UNDP: Tanzania Yaongoza Mpango wa Majaribio Mageuzi ya UN

Logo ya Taifa la Tanzania
TANZANIA imefanya vizuri zaidi na kuonyesha mafanikio zaidi kuliko nchi nyingine yoyote duniani kati ya nchi nane ambazo zilikuwa zinashiriki katika Mpango wa Majaribio wa Kuuwezesha Mfumo wa Umoja wa Mataifa Kufanya Kazi kwa Pamoja wa Delivering as One ambao sasa umepanuliwa kushirikisha nchi nyingi zaidi baada ya kuonyesha faida kubwa.

Hayo yamesemwa Jumanne, Januari 14, 2014, na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) na Mratibu Mkazi wa Shughuli za Umoja wa Mataifa (UN Resident Coordinator) katika Tanzania, Dk. Alberic Kacou wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Ikulu, Dar es Salaam.
Dk. Kacou ambaye alikuwa anaagana na Rais Kikwete baada ya kuitumikia UN katika Tanzania kwa miaka minne unusu ameondoka nchini baadaye leo adhuhuri kwenda Makao Makuu ya UN, New York, Marekani, ambako atakuwa Mkuu wa Utawala (Chief of Staff) na Mkurugenzi wa Ofisi ya Utawala na uendeshaji wa UNDP.
Katika mazungumzo yao na Rais Kikwete, Dk. Kacou amemwelezea Rais Kikwete mafanikio ambayo yaliyopatikana katika mahusiano ya UN/UNDP na Tanzania katika miaka minne iliyopita ikiwa ni pamoja na shirika hilo la Umoja wa Mataifa kuunga mkono kifedha na kiufundi shughuli za uchaguzi mkuu katika Tanzania.
Kuhusu mpango wa Delivering as One ambao unalenga kuuwezesha Umoja wa Mataifa kuwa na ufanisi zaidi na kutoa huduma kwa haraka na ubora zaidi na kupunguza matumizi, Dk. Kacou amemwambia Rais Kikwete:

“Tanzania imetoa mchango mkubwa sana katika mageuzi yanayofanyika ndani ya UN ya Delivering as One kiasi cha kwamba nchi yako, Mheshimiwa Rais, imeongoza miongoni mwa nchi nane ambako majaribio ya mfumo huo mpya yalikuwa yanafanyika. Serikali yake imeonyesha kiwango cha juu sana cha kuyakubali na kuyaongoza majaribio hayo. Matokeo yake ni kwamba mpango huo sasa unapanuliwa na kuanza kufanya kazi katika nchi nyingine 45 duniani.”

Dk. Kacou amesifia sana amani na utulivu wa Tanzania na kusema kuwa sifa hizo ndizo zinaendelea kuifanya Tanzania nchi ya mfano katika eneo ambako amani na utulivu ni tunu za nadra sana. Naye Rais Kikwete amemwambia Dk. Kacou: “Tunakushukuru sana. Wakati wa uongozi wako, uhusiano wa Tanzania na UN umeimarika sana na nchi yetu imenufaika sana na hali hiyo ya kuimarika kwa uhusiano. Uongozi wako umekuwa wa mfano kabisa na ni matarajio yetu kuwa mrithi wako ataendeleza mazuri mengi ambayo unayaacha nyuma.”

Ameongeza Rais Kikwete: “Umekuwa mmoja wa viongozi bora zaidi wa UNDP katika nchi yetu. Chini yako, UNDP imesaidia kuleta uwiano bora zaidi baina ya taasisi mbali mbali za kimataifa na za Umoja wa mataifa. Chini yako, UNDP imekuwa ni sauti ya busara katika dunia ambako busara ina mipaka yake.”

“Tunathamini sana mchango wako katika maendeleo ya Tanzania. Tunathamini juhudi zako na mafanikio yako katika miaka yako minne ya uongozi bora wa UNDP katika nchi yetu. Tunakutakia heri na mafanikio makubwa katika kazi yako mpya na katika maisha yako ya baadaye. Umethibtibisha kuwa wewe ni binadamu bora na ofisa bora wa Umoja wa Mataifa.”