Askari Polisi Atukanwa Hadharani Akitekeleza Majukumu

Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, Said Mwema

Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, Said Mwema

Na Joseph Kayinga, Dar es Salaam

ASKARI wa Jeshi la Polisi nchini, Koplo Genja mwenye namba E-8455 ametukanwa na kudhalilishwa hadharani na dada mmoja mwenye asili ya Asia, baada ya afande huyo kutokubaliana na amri ya dada huyo ya kuacha kuchukua picha za gari lilohusishwa na makosa ya kiusalama barabarani.

Tukio hilo limetokea jirani na makutano ya barabara za Bibi Titi Mohammed na Zanaki, majira ya saa mbili na nusu asubuhi ya Ijumaa baada ya juhudi za askari wa jeshi hilo kumsihi kijana mmoja wa kiasia aliyekuwa akiendesha gari dogo aina ya Carina lenye namba za usajiri T642 CLQ kugoma kutekeleza maelekezo na amri kadhaa za askari waliokuwepo eneo la tukio.

Awali kijana huyo hakutekeleza amri iliyomwelekeza kuingia barabara ya Zanaki kutoka barabara ya Bibi Titi wakati msafara ulioongozwa na Jeshi la Polisi ulipokaribia kupita eneo hil. Amri iliyotolewa na PC John mwenye namba G-9487 aliyekuwepo eneo hilo, badala yake kijana huyo alikaidi na kuendelea mbele kidogo ndani ya barabara hiyo na kuegesha gari eneo finyu baada ya kulazimishwa asiendelee mbele zaidi.

Kufuatia tukio hilo PC John aliwaomba msaada kwa askari wenzake wanaotumia pikipiki waliopita eneo hilo kumhoji huku yeye akiendelea kuongoza magari ambayo kwa asubuhi hiyo yalikuwa mengi sana. Ni katika mahojiano hayo kijana huyo aliposhindwa kutoa ushirikiano kwa askari hao ambao nao waliomwita Koplo Genja kwa msaada zaidi.

Koplo genja alipofika eneo hilo alimuomba kijana huyo kushuka kwenye gari akagoma, alichokifanya ni kufungua kidogo kioo cha gari hilo kilichokuwa hakionyeshi ndani “tinted” na kuendelea kujibu maswali aliyoulizwa.

Mwishowe alifunga kioo na kuonekana akipiga simu kwa jamaa zake ambapo baada ya dakika chache alifika dada mmoja ambaye alimhoji afande Genja juu ya kinachoendelea. Ni katika mazungumzo hayo hawakuelewana ndipo afande aliamua kutoa kamera ndogo na kupiga picha kama vielelezo.

Tukio hilo lilionekana kumuudhi dada huyo kiasi cha kutamka  mara kadhaa maneno “…Do not take pictures” na hatimaye kusikika akitamka neno “Stupid”. Neno hilo ndilo lililowashtusha na kuwafadhaisha raia kadhaa waliokuwa wakishuhudia tukio hilo akiwemo mwandishi wa habari hii.