri Mkuu alikuta viti vyote vya zamani vimekwishaondolewa na akaonyeshwa sehemu moja ya mfano iliyopangwa viti vinane kuashiria muonekano utakavyokuwa mara baada ya kazi hiyo kukamilika.

Dk. Mzee alimweleza Waziri Mkuu kwamba wanatarajia kuweka viti 670 vya wajumbe wa kawaida pamoja na viti 24 kwa ajili ya wajumbe wenye mahitaji maalum. “Kule nyuma tutaweka viti vya kuzunguka ili hata kama mjumbe mmoja ana ulemavu wa miguu na amekuja na baiskeli yake aweze kutoka na kukaa kwenye kiti chake kwa urahisi,” alisema.

Alimweleza Waziri Mkuu kwamba viti vya Spika na Makatibu wa Bunge vipo tayari, mfumo wa vipaza sauti uko sawa na kwamba kila kipaza sauti kimoja kitakuwa kinatumiwa na watu wawili kulingana na mpangilio wa ukaaji ulivyo. Alipoulizwa na Waziri Mkuu kuhusu sehemu ya kukaa waandishi wa habari, Eng. Mzee alisema sehemu zao zitaendelea kubaki zilivyo. Alipohoji endapo kutakuwa na kazi za Kamati, zitafanyikia wapi, Waziri Mkuu alijibiwa kwamba kuna kumbi tisa za kutosha watu 25-30 zinaandaliwa katika jengo la utawala Annex.

Waziri Mkuu pia alikagua sehemu ya mgawaha kwa ajili ya wajumbe wa bunge hilo na kuonyeshwa sehemu ya basement ambayo alikuta inafanyiwa matengenezo ili iweze kuchukua watu 500 kwa wakati mmoja. Pia alikagua mgahawa wa zamani wa bungeni na kuelezwa kwamba utatumiwa na watumishi tu na hivi sasa unafanyiwa ukarabati ili uweze kutosha watu 120 kwa wakati mmoja.

Waziri Mkuu alikagua pia chumba cha Hansard ambako alielezwa kuwa kimeongezwa ili kiweze kutosha watumishi 80 ikilinganishwa na watumishi 25 waliokuwepo zamani. Pia alikagua server room ambayo imehamishiwa eneo yalipokuwa matawi ya benki na zahanati.

Alipouliza kuhusu eneo la kuegeshea magari, Waziri Mkuu alielezwa kwamba limetengwa eneo la kutosha magari 400 ambalo hivi sasa linafanyiwa maandalizi. Katika jengo la Utawala Annex, Waziri Mkuu alielezwa jengo hilo litakuwa na ofisi, vyumba vya mazoezi (gym), zahanati na ofisi za kutolea huduma za kibenki.

Akitoa maelezo kuhusu kazi ya ukarabati inayoendelea, Kamishna Msaidizi wa Magereza ambaye ni msimamizi wa ujenzi wa jengo la Utawala Annex, Eng. Salum Omari alisema walianza kazi hiyo Januari 2, mwaka huu na wanatarajia kuikamilisha ifikapo Februari 2, mwaka huu. Alipoulizwa kama watamudu kuikamilisha kazi hiyo katika tarehe iliyopangwa, Eng. Omari alimhakikishia Waziri Mkuu kwamba wataikamilisha katika muda huo.