Mamlaka ya Hali ya Hewa Yatahadharisha Mvua Kubwa Kunyesha

Moja ya jengo likiwa limezungukwa na maji kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha.

Moja ya jengo likiwa limezungukwa na maji kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha.

MAMLAKA ya Hali ya Hewa nchini (TMA) inatoa tahadhari ya kuwepo kwa vipindi vya mvua kubwa katika maeneo ya nyanda za juu Kaskazini-Mashariki, ukanda wa Ziwa Victoria pamoja na Magharibi mwa Tanzania.

Kwa mujibu wa taarifa ya TMA mvua hizo zinatarajia kunyesha kuanzia Desemba 12, 2013 hadi Desemba 13 Desemba, 2013. “…hivi ni vipindi vya mvua kubwa (zaidi ya mm 50 katika masaa 24 yajayo) katika maeneo yaliyotajwa hapo juu,” ilisema taarifa hiyo ya TMA.

Taarifa hiyo iliyataja maeneo yatakayoathirika kuwa ni pamoja na Nyanda za Juu Kaskazini-Mashariki yaani mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro, Ukanda wa Ziwa Victoria yaani mikoa ya Kagera, Mwanza na Mara.

Mengine ni pamoja na Magharibi mwa nchi kwenye mikoa ya Kigoma na Tabora. TMA imesema hali hiyo inatokana na kuimarika kwa mfumo wa mgandamizo mdogo wa hewa ikiwa ni muendelezo wa ukanda wa mvua wa ITCZ.

“…Wakazi wa maeneo hatarishi yaliotajwa wanashauriwa kuchukua tahadhari. Hata hivyo Mamlaka ya Hali ya Hewa inaendelea kufuatilia hali hii na itatoa mrejeo zaidi.” Imefafanua taarifa hiyo.