Yohane Gervas, Rombo
VIJANA wilayani Rombo wametakiwa kufanya kazi kwa bidii sambamba na kujiunga katika vikundi mbalimbali vya ujasiriamali ili waweze kukabiliana na umasikini unaowakabili.
Rai hiyo imetolewa na mwenyekiti wa asasi ya Kiraia ya umoja wa vijana wa wilaya ya Rombo (UVIWARO), Neema Mremi wakati alipokuwa akizungumza na vijana wa wilaya hiyo katika mkutano Mkuu wa mwaka wa asasi hiyo.
Mremi amesema kuwa vijana wanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo suala la ukosefu wa ajira hali inayowafanya vijana wengi kujiingiza katika vitendo viovu kama vile uvutaji wa bangi na matumizi ya madawa ya kulevya jambo linalohatarisha maisha yao.
Amesema kuwa kwa kuzingatia haja iliyopo ya kasi ya kubwa ya maendeleo ya vijana wanatakiwa kushirikiana ili waweze kupena mawazo tofauti tofauti yanayoweza kubadilisha maisha yao kwa ujumla.
Akizungumzia mafanikio ya Asasi hiyo ya UVIWARO Mremi amesema kuwa hadi sasa wameweza kuwaunganisha vijana wengi wa tarafa zote tano za Wilaya ya Rombo na hadi sasa wamekwisha andaa mkakati wa kuwatafutia ufadhili na mikopo ili waweze kuanzia miradi yao.
Mremi ametoa wito kwa vijana wasiokuwa na ajira na walio katika ajira kujiunga na asasi hiyo ili waweze kupeana mbinu mbalimbali za kukabiliana na umaskini hali itakayoinua maendeleo katika Wilaya ya Rombo.