Chuo cha Diplomasia Chawanoa Maofisa Serikalini na Sekta Binafsi

Centre for Foreign Relations Logo

Centre for Foreign Relations Logo

KATIKA kuendeleza wajibu wake wa kutoa mafunzo ya muda mfupi, Chuo cha Diplomasia kimeendesha mafunzo ya juma moja ya Itifaki na Uhusiano kati ya tarehe 16 – 20 Desemba, 2013. Mafunzo haya yalilenga kuwaongezea uwezo maafisa mbali mbali kutoka serekalini na sekta binafsi. Mafunzo haya ni muendelezo wa mafunzo ya muda mfupi yatolewayo na Chuo cha Diplomasia, mathalan usuluhishi na utatuzi wa migogoro (Conflict Resolution and Mediation skills) na Itifaki na Uhusiano ( Protocol and Public Relations)

Mafunzo hayo yalihusisha maofisa wa kada mbalimbali kutoka idara za Serikali na sekta binafsi kama Benki Kuu ya Tanzania, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mamlaka ya Ufilisi, Vizazi na Vifo (RITA), Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC), Umoja wa Mataifa (UN) na Chuo Kikuu cha Dar es salaam.

Mafunzo hayo ya juma moja yaliyofanyika Kurasini Dar es salaam, washiriki walijifunza jinsi ya kuratibu itifaki za dhifa, sherehe za kitaifa na mikutano mingine mbali mbali. Pia walijifunza Diplomasia, uhuisiano wa umma na namna bora ya kuandaa taarifa kwa ajili ya mawasiliano na umma.

Akifunga mafunzo hayo, Mkuu wa Idara ya Utafiti, Uchapishaji, Ushauri na Kozi fupi, Bw. Juma M. Kanuwa alisisitiza kwamba mafunzo hayo yatawasaidia maofisa hao kuboresha utendaji wa kazi zao.

“Kazi zinazohusiana na itifaki na uhusiano wa umma (Protocol and Public Relations) zinahitaji utaalam ambao utamfanya mtu aweze kutimiza majukumu yake kwa ufasaha na kufikia malengo na matokeo mazuri. Hivyo mafunzo haya ya Itifaki na mengine yote yanayotolewa na Chuo cha Diplomasia yana lengo la kuwajengea uwezo na utaalam washiriki wote ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi na kupata matokeo bora,” alisema.

Kwa kawaida wawezeshaji wa mafunzo hayo ya muda mfupi katika Chuo cha Diplomasia, huwa ni mabalozi na wakufunzi waliobobea katika mambo ya Diplomasia na hivyo kuwapa washiriki uzoefu na mafunzo ya kiutendaji zaidi ili kuwajengea uwezo na ufanisi katika kuboresha majukumu yao.

Imetolewa Ijumaa na:Shoo Innocent, Ofisa Uhusiano
Simu: 0782 471698