HOTUBA ya Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete katika hafla ya mazishi ya hayati Nelson Mandela aliyekuwa rais wa kwanza mzalendo wa taifa la Afrika Kusini imeleta mvuto katika hafla hiyo baada ya rais Kikwete kuelezea historia ya uhusiano mzuri uliokuwepo kati ya mataifa hayo mawili tangu Afrika Kusini ikisaka uhuru wake.
Hatuba ya Kikwete iliwagusa waombolezaji wengi baada ya kuelezea namna Tanzania ilivyoweza kuchangia taifa hilo kubwa kunyakua uhuru wao chini ya harakati za Nelson Mandela ambaye anaaminika ni Baba wa demokrasia wa Taifa hilo na Afrika. Akizungumzia historia hiyo Rais Kikwete alisema Tanzania ina uhusiano mzuri na nchi hiyo tangu harakati za ukombozi wa taifa la Afrika Kusini toka katika mikono ya ubaguzi wa rangi.
Alisema uhusiano wa Tanzania na Afrika Kusini utaendelea na msiba wa kiongozi huyo ni pigo kwa Tanzania pia kutokana na uhusiano aliyokuwa ameujenga tangu enzi za Rais wa Kwanza wa Tanzania, Hayati Mwalimu Julias Nyerere. Alisema uhusiano mzuri kati ya Tanzania na Afrika Kusini ulidhihirishwa na mapokezi ambayo alipewa Nelson Mandela kipindi alipolitembelea taifa la Tanzania, kwani alipewa mapokezi makubwa na umati mkubwa wa wananchi rekodi ambayo haijawahi kuvyunjwa na kiongozi yoyote aliye wahi kuitembelea Tanzania.
Aidha alimfananisha hayati Mandela kuwa mbali ya kuwa kiongozi wa kweli pia ni shujaa na nembo ya Afrika. Alisema kiongozi huyo ameweza kulibadilisha taifa la Afrika Kusini kuwa taifa jipya ambalo raia weupe na weusi wanaishi kwa amani na usalama huku wakiendesha shughuli zao kwa ushirikiano na upendo tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma kabla ya uongozi wa Mandela.