ASKARI wawili wa Jeshi la Polisi na Magereza pamoja na raia watatu wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Mbeya wakituhumiwa kwa ujambazi wa kutumia silaha. Watuhumiwa hao watano kwa pamoja walifikishwa mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Mbeya, Michael Mteite wakituhumiwa kwa kosa moja la unyang’anyi wa kutumia Silaha kinyume cha Sheria kifungu cha 287 sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Mwendesha mashtaka wa Serikali, Archiles Mulisa aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Mshitakiwa namba moja ambaye ni Askari Polisi, PC James namba F8302 wa Wilaya ya Mbeya ambaye kabla ya kufikishwa mahakamani alivuliwa Uaskari baada ya kuhukumiwa kijeshi.
Aliwataja wengine kuwa ni mshtakiwa namba mbili kuwa ni Elinanzi Mshana (22) Mkazi wa Iyela Jijini Mbeya, Askari Magereza namba B 500 Sajenti Juma Mussa (37) wa Gereza la Ruanda Mbeya, Mbaruku Hamis (29) Mkazi wa Iyela na Amri Kihenya (38) Mkazi wa Iyela.
Akisoma mashtaka yao Mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Michael Mteite, Mulisa alisema watuhumiwa hao walitenda kosa hilo Januari 3, Mwaka huu majira ya saa 11 jioni katika eneo la Mlima Kawetere barabara ya Mbeya Chunya. Alisema watuhumiwa hao kwa pamoja walitenda kosa hilo kwa kulizuia gari aina ya Pick Up lililokuwa likiendeshwa na Ezekia Matatira (34) Mkazi wa Iyunga Jijini Mbeya ambaye alikuwa na mtu aliyekuwa akifahamika kwa jina la Sreedhar Pasupelet (38) mwenye asili ya Kiasia wakitumia magari madogo mawili ambayo ni GX 100 Toyota Cresta T 782 BEU na Gari lingine ambalo lilikuwa na namba za Chesesi GX 6011832 AINA YA Grand Mark II.
Aliongeza kuwa mbinu iliyotumika ni watuhumiwa hao kutega magogo barabarani huku wakiomba msaada kwa madai kuwa magari yao yameharibika na ndipo baada ya wahanga kusimama waliwapora vitu vyao wakiwa na mapanga ambavyo ni pesa shilingi Milioni 3.5, Mabegi matatu yenye nguo mbalimbali, Kompyuta mpakato, simu aina ya Sumsung yenye thamani ya Shilingi Laki mbili pamoja na simu ya dereva aina ya Tekno ambayo aliitambua Mahakani na kutumika kama kielelezo.
Hata hivyo watuhumiwa wote kwa pamoja walikana kuhusika na matukio hayo ambapo upande wa mashtaka ulileta Shahidi mmoja ambaye ni Dereva wa Pick up Ezekia Matatira ambaye aliwatambua washtakiwa wote watano na kuiambia mahakama kuwa siku hiyo ya tukio aliagizwa na bosi wake kwamba awapeleke wageni Chunya na ndipo alipotekwa katika eneo hilo huku watekaji wakiagizwa na maaskari na yeye kufungwa pingu na kutishiwa na panga.
Aidha kutokana na kesi hiyo Hakimu Mteite aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 15, mwaka huu ambapo upande wa Mashtaka utaleta mashahidi wengine huku watuhumiwa wakirudishwa Rumande baada ya dhamana yao kufungwa.
Chanzo; Mbeya yetu Blog