Malkia Máxima wa Uholanzi Kushiriki Kukuza Wakulima Wadogowadogo Tanzania

Malkia Máxima wa Uholanzi Kushiriki Kukuza Wakulima Wadogowadogo Tanzania

Malkia Máxima wa Uholanzi Kushiriki Kukuza Wakulima Wadogowadogo Tanzania

MTUKUFU Malkia Máxima wa Uholanzi na maofisa waandamizi wa mashirika matatu ya chakula ya Umoja wa Mataifa wanaungana ili kukuza uelewa kuhusu namna upatikanaji wa huduma za fedha – kama vile akaunti za benki, mikopo ya muda mfupi, mikopo midogo, uwekaji akiba na bima – zinavyoweza kukuza ubora wa maisha na riziki za wakulima wadogowadogo na watu maskini wa vijijini.

Malkia Máxima anajiunga kwenye ziara hiyo katika nafasi yake kama Balozi Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Ushirikishwaji kwenye Masuala ya Fedha kwa ajili ya Maendeleo (UNSGSA). Aliwasili jijini Addis Ababa jana tayari kuanza safari ya siku tano nchini Ethiopia na Tanzania, pamoja na Maria-Helena Semedo, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO), Ertharin Cousin, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula Duniani (WFP) na Adolfo Brizzi, Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Ushauri wa Kiufundi katika Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD). Mnamo Jumatano, kundi hili limepangiwa kusafiri hadi Dar es Salaam, Tanzania, ambapo watakaa hadi tarehe 13 Desemba.

Malkia Máxima na wawakilishi waandamizi wa mashirika ya UN ya chakula yenye makao yao jijini Roma — FAO, IFAD na WFP – watakutana nchini Ethiopia na pia Tanzania na maofisa wa ngazi za juu wa serikali na viongozi waandamizi wa mashirika ya fedha ya kitaifa na kimataifa. Wakati wa ziara ya maeneo ya miradi katika nchi zote mbili, watakuana na wanavijiji na wakulima wadogowadogo na kujadiliana kuhusu namna ya kupanua upatikanaji wa huduma za fedha ili kuwasaidia wakulima kumudu mtiririko usio wa uhakika wa fedha na ili wapate kushughulikia majanga kama vile ukame na mafuriko, kuwekeza katika mitaji ili kuongeza uzalishaji, kufikia masoko na kupata kinga ya bima ili kupunguza hasara ya kupoteza mazao.

Balozi Maalumu na mashirika matatu ya chakula wanashirikiana na serikali na sekta binafsi ili kupanua huduma za fedha kwenye makundi ya pembezoni ya watu, hasa wanawake, ambao mara nyingi wanakumbana na vikwazo vya kisheria na sera, na vile vile vikwazo visivyo na uwiano kwa huduma, mafunzo na taarifa. Ushrikishwaji mkubwa Zaidi kwenye masuala ya fedha unaweza kusaidia kuongeza mafanikio ya wazalishaji wadogo ambao huwa hawhudumiwi na taasisi za mikopo midogomidogo, lakini ambao huonekana kwamba wao ni wa ‘hatari mno’ na benki za biashara.

Alhamisi, tarehe 12 Desemba, Malkia Máxima atatoa hotuba muhimu wakati wa uzinduzi wa Muundo wa Kitaifa wa Ushirikishwaji kwenye Masuala ya Fedha katika Benki Kuu ya Tanzania. Tukio hilo litafuatiwa na mkutano na vyombo vya habari.

Mikutano ya vyombo vya habari na mashirika manne ya Umoja wa Mataifa itafanyika jijini Addis Ababa mnamo tarehe 11 Desemba na jijini Dar es Salaam mnamo tarehe 13 Desemba.