Wakulima Wanavyolalamikia Dawa ‘Feki’ za Kilimo…!

Baadhi ya dawa zinazodaiwa ni feki

Baadhi ya dawa zinazodaiwa ni feki

TANGU kuanzishwa kwa kauli mbiu ya kilimo kwanza, kumekuwa na juhudi kubwa zinazofanywa na serikali kuhakikisha wakulima wanaingia kwenye kilimo cha kisasa. Juhudi hizo zimetiliwa nguvu zaidi katika kuimarisha upatikanaji wa pembejeo za kilimo ili kuwafanya wakulima kuzitumia na kuimarisha kilimo chao.

Baadhi ya dawa zinazodaiwa kuwa feki

Pamoja na juhudi hizo za serikali, bado kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wakulima juu ya pembejeo hizo za kilimo, ambapo zimekuwa zikilalamikiwa kwa kuharibu mazao.

Kwa mfano, mbolea ya Minjingu imekuwa ikilalamikiwa na wakulima kwa kile kinachoelezwa kukausha mazao yao na kutokuwa na virutubisho vya msingi kwa ajili ya ukuaji wa mazao.

Katika kuonesha kuwa kuna matatizo ya msingi katika kupatikana kwa dawa na mbolea kwa ajili ya mazao ya wakulima, kelele nyingi zimekuwa zikisikika pia bungeni kulalamikia mbolea na dawa feki.

Katika Bunge lililopita baadhi ya wabunge waliitaka serikali kushughulikia malalamiko ya wakulima kutokana na mbolea na dawa zinazosambazwa na mawakala kutokuwa na ubora.

Wabunge hao walieleza kuwa pamoja na serikali kuhamasisha wakulima kwa kauli mbiu ya kilimo kwanza lakini kumekuwa na tatizo la mbolea na dawa hizo kutokidhi viwango na matokeo yake kuua mazao.

Katika kujibu malalamiko ya wabunge, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, aliwahi kueleza kuwa serikali inafanyia kazi malalamiko ya dawa na mbolea ya Minjingu. Wakati hali ikiwa hivyo bungeni, wakulima sehemu mbalimbali nchini wameendelea na kilio cha kupatikana kwa dawa feki za kilimo, kitu ambacho kimezidi kuwaathiri katika kilimo chao.

Kwa mfano, wakati wakulima wakitafuta mbinu za kuongeza tija kwenye kilimo, baadhi ya wafanyabiashara wameingiza na kusambaza dawa bandia. Dawa hizo ambazo zinatengenezwa na baaadhi ya kampuni zilizoko mkoani Morogoro zimesambazwa kwa kutumia nembo ya kampuni zingine za dawa nchini. Baadhi ya wakulima wanasema kuwa dawa hizo ambazo hazijapata vibali au kuthibitishwa na mamlaka husika, zinatishia kupunguza ufanisi wa kilimo.

Dawa hizo, zikiwemo aina ya Karate 50ec na Selecron720ec, zinasambazwa kwa wakulima zikiwa na nembo na vifungashio vya kampuni zingine za dawa za kilimo. Inadawa dawa hizo zinatengenezwa mkoani Morogoro lakini maelezo yaliyopo kwenye kopo yanaonyesha zimetengenezwa nchini Zimbabwe na Malawi.

Baadhi ya wakulima mkoani Mbeya wanaeleza kuwa, dawa hizo hazina ubora na zimekuwa kikwazo kwa maendeleo yao katika kuongeza tija ya uzalishaji. Mkulima John Mwaipopo, mkazi wa wilaya Mbarali, anasema serikali inatakiwa kuwakamata wafanyabiashara wanaouza dawa zisizo na ubora.

“Wakulima wananyanyasika kwa kuuziwa dawa na pembejeo zisizo na ubora kila kukicha.Tumewahi kuuziwa saruji iliyochanganywa na chumvi eti ni mbolea, sasa tumeanza kuletewa dawa feki,”anaeleza.

