Baadhi ya wabunge wa CCM wakiwa bungeni Dodoma.
Dodoma
VUGUVUGU la kuondolewa kwa Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini, lilianzia ndani ya kikao cha wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambapo walivutana vikali kabla ya kuazimia kuitoa bungeni bajeti hiyo.
Vyanzo vya habari kutoka katika mkutano huo uliofanyika mjini Dodoma siku moja kabla ya Serikali kuiondoa bungeni bajeti hiyo; vilisema hali ilikuwa mbaya ndani ya kikao hicho baada ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kutaka wakubaliane kuipitisha bajeti hiyo kutokana na wingi wao.
Hata hivyo walishindwa kukubaliana kutokana na upepo wa kisiasa ulivyo bungeni huku wananchi wakiendelea kutaabika na mgawo wa umeme uliopo nchi nzima kwa sasa.
Chanzo chetu kilisema Waziri Mkuu aliwasilisha hoja mbili za kuiondoa bajeti hiyo ama wabunge wakubaliabe kwa pamoja kuipitisha, lakini wajumbe waking’ang’ania hoja ya kwanza ya kuiondoa.
Akizungumza katika kikao hicho, Mbunge wa Simanjiro, Christopher ole Sendeka alisema lazima bajeti hiyo iondolewe na jambo la msingi ni kuangalia nani anaweza kuiondoa bungeni.
Baada ya hapo walikubaliana Waziri Mkuu ndiye azungumze hali halisi iliyopo na kasha, Waziri wa Wizara hiyo, William Ngeleja ndio aiondoe.
Sendeka alisema umeme utafutwe kwa namna yoyote ili kuwaondoa watanzania hapa waliopo hivi kutokana na shughuli zao za uchumi kudidimia.
“Hali yam le ndani haikuwa nzuri, watu walikuwa wamechachamaa, ole Sendeka, alisema umeme lazima utafutwe kwa njia yoyote bila kuzingatia ni kampuni gani itasaidia kufanikisha jambo hilo, kama ni IPTL au Symbioni,” kilisema chanzo hicho.
Chanzo hicho kilisema Mbunge wa Mbozi Mashariki, Godfrey Zambi (CCM), alisema kuna tatizo kubwa la umeme.
“Lakini nimejaribu kuangalia kwenye kitabu cha bajeti nimeona kuna fedha za kununulia magari na matumizi mengine, hivyo magari hayo kwa mwaka huu yasinunuliwe na fedha hizo zitumike kuhakikisha umeme unapatikana,” alisema Zambi.
Mbunge wa Viti Maalum, Margret Sitta alisema Serikali mbona huwa inanunua ndege, sasa kwanini ishindwe kununua mitambo ama majereta ya kuzalisha umeme haraka iwezekanavyo. Baadaye walikubaliana hoja hiyo iondolewe lakini wasitaje muda maalum wa kuirudisha.
Mbunge wa Kilindi, Beatrice Shellukindo (CCM), alisema yeye alichukua uchukua uamuzi wa kulipeleka suala hilo bungeni ili kukisafisha chama chake ambacho kimeanza kupoteza mwelekeo.
“Mimi nimefuatwa mpaka saa nne usiku na watu wakiwa na bahasha lakini mimi nimeendelea na msimamo wangu wa kutozichukua, siyo kwamba namchukia Katibu Mkuu hapa, lengo langu hasa ni kutaka kukisafisha chama chetu,” alisema Shellukindo.
Mbunge wa Mwibara, Alphaxard Lugola alisema vita vya wenyewe kwa wenye nchini Congo haishi kutokana na baadhi ya watu kunufaika nayo, hivyo hata suala la umeme nchini kuna watu wananufaika nalo.
“Congo mpala leo wana vita ambayo haishi hii ni kutokana na watu kunufaika, hivyo hata sisi hili suala la umeme halitakwisha leo kutokana na watu kunufaika nalo.
“Ni bora wanaotuhumiwa kuchangisha fedha kwa ajili ya kuhonga ili bajeti ipite watimuliwe wote, wakiendelea kuwepo tatizo halitakwisha hata tukitafuta fedha na mitambo bado tatizo litakuwepo,” alisema Lugola.
Chanzo hicho kiliendelea kueleza kuwa baada ya Lugola kutaka hatua zichukuliwe dhidi ya David Jairo, wabunge wakacharuka kwa kuungana mkono ili Katibu Mkuu huyo aondolewe kwenye nafasi yake.
Ndipo Mbunge wa Mafia, Abdulkarim Shaha (CCM), aliposema yeye amekutana na Jairo mara baada ya kuhairishwa kwa kikao cha bunge cha mchana lakini alichomwambia kinakatisha tama.
“Nimekutana na Jairo mchana huu ananiambia hatumuwezi…sisi ni ‘comedy’ hivyo tutapiga kelele na yeye ataendelea kudunda, huyu ni mtu wa ajabu sana hiki kiburi anakipata wapi, hivyo tunakuomba waziri mkuu umfukuze kazi leo hii,” kilibainisha chanzo hicho.
Kiliongeza kuwa baada ya mbunge huyo kusema hivyo, wabunge walicharuka na kuwa kama mbogo wakitaka katibu huyo wa wizara atimiliwe yeye pamoja na Mkurugenzi wa TANESCO.
Baada ya marumbano hayo waziri mkuu Pinda aliwatuliza nakuwataka watulie kwasababu yeye hana mamlaka ya kumtimua mwenye mamlaka hayo ni rais hivyo wasubiri na kuhusu Mkurugenzi wa TANESCO, aliwaambia wasubiri uchunguzi ufanyike kwanza kwasababu shirika hilo linajiendesha kwa hasara.
“Kuhusu ndugu Mhando naomba kwanza tuvute subra uchunguzi kwanza tunaweza kusema uwezo wake wa kuongoza ni mdogo kumbe ni shirika lenyewe kukosa fedha za kujiendesha,” alisema Pinda.