Mahakama Nkasi Yalalamikiwa Kuvunja Ndoa Yenye Mgogoro Bila Kugawanya mali

Maria Tarafa (wa kwanza kushoto) akiwa na watoto wake wanne aliozaa na Ndebile Kazuri akiwa amekaa kwenye kifusi cha sehemu ya nyumba anayokaa, mumewe ameibomoa nyumba hiyo ili kumfukuza eneo hilo.

Maria Tarafa (wa kwanza kushoto) akiwa na watoto wake wanne aliozaa na Ndebile Kazuri akiwa amekaa kwenye kifusi cha sehemu ya nyumba anayokaa, mumewe ameibomoa nyumba hiyo ili kumfukuza eneo hilo.


Na Joachim Mushi, Nkasi
MAHAKAMA ya Mwanzo Namanyere wilayani Nkasi imelalamikiwa kwa kitendo cha kuvunja ndoa iliyokuwa na mgogoro kwa wanandoa bila kugawanya mali iliyochumwa kipindi cha wanandoa wakiishi kama mke na mume. Bi. Maria Tarafa (25) mkazi wa Kijiji cha Isale ambaye ni mmoja wa wanandoa hao ametoa malalamiko hayo hivi mjini hapa alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi, huku akiituhumu mahakama hiyo haijampa nafasi ya kujitetea kama akiwa kama mlalamikiwa.

Alisema mumewe, Ndebile Kazuri (31) alikuwa akitaka kumtelekeza yeye na watoto wao wanne kwa muda mrefu kwa kutaka kuivunja ndoa yao halali kinyemela, lakini alikuwa akimshinda kila alipoitisha vikao vya wazazi na viongozi wa vijiji na kata akitaka kuivunja ndoa hiyo bila kutoa haki kwa mama na watoto (huduma).

Alisema mume huyo wameishi naye kama mtu na mke wake tangu mwaka 2003 na kufanikiwa kupata watoto wanne ambao walikuwa wakiishi eneo moja na baba yao huku Kazuri naye akiishi na mwanamke mwingine eneo hilo ambaye pia wamezaa naye.
“…Licha ya kuishi naye amekuwa akinipiga na kunifukuza niondoke kwake na watoto wangu nirudi kwetu, lakini mimi nimekataa mara zote na kumwambia nitakuwa tayari kuondoka baada ya kupata haki zangu na watoto kuhakikisha wako katika malezi mazuri,” alisema Bi. Tarafa.

Alisema mumewe aliamua kwenda baraza la kata na kuomba barua ili aende mahakamani kuiomba mahakama ivunje ndoa yake na mkewe aondoke na kurudi kwa wazazi wake. Kazuri alifungua kesi katika Mahakama ya Mwanzo, Namanyere Wilaya ya Nkasi Oktoba 28, 2013, kesi namba 26/2013 iliyosikilizwa na Hakimu aliyetajwa kwa jina la B. Stanley.

Alisema mahakama ilimwita kwa mara ya kwanza na kumsomea maelezo ya mdai (mumewe) ya kuomba ndoa yao ivunjwe yeye alipinga na kutaka awasilishe maelezo yake lakini mahakama iligoma kwa madai ilichoitaji kwa mlalamikiwa ni kujibu kama yupo tayari au la na si kupata maelezo. “…Niliomba niliomba nipewe nafasi ya kuzungumza upande wangu lakini walikataa na kuniambia; mama tumekuja kusikiliza kesi ya talaka na si maelezo mengine, we sema kama upo tayari au la…,” alisema.

Aliongeza kuwa Novemba 18, 2013 baada ya yeye kukiri kuwa yupo tayari kuachana na mume huyo iwapo atapata haki zake na watoto, mahakama ilivunja ndoa hiyo na kuamuru aondoke na watoto wawili bila kueleza namna watakavyo pata huduma toka kwa baba yao.
Alisema mahakama iliamuru watoto wa miaka 7 na 9 watabaki kwa baba yao nay eye kuondoka na wawili wenye miaka miaka chini ya saba. Aliongeza kuwa Mahakama iliamuru apewe magunia 9 ya mahindi kati ya 10 ambayo tulilima pamoja na bati 7.
“…Mume wangu alidanganya kuwa hatuna mali pale mahakamani, mimi nikaeleza ni uongo kwani tuna ng’ombe zaidi ya 127, buzi 30, nyumba mbili pale kijijini Isale pamoja na hekari zaidi ya 70 za ardhi…hawakunisikiliza pale mahakamani. Ukweli ni kwamba tunamali hizo ambazo tulichuma tukiwa wote,” alisema Bi. Tarafa.

Mwandishi wa habari hii amebahatika kupata nakala ya hukumu ya kesi hiyo, ambayo kweli haikuonesha namna watoto wanaobaki kwa mama watahudumiwaje licha ya kuamuru kuwa watabaki na mamayao. Akizungumzia sakata hilo, Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya, Ramadhan Rugemalira alisema mama huyo anahaki ya kufungua kesi ya madai kuomba mgawanyo wa mali na matunzo kwa watoto endapo hakuridhika na hukumu iliyotolewa kwa shauri hilo. “…Anachotakiwa kuomba mahakamani kwa sasa ni mgawanyo wa mali, kwamba katika kesi yao ambayo mahakama ilivunja kuna mali ambazo mahakama haikuzizungumzia kabisaa lakini na mimi (mke) ninahaki na mali hizo, unaona…ataleta ushahidi kama ng’ombe hao wapo kama kuna ardí na nini…hivyo huyo mwanaume ataitwa na kesi kusikilizwa,” alisema Rugemalira.

Hata hivyo, Hakimu Rugemalira alisema huenda mtoa hukumu wa mwanzo aliteleza kwa kitendo cha kutoainisha namna watoto wanaobaki kwa mama watalelewa vipi. Alisema pamoja na hayo bado mama huyo anahaki ya kufungua madai mengine kudai haki hizo. Tulipo zungumza na Kazuri juu la mali ambazo mke anazilalamikia, yaani ng’ombe 127, nyumba 2, mbuzi 30 na ardhi hekari 70 alisema mali hizo alipewa na babayake wakati anaanza maisha hivyo bado ni mali ya babayake ambaye alidai yupo hadi sasa. Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi umebaini baba yake na Kazuri (yaani Kazuri Moshi) ni marehemu alifariki tangu Machi 2004 na mali zake kugawiwa kwa watoto wake.

Hata hivyo mtalaka wake Kazuri anasema walipewa ng’ombe za urithi toka kwa baba yake na Kazuri zikiwa 65 lakini wamezizalisha hadi kufikia idadi zilipo sasa pamoja na mashamba na nyumba lakini anashangaa mzazi mwenzake anamdhulumu kila kitu.
-Imeandaliwa na dev.kisakuzi.com kwa kushirikiana na TAMWA