Na Mwandishi Wetu
NAIBU Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Dk. Makongoro Mahanga ameingia kwenye kashfa nzito ya kuvunja sheria za kazi nchini kwa kumtumikisha msaidizi wake wa Ofisi ya Bunge (PS), Bi. Itika Kasambala kwa miaka 10 bila mkataba na kumlipa sh. 200,000 kama mafao ya kufanya kazi kwa miaka 10.
Naibu Waziri, Mahanga anakuwa kiongozi wa kwanza kuingia kwenye kashfa hiyo huku akiwa kwenye taasisi ya Serikali inayosimamia ajira na waziri mwenye dhamana na ajira na haki za wafanyakazi nchini chanzo chetu kimeelezwa.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi wakili wa Bi. Kasambala, Nyaisa Godwin alisema kuwa kesi namba CMA/DSM/ILA/R.711/13 imefunguliwa Mahakama ya Kazi Jumanne ya wiki iliyopita kwenye Tume ya Usuluhishi na Upatanishi Kazini. Wakili Godwin alisema katika maelezo yake Naibu Waziri aliiambia mahakama kuwa Kasambala alikuwa akifanya kazi kwake kama mwanafunzi wa chuo kwenye mazoezi (field toka chuoni) japokuwa alishidwa kuithibitishia mahakama kwa ushawishi wa barua ya ‘field’ toka chuoni.
“…Tulishagazwa na majibu ya waziri kwamba dada huyo alikuwa ‘field’ na nilimuuliza ‘field’ ya miaka 10? Alishidwa kutoa jibu mbele ya mpatanishi (Arbitrator),” alisema wakili Godwin.
Aliongeza kuwa kwa mujibu wa sheria za kazi na mahusiano kazini, Naibu Waziri amekiuka kifungu cha 3 cha sheria ya Taasisi za kazi za mwaka 2004 na pia amekiuka sehemu ya tatu ya viwango vya ajira na sehemu ndogo ‘A’ kwa kushidwa kuandika mkataba kwa mujibu wa kifungu cha 14 ibara ya kwanza kama sheria ya kazi na mahusiano kazini inavyotaka. Katika kifungu hicho cha 14 ibara ya kwanza kinasema mkataba utakuwa wa kipindi cha muda usiotajwa, mkataba wa kazi maalumu na mkataba unatakiwa kuwa wa maandishi ambapo vyote Mhe Naibu Waziri hakufanya.
Ibara ya 15 kifungu cha.-(1) kinasema kwa kuzingatia masharti ya kifungu kidogo cha (2) cha kifungu cha 19, mwajiri anatakiwa kumpa mfanyakazi, wakati mfanyakazi anapoanza kazi, taarifa zifuatazo kwa maandishi, jina, umri, anuani ya kudumu na jinsia ya mfanyakazi; mahali alipoajiriwa; kazi zake; tarehe ya kuanza; muundo na muda wa mkataba; kituo cha kazi; masaa ya kazi; ujira na njia ya ukokotoaji wake, na taarifa za mafao mengine.
Wakili Godwin alisema kutokana na matatizo ya kuachishwa kazi ghafla bila taratibu dada huyo amepata maradhi ya presha, vidondo vya tumbo na maradhi mengine baada ya kufanya kazi kwa mbunge kwa miaka 10 bila matibabu wala kulipiwa mafao katika Mfuko wa Hifadhi ya Jamii. Wakili Nyaisa alisema kesi ya Naibu Waziri wa Kazi itasomwa tena Februari 13, 2014 katika Tume ya Usuluhisho na Upatanishi Kazini.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi hivi karibuni jijini Dar es Salaam, Bi. Itika Kasambala (31) anasema alianza kazi kwa Mbunge huyo wa Segerea na Naibu Waziri wa kazi, Dk. Mahanga, mwaka 2003 kama PS (Personal Secretary) kwa makubaliano ya kumpa mshahara wa sh. 120,000 kwa mwezi lakini alianza kumlipa sh. 50,000 tu.
“…Aliniambia kwamba nianze kazi kwanza baadaye atanipa mkataba wa ajira na kunilipa mafao ya Hifadhi ya Jamii na matibabu lakini baada ya miaka kumi ananitumia sms (ujume wa simu) akiwa Dodoma kwamba kazi basi sikuhitaji tena,” Kasambala alisema.
Amesema kwamba Mbunge huyo alimtumia sms akiwa kwenye vikao vya bunge mjini Dodoma mwaka 2013 mwezi wa sita akimjulisha kwamba ajira yake imefikia kikomo kwa sababu hana uwezo tena wa kumlipa mshahara na mahitaji mengine ya kiofisi.
Kasambala aliendelea kusema kwamba mara ya kwanza wakati anaanza kazi mwezi wa tano mwaka 2003 baada ya msaidizi wa ofisi ya mbunge Mahanga kuacha kazi na ndipo alipotafutwa yeye na walikwenda kuelewana kwa malipo ya 120,000 kwa mwezi. Alisisitiza kwamba mara baada ya kuanza kazi kwa ofisi ya mbunge alikuwa analipwa pesa mkononi na baadaye kwa Tigo-pesa na baada ya muda akawa anachukua pesa ya mshahara toka Manisapaa ya Ilala kama posho ya Mahanga kama diwani kila mwezi.
Aliongeza kuwa tangu aanze kazi kwa Mahanga hakuwa anatoa huduma zozote kama matibabu au fedha kwa ajili ya siku kuu ilikuwa ni mshahara tu wa 120,000 kwa mwezi lakini kila akimfuata ili waandikishiane mkataba alikuwa akimzungusha bila sababu za msingi. Bi. Kasambala aliongeza kuwa amefanya kazi kwa Mahanga tangu akiwa mbunge wa Ukonga na baadaye Segerea lakini ameshidwa kuheshimu sheria za ajira na taratibu za kazi wakati yeye mwenyewe ni waziri mwenye dhamana ya ajira kwa watanzania.
Alisema mwaka jana Septemba 14, 2013 alimtumia kwa Tigo pesa kiasi cha sh. 200,000 kama mafao yake baada ya kufanya kazi kwa takribani miaka 10 kama Msaidizi wake wa Ofisi ya Mbunge. Alisema aliamua kwenda Chama cha Wafanyakazi wa Hifadhi, Mahoteli, Majumbani na Kazi Nyingine (CHODAWU) kwa msaada zaidi wa kisheria na baada ya kukutanishwa na Mahanga bado alikuwa mgumu kukubaliana kiungwana mpaka ikawalazimu kwenda Tume ya Usuluhishi na Upatanishi Kazini.
Juhudi za kumtafuta, Naibu Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Dk. Mahanga hazikuzaa matunda baada ya simu yake ya kiganjani kushidwa kupatikana kwa muda mrefu alipotafutwa kwa ajili ya kutoa ufafanuzi zaidi juu ya tuhuma hizo.