Nahodha wa Kilimanjaro II Ahojiwa Polisi Zanzibar Ajali ya Meli

Nahodha wa Kilimanjaro II Ahojiwa Polisi Zanzibar Ajali ya Meli

Nahodha wa Kilimanjaro II Ahojiwa Polisi Zanzibar Ajali ya Meli

WAKATI watu saba wakiwa bado hawajaonekana baada ya boti ya Kilimanjaro II, kupata ajali na abiria kuzama baharini, nahodha wa chombo hicho alitoa taarifa za uongo kuhusu ajali hiyo imefahamika. Akizungumza na gazeti hili, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri Baharini (ZMA), Mhandisi Abdi Omar Maalim, alisema taarifa iliyotolewa na nahodha katika kituo cha mawasiliano zilikuwa za uongo na hivyo kusababisha kazi ya uokozi kuchelewa.

Alisema baada ya boti hiyo kupigwa wimbi, abiria waliokuwa wamekaa juu waliteleza na kutumbukia baharini lakini nahodha katika ripoti yake alisema hakuna abiria waliotumbukia. Alisema hata alipotakiwa kupewa msaada na Kituo cha Mawasiliano cha Zanzibar, alisema hahitaji kwa sababu vitu vilivyotumbukia bahari ni vifaa vya uokozi na mizigo.

“Nahodha alitoa taarifa za uongo na kusababisha zoezi la uokoaji kutokufanyika kwa wakati mwafaka, baada ya kutokea ajali hiyo,” alisema Mhandisi Maalim.

Alisema ajali hiyo ilitokea saa 3:30 asubuhi lakini kazi ya uokoaji ilianza alasiri baada ya kupokea taarifa kutoka kwa abiria kuwa wenzao wamezama baharini baada ya meli kupigwa na wimbi. Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano, Rashid Seif Suleiman amesema nahodha wa chombo hicho alianza kuhojiwa na polisi juzi. Alisema kazi kubwa inayofanyika sasa ni kutafuta watu ambao bado hawajaonekana na baada ya kukamilika ataamua kama kuna haja ya kuunda tume ya kuchunguza ajali hiyo.

Alisema baada ya uhakiki wa majina ya abiria waliosafiri na boti hiyo wamegundua kuwa jumla ya watu 15 walizama baharini baada ya boti kupigwa na wimbi na kusababisha injini kuzimika. Waziri Seif alisema hadi jana maiti tano zimepatikana na watu watatu wameokolewa.

Msimamizi Mwandamizi wa chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Mnazimmoja, Vuai Jabir Hassan aliwataja marehemu kuwa ni Rashid Said Ali (11) mkazi wa Ilala Dar es Salaam, Akram Khamis Issa (11) wa Mwanakwerekwe, Masoud Hamad (30) wa Wete Pemba, Nushra Khamis (9) na Fatma Asir Khamis (18) wa Magogoni Wilaya ya Magharibi Unguja.

Aliwataja waliookolewa kuwa ni Ali Maulid Haji (Mwanakwerekwe), Ali Salum Ali (Pemba) na Mahir Ali Issa (Mwanakwerekwe).

Wakati huohuo, huduma za usafiri kati ya Unguja na Pemba zimesitishwa kwa muda kutokana na kuchafuka kwa hali ya hewa katika Bahari ya Hindi. Habari zilisema hatua hiyo ni ya kiusalama.
CHANZO: Mwananchi