HOTUBA YA MHESHIMIWA DK. MOHAMMED GHARIB BILAL, MAKAMU WA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KATIKA UFUNGUZI WA MAADHIMISHO YA SITA YA KITAIFA YA SIKU YA HAKI ZA BINADAMU NA MAADILI, VIWANJA VYA MNAZI MMOJA, DAR ES SALAAM,
TAREHE 10 DESEMBA 2013.
Mheshimiwa Mathias Chikawe, Waziri wa Katiba na Sheria;
Mheshimwa Angela Kairuki, Naibu Waziri Katiba na Sheria;
Mheshimiwa Pandu Ameir Kificho, Spika wa Baraza la Wawakilishi;
Mheshimiwa Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Jaji Kiongozi mstaafu Ameir Manento;
Mheshimiwa Jaji Kiongozi, Faki Jundu;
Mheshimiwa Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa hapa Tanzania, Joyce Mends- Cole;
Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali;
Waheshimiwa Makamishna wa Tume na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma;
Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria;
Waheshimiwa Mabalozi;
Waheshimiwa Viongozi mbalimbali wa Serikali; Waheshimiwa Wabunge na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi;
Viongozi wa Vyama vya Siasa, Dini na Jumuiya za Kijamii;
Wageni Waalikwa;
Ndugu Wanahabari;
Ndugu Wananchi;
Mabibi na Mabwana.
Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehma, kwa kutujalia uzima na kutuwezesha kukusanyika hapa leo, kushuhudia Maadhimisho haya ya Siku ya Haki za Binadamu na Maadili ambayo husherehekewa Duniani kote Desemba 10 kila mwaka.
Nitumie nafasi hii pia kuwakaribisha na kuwapongeza nyote mliofika mahali hapa. Mmefanya hivi kutokana na sababu moja tu kubwa, nayo ni kwamba; Kila mmoja wenu anatambua na kujali umuhimu wa Haki za Binadamu na Maadili mema ndani ya jamii yetu.
Niwashukuru pia wale wote waliofanikisha tukio hili kwa njia moja ama nyingine. Kipekee niwashukuru Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Wizara ya Katiba na Sheria, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma na Umoja wa Mataifa -Tanzania, kwa jitihada zao kubwa za kuratibu na hatimaye kufanikisha Maadhimisho haya. Hongereni sana.
Ndugu Wananchi;
Mabibi na Mabwana;
Tanzania imekuwa ikiadhimisha siku hii kutokana na ukweli kuwa sisi ni wanachama wa Umoja wa Mataifa ambako ndiko chimbuko la Haki za Binadamu, na kwamba kama Taifa, tunawajibika moja kwa moja kuzikuza, kuzilinda na kuzitekeleza hapa nchini.
Serikali ya Tanzania inao wajibu wa kulinda na kukuza Haki za Binadamu kama ilivyoelezwa na kufafanuliwa ndani ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Mikataba ya Kimataifa na Kikanda ya Haki za Binadamu na sheria mbalimbali za nchi.
Kwa kutimiza wajibu wa kulinda na kukuza Haki za Binadamu, Tanzania ni miongoni mwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa zilizoridhia mikataba mingi ya kimataifa inayohusu Haki za Binadamu. Baadhi ya mikataba hiyo ni pamoja na; Tamko la Ulimwengu juu ya Haki za Binadamu la 1948; Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa wa 1966; Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiuchumi, Kijamii na Kiutamaduni 1966; Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watoto 1989; Mkataba wa Kimataifa wa Kuondoa aina zote za Ubaguzi wa mwaka 1965; Mkataba wa Kimataifa wa Kuondoa Ubaguzi wa aina yoyote dhidi ya Wanawake wa mwaka 1979; Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watu Wenye Ulemavu wa mwaka 2008; Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Haki za Watu wa mwaka 1981 na Mkataba wa Afrika wa Haki na Ustawi wa Watoto wa mwaka 1990.
Baadhi ya mikataba hii tayari imeingizwa katika sheria zetu za nchi, ama kwa kuunda sheria mpya au kurekebisha zile zilizopo, ili kuhakikisha kuwa ulinzi wa Haki za Binadamu unaimarishwa.
Aidha, pamoja na kuridhia mikataba hii, Serikali imekuwa ikiandaa ripoti mbalimbali za utekelezaji wa Haki za Binadamu ambazo zimekuwa zikiwasilishwa kwenye vyombo