MATUMAINI ya kupatikana kwa amani nchini Sudan Kusini yameingia mashakani baada ya mazungumzo ya ana kwa ana ya pande zinazopingana yaliyokuwa yakitarajiwa kufanyika nchini Ethiopia kuchelewa.
Waziri wa Mambo ya nje wa Ethiopia, Tedros Adhanom amesema mazungumzo hayo yaliyokuwa yafanyike siku ya Jumamosi hayatafanyika kama ilivyokuwa imetarajiwa. Alisema mikutano inaendelea mjini Addis Ababa ili kuandaa agenda za mazungumzo hayo ya pande zinazopingana.
Taarifa kutoka Juba zinasema mapigano makali yanaendelea, ambapo pia majeshi yanayomuunga mkono Rais Salva Kiir nayo yanajiandaa kwa mashambulizi katika eneo la Bentiu na Bor miji ambayo kwa sasa inashikiliwa na wafuasi wa Riek Machar aliyekuwa makamu wa rais wa zamani.
Taarifa zinaeleza kuwa pande zote zinajaribu kuimarisha udhibiti wa kijeshi kabla ya kuanza kwa mazungumzo ya suluhu.
-BBC