JK Asitushwa Kifo cha Dk Mgimwa, Asema Taifa Lilimuhitaji

JK Asitushwa Kifo cha Dk Mgimwa, Asema Taifa Lilimuhitaji
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amepokea kwa mshtuko na huzuni kubwa taarifa za kifo cha Waziri wa Fedha, William Mgimwa, aliyekuwa pia Mbunge wa Jimbo la Kalenga (Mkoa wa Iringa) kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM).
Rais Kikwete amesema kuwa taifa limempoteza Waziri Mgimwa katika kipindi lilipokuwa linamhitaji zaidi kutokana na mchango wake mkubwa ambao amekuwa akiutoa kupitia nafasi zake za Waziri wa Serikali na mwakilishi wa wananchi wa Jimbo la Kalenga.
Kifo cha Mgimwa kimetangazwa mchana wa Januari Mosi, 2014, na Katibu Mkuu Kiongozi (KMK) Balozi Ombeni Sefue kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika tangazo lake, Balozi Sefue amesema kuwa Waziri Mgimwa ameaga dunia asubuhi ya leo saa 5:20 (Saa za Afrika ya Kati) katika Hospitali ya Kloof Medi-Clinic, Pretoria, Afrika Kusini ambako amekuwa amelazwa kwa muda sasa. Balozi Sefue amesema kuwa maandalizi ya kuurudisha nyumbani mwili wa Waziri Mgimwa yanafanywa na Serikali kwa kushirikiana na familia yake na kuwa taarifa zaidi kuhusu suala hilo zitatolewa baadaye kwa kadri zinavyopatikana na maandalizi yanavyoendelea.

Katika salamu zake kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda na kwa familia ya Marehemu Mgimwa, Rais Kikwete amesema: “Sina maneno ya kutosha kuelezea mshtuko na huzuni yangu kubwa kufuatia taarifa za kifo cha Mheshimiwa Mgimwa. Binafsi nimemtembelea mara mbili kwenye Hospitali alikokuwa amelazwa na mara ya mwisho hali yake ilikuwa imeimarika. Tulizungumza kwa kiasi cha dakika 10 hivi akanielezea nia yake na tamaa yake ya kurejea nyumbani kwa sababu hali yake ilikuwa nzuri.”
Ameongeza Mheshimiwa Rais Kikwete: “Sote tunajua mchango wake katika Serikali. Sote tulitamani kuendelea kuwa naye, lakini haya ni mapenzi ya Mungu.”

“Napenda kutoa pole nyingi na rambirambi zangu za dhati kwa wana-familia wote kwa kuondokewa na mhimili wao. Naungana nanyi katika kuomboleza msiba huo mkubwa. Napenda mjue kuwa msiba huu ni msiba wangu pia. Machungu yenu ni majonzi yangu,” amesema Rais Kikwete. Rais pia amewatumia rambirambi wananchi wa Jimbo la Kalenga akisema kuwa wamempoteza mwakilishi na mtetezi mahiri wa maslahi yao.