Pamoja na malalamiko hayo, Mkurugenzi Msaidizi wa Afya ya Mimea, kutoka Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, Fabian Mkondo, anaeleza kuwa wamepokea malalamiko hayo na wanafanyia kazi.

Kwa jumla, malalamiko juu ya kuwepo kwa dawa na mbolea feki yamechangia kushusha ari ya wakulima na kuondoa dhana ya kilimo kwanza, kitu ambacho kinaweza kuleta athari zaidi katika uzalishaji.

Katika kuendelea kuonyesha namna ambavyo kumekuwa na usambazaji wa mbolea na dawa feki, wakulima wa mpunga, mahindi na mazao mengine katika Kata ya Dakawa na maeneo mbalimba, wilayani Mvomero, nao wamekumbwa na dhahama hiyo.

Wakulima hao wanalalamikia kitendo cha mawakala wa mbolea na pembejeo, kuwasambazia mbolea na dawa feki zinazoua mazao yao kupitia mfumo wa vocha.

Wakulima hao wanaeleza kuwa kumekuwa na ujazo mdogo wa mbolea na mbolea hiyo imekuwa ikiua mazao , kuyadumaza, kubadilisha rangi na hatimaye kukauka. Katika kusikia kilio cha wakulima hao, Mkuu wa mkoa wa Morogoro, Joel Bendera, anakiri kupokea malalamiko ya wakulima na amekubaliana na malalamiko yao.

Vilevile, Bendera anawataka mawakala kusambaza mbolea na dawa zilizo na viwango tofauti na hivyo serikali itawachukulia hatua kali za kisheria.

Mnyororo wa malalamiko ya wakulima juu ya pembejeo zisizo na ubora upo pia kwa wakulima wa  Kata ya Ikuwo wilayani Makete mkoani Njombe, ambao wanalalamikia wafanyabiashara wa pembejeo wanaowauzia mbegu za mazao, zisizokuwa na ubora unaotakiwa kulingana na mazingira yao.

Wananchi hao, walitoa malalamiko hayo , walipotembelewa na wataalamu wa mbegu kutoka kampuni ya Highland Seed Growers mkoani Mbeya. Wanasema baadhi ya wafanyabiashara wa pembejeo, wamekuwa na tabia ya kuwauzia mbegu za mazao ambazo hazina ubora unaotakiwa na kusababisha kukosa mavuno mazuri.

Wanaeleza kuwa kutokana na wengi wao kutokuwa na utaalam mzuri wa kutambua mbegu bora, wamejikuta wakiingia hasara ya kununua na kutumia mbegu zisizofaa zinazouzwa na baadhi ya kampuni. Ofisa Kilimo wa Kata ya Ikuwo, Olimpa Ukwama, anaeleza kuwa hali hiyo,imetokana na wakulima hao kutotafuta ushauri wa kitaalam kutoka kwa wataalam wa kilimo kabla ya kutumia mbegu na dawa zinazosambazwa na kampuni mbalimbali wilayani humo.

Meneja Masoko wa Kampuni ya Highland Seed Growers, John Mbele, anasema utafiti uliofanywa na kampuni hiyo, umebaini chanzo cha hali hiyo ni ufahamu mdogo wa wakulima kuhusu namna ya kutambua mbegu na dawa bora na kuchelewa kufikishwa kwa pembejeo. Kwa msingi huo, kuna umuhimu kwa serikali kuchukua hatua za haraka kupambana na mtandao wa kusambaza dawa na mbolea feki kwa wakulima, ili kutekeleza kauli mbiu ya kilimo kwanza kwa vitendo.
Kushindwa kuwabana watu hao wanaosambaza mbolea na dawa feki kwa wakulima kutachangia kushusha uzalishaji na kurudisha nyuma ari ya wakulima katika kujishughulisha na kilimo, kwa kuwa matumaini yao ya uzalishaji yanakuwa yanapotea.

Kupotea kwa matumaini kwa wakulima kutachangia baadhi yao kuogopa kutumia mbolea na dawa zozote hivyo kurudi kwenye kilimo kwa kijadi ambacho hakitazalisha kulingana na matarajio ya serikali na wakulima.