Na Mwandishi Wetu
JESHI la Polisi Tanzania, limepeleka timu maalumu ya askari kutoka makao makuu kwenda wilayani Ulanga, Mkoa wa Morogoro katika Operesheni ya kuwasaka na kuwakamata baadhi ya wananchi waliovamia kituo cha Polisi na kukichoma moto pamoja na kuharibu mali zakituo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi, SSP – Advera Senso, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Said Mwema amelazimika kutuma kikosi hicho ili kwenda kuongeza nguvu katika Operesheni maalumu ya kuwasaka wananchi waliohusika ili sheria ichukue mkondo wake dhidi yao.
Taarifa inasema timu hiyo maalum ya askari itaongozwa na Kamishina wa Operesheni na Mafunzo (CP), Paul Chagonja kutoka Makao Makuu ya Polisi. SSP Senso alisema Jeshi la Polisi linalaani vikali tukio hilo linaloashiria vitendo vya vurugu na uvunjifu wa amani.
Alisema tukio hilo pia limesababisha vifo na majeruhi pamoja na kujenga hofu miongoni mwa jamii, ambapo wananchi 3 walipoteza maisha na wengine 3 walijeruhiwa na kuchomwa moto kituo na malizake.
“Mnamo tarehe 18/12/2013 majira ya saa tatu asubuhi katika kata ya Malinyi, tarafa ya Malinyi, wilaya ya Ulanga, mkoani Morogoro, kundi la watu kutoka maeneo mbalimbali kijijini hapo walivamia kituo cha Polisi Malinyi kwa lengo la kutaka kuwatoa kwa nguvu watuhumiwa 4 waliokuwa wamekamatwa kwa tuhuma za mauaji.” alisema.
“Katika jitihada za kuhami kituo, askari polisi walitoa tahadhali mbalimbali za kuwataka wananchi hao watawanyike ikiwemo kupiga mabomu ya machozi, lakini wananchi hao waliendelea kukaidi amri hiyo. Katika purukushani hizo za askari kutetea kituo na wavamizi kuendelea kuharibu mali za kituo ikiwemo kukichoma moto, wananchi 3 walipoteza maisha na wengine 3 walijeruhiwa,” alisema Senso katika taarifa hiyo.
Aidha, alisema IGP Mwema ametoa wito kwa wananchi wa mkoa wa Morogoro hususani wilaya ya Ulanga kata ya Malinyi, kuwa watulivu na kuendelea kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi wakati uchunguzi ukiendelea, mtu yeyote mwenye taarifa za wahalifu hao anaombwa kutoa taarifa kwenye namba ya simu ifuatayo 0754 78 55 57 au katika kituo chochote cha Polisi, ili wahalifu hao waweze kukamatwa na kufikishwa mahakamani.