Na Mwandishi Wetu
BONDIA Kalama Nyilawila yupo katika mazoezi makali kabla ya kumkabili mpinzani wake Ibrahimu Maokola pambano litakalo fanyika Desemba 31, ambalo ni mpambano wa kufunga mwaka utakaoshirikisha mabondia mbalimbali pia. Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Kalama alisema yupo ‘fiti’ wakati wowote kwa ajili ya mpambano huo kwani ana usongo wa kuonesha ngumi zinachezwa vipi kwa mabondia chipukizi nchini.
Mpambano huo utaanza kabla ya bondia Fransic Miyeyusho kupanda jukwaani kuvaana na David Chalanga kutoka Kenya mpambano wa kimataifa wa mchezo wa masumbwi na mapambano mengine ni pamoja na Ibrahimu Class ‘King Class Mawe’ atavaana na Mohamed Kashinde huku Cosmas Cheka akioneshana ubabe na Iddy Mnyeke, Antoni Mathias atamenyana na Fadhili Majiha ambapo mapambano yote ya utangulizi yatakuwa ya raundi 6.
Mpambano huo pia utasindikizwa na burudani za muziki akiwemo msanii Kala Pina, Kimbunga Noma na wengine wengi ambao watauanga mwaka na kukaribisha mwaka mpya kwa njia ya burudani mwanzo mwisho.