Zitto Kabwe ‘Amevuliwa’ Uanachama, Dk Mkumbo, Mwigamba ‘OUT’ Chadema

Mbunge wa Chadema, Zitto Kabwe

Mbunge wa Chadema, Zitto Kabwe


Dk. Kitila Mkumbo

Dk. Kitila Mkumbo

Na Mwandishi Wetu

KUNA dalili zote kuwa Mbunge wa Kigoma Kiskazini kupitia Chadema, Zitto Kabwe amefukuzwa uanachama kama ilivyotangazwa na chama hicho kufukuzwa kwa wanachama wawili ambao walikuwa wakituhumiwa pamoja naye kukisaliti chama hicho.

Chadema kupitia kwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Willbrod Slaa tayari wametangaza kuwafukuza uanachama aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu wa chama hicho, Dk. Kitila Mkumbo pamoja na aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba.

Zitto ni mtuhumiwa pekee aliyebaki kati ya Dk. Mkumbo na Mwigamba ambao walikuwa wakituhumiwa kwa pamoja kukisaliti chama hivyo hivyo kwa hatua ya awali walikuwa wamevuliwa madaraka yote ya chama ndani ya Chadema ilhali wakisubiri maamuzi zaidi ya Kamati Kuu ambayo ndiyo yamewafukuza watuhumiwa wawili. Mahakama Kuu Tanzania, juzi ilizuia kwa muda Kamati Kuu ya Chadema kujadili ajenda zozote zinazomhusu aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wake (Zitto Kabwe) hadi ombi lake la rufaa ya kupinga maamuzi ya Kamati Kuu litakaposikilizwa.

Kufuatia maamuzi ya Chadema dhidi ya Dk. Mkumbo na Mwigamba kuna dalili zinazoonesha kuwa Zitto naye amefukuzwa uanachama kwani tayari Kamati Kuu imemzuia kufanya shughuli zozote za chama hicho kwa sasa. Zitto alifungua kesi kupinga uamuzi wa Kamati Kuu ya Chadema kumvua nafasi zote za chama hicho kwa tuhuma za kuandaa waraka wa siri ambao ulikuwa na malengo ya kukiangamiza chama.

Kesi ya Zitto iliyoko mahakamani ndiyo imemlinda kwa sasa kwani mahakama imezuia Chadema kumjadili kiongozi huyo maarufu nchini hadi hapo maamuzi ya mahakama yatatolewa katika kesi ya msingi aliyofungua akikilalamikia chama chake.

Taarifa za ndani toka Chadema zinasema Zitto naye amefukuzwa uanachama lakini haikuwa rahisi kumtaja kwa sasa kwa kuwa anapingamizi la mahakama hadi kesi aliyofungua iishe mahakamani. “…Naye tayari kafukuzwa lakini wameshindwa kutaja kwa kuwa kuna kesi inaendelea mahakamani, ndiyo maana kwa sasa amezuiwa na chama kufanya shughuli zote za chama,” kilisema chanzo kimoja.

Mchambuzi mmoja wa masuala ya siasa nchini ameuambia mtandao huu kuwa kuna dalilizote kuwa Zitto naye amefukuzwa ndani ya Chadema kwa kuwa wenzake wote waliotuhumiwa nao wametimuliwa huku yeye akizuia kufanya shughuli zozote za chama. “…Hata akifukuzwa uanachama mi namshauri abaki kimya au atulize akili afanye mambo yake ipo siku Chadema watamkumbuka na kumrudisha kazini,” alishauri mshauri huyo.