RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amewataka Watanzania kuendelea kutoa maoni yao kuhusu aina ya Katiba wanayoitaka akisisitiza kuwa siyo dhambi kwa watu kutoa maoni yanayopingana na mapendekezo ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa tofauti na maneno yasiyokuwa ya kweli ambayo yamekuwa yanasambazwa na baadhi ya watu kuwa kazi ya Katiba imekamilika, bado Katiba mpya haijapatikana na wananchi wanaombwa kuendelea kutoa mapendekezo na maoni yao.
Rais Kikwete ametoa ufafanuzi huo kuhusu mchakato wa kusaka Katiba mpya nchini wakati alipokuwa anapokea Matembezi ya Vijana wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Kuadhimisha Miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar katika sherehe iliyofanyika kwenye Viwanja vya Maisala, mjini Zanzibar, Januari 5, 2014.
Akizungumza baada ya risala za vijana ambazo zimesisitiza msimamo wa CCM kuhusu aina ya Muungano ambao chama hicho kimeutetea tokea kuundwa kwake, Rais Kikwete amewaambia wananchi: “Tunataka Katiba ya watu wote, siyo Katiba ya kikundi ama vikundi vya watu. Hivyo, toeni maoni na mapendekezo yenu bila hofu wala woga kuhusu aina ya Katiba ambayo mnaitaka. Ni haki yenu kutoa mawazo yenu bila hata kujali mtu mwingine anasema ama kufikiria nini. Kila mtu ana uhuru wa kutoa maoni yake na hata kutofautiana na mapendekezo ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba siyo dhambi.”
Rais Kikwete amesema kuwa wananchi wanaweza kutoa maoni yao kwa njia nyingi ikiwa ni pamoja na kupitia kwa wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar ambao wote watakuwa ni wajumbe wa Bunge la Katiba. Jumatatu iliyopita, Desemba 30, mwaka jana, 2013, Tume ya Katiba iliyoongozwa na Makamu wa Kwanza wa Rais na Waziri Mstaafu, Mheshimiwa Jaji Joseph Sinde Warioba ilimkabidhi Rais Kikwete Ripoti ya Tume hiyo ambayo ni pamoja na Rasimu ya pili ya mapendekezo ya Katiba mpya.
Ameongeza Rais Kikwete: “Kuna watu wameanza kupotosha wengine kwa kusema kuwa kazi ya Katiba imekamilika. La hasha. Tume imetoa mapendekezo ambayo yanatakiwa kujadiliwa na kuamuliwa ipasavyo na Bunge la Katiba. Bunge hilo lina mamlaka ya kuamua linavyoona inafaa kwa kifungu chochote cha mapendekezo ya Tume.”
Amesisitiza Rais Kikwete: “Itumieni vizuri fursa hii kutoa maoni yenu ili tupate Katiba inayotupatia Muungano imara na nchi ya kidemokrasia na inayozingatia na kuheshimu haki za binadamu. Tupate Katiba ambayo itaendelea kuifanya nchi yetu salama, tulivu na yenye kupata maendeleo shirikishi na kunufaisha wote.”
Katika hotuba yake, Rais Kikwete pia amewakumbusha vijana historia ya vyama vya ukombozi wa TANU na ASP, historia ya mahusiano kati ya vyama hivyo na watu wa Bara na Visiwani na chimbuko la Muungano wa Tanzania ambao ulizaliwa Aprili 26, 1964 na mchango wa Mapinduzi ya Zanzibar katika kuzaliwa kwa Muungano huo.
“Vile vile inatupasa tukumbuke kuwa Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ndiyo yalikuwa chachu ya Muungano wa nchi zetu mbili. Huwezi kuzungumzia Muungano bila Mapinduzi. Kama Mapinduzi yasingefanyika Muungano usingekuwepo. Muungano ni mtoto wa Mapinduzi.”
Rais Kikwete ambaye alikuwa katika ziara ya kikazi ya siku mbili Tanzania Visiwani amerejea Dar es Salaam mchana wa leo.