MGAHAWA wa kisasa ambao unatajwa kuwa ni moja kati ya vivutio vya utalii jijini Dar es Salaam unaojulikana kama Akemi, umetimiza mwaka mmoja kwa kuleta mapinduzi makubwa katika sekta ya huduma za mgahawa hapa nchini huku ikijivunia mafanikio ya kuwa kituo cha utalii jijini Dar es Salaam.
Akemi ni mgahawa unaopatikana ghorofa ya 21 sawa na futi zaidi ya 250 toka chini katika jengo refu la Diamond Jubilee Tower lililopo katikati ya jiji la Dar es Salaam ikiwa na sifa ya kuwa mgahawa wa kwanza na pekee Tanzania wenye meza inayozunguka nyuzi 360 ndani ya dakika sitini na kuwafanya wageni kupata huduma ya chakula huku wakipata nafasi ya kuangalia mandhari ya jiji zima la Dar es salaam kupitia madirisha ya vioo.
Katika sherehe za kuazimisha mwaka mmoja toka kuzinduliwa rasmi kwa mgahawa huo wa Akemi, Mkurugenzi wa Akemi Bi. Priya Kanibar alisema kwamba wanayofuraha ya kutimiza mwaka mmoja wa kutoa huduma bora za mgahawa jijini Dar es Salaam, Akemi imekuwa ni moja ya vivutio vipya vya utalii kwa wageni wanaotoka nje ya nchi na hata mikoa mengine na wanawashukuru wadau wa sekta ya Utalii kwa kuwa Karibu na mgahawa huo ambao unalitangaza jiji la Dar es Salaam kama kituo kingine bora cha utalii.
“Tunafuraha ya kutimiza Mwaka mmoja katika kutoa huduma bora na kutangaza vyema jiji la Dar es Salaa na Tanzania, kwa sasa Dar es Salaam ndio jiji pekee kwa Afrika Mashariki na kati kuwa na mgahawa wenye sehemu ya kula chakula inayozunguka kwa nyuzi 360 ndani ya saa moja, hivyo kulifanya jiji hili kuongezeka thamani katika sekta ya utalii na biashara, tunajivunia Kuanzisha biashara hii hapa na bado tunavitu vingi vya kufanya ili huduma zetu ziwe bora zaidi na kuongeza pato la Taifa” alisema Bi. Priya
“Kila mtu anapenda kuona mandhari nzuri na Dar es Salaam ina hiyo mandhari ya kuwavutia watu mbalimbali duniani kama mtu akipata eneo zuri la kuanagalia kama Akemi, unaweza kuwa na chakula kizuri na huduma nzuri katika mgahawa wako au hata nyumbani lakini kama unakula katika mazingira ambayo si mazuri na bora yenye kuvutia basi chakula hicho sidhani kama kitakuwa kizuri tena, Akemi tumejali yote ya huduma bora, chakula bora lakini pia mazingira bora ya kuvutia ambapo mteja anafurahia kila kitu” aliongezea Priya.
Mgahawa wa Akemi ulianza huduma zake Desemba 2012 ambapo lengo lake likiwa ni kutoa nafasi nzuri ya kupata huduma za mgahawa zenye hadhi kwa wageni wa ndani na nje ya nchi ambapo Mwezi wa Agosti mwaka huu iliandaa hafla fupi ya kuwakutanisha wadau wa utalii nchi Tanzania katika kuangalia ni namna gani mgahawa huu unaweza kuwa kivutio kikubwa cha utalii jijini Dar es salaam na nchini kwa ujumla ambapo wadau kutoka sekta na kampuni mbalimbali walihudhuria wakiongozwa na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB).
Akizungumzia hafla hiyo Mkurugenzi wa Akemi Bi Priya alisema kwamba “Tuliandaa hafla ile ili kuwakutanisha wadau wa utalii Tanzania na kuwapa fursa ya kujadili ni jinsi gani mgahawa unaweza kuongeza pato la taifa kupitia utalii, sisi tupo Dar es Salaam ambapo watalii wengi hupita hapa kabla ya kwenda sehemu nyingine za utalii kama Arusha, Zanzibar na Kilimanjaro hivyo hii ni fursa kwa jiji la Dar es Salaam kujiongezea kipato na kupitia Akemi tuko tayari kushirikiana na wadau wote katika sekta ya utalii”
Kwa wapenzi wa vyakula mgahawa wa Akemi unatoa fursa ya kupata vyakula vya Kitanzania lakini pia vile vya Kimataifa kutoka kwa wapishi wa kimataifa waliobobea katika fani ya upishi. Ukiwa ni mgahawa pekee unaozunguka Tanzania, Akemi bado ina malengo ya kufikia mafanikio makubwa zaidi katika kutoa huduma bora za mgahawa pamoja na burudani kwa wateja wake wa nje na ndani ya nchi na kuendelea kuleta mapinduzi ya kibiashara katika sekta ya mgahawa Tanzania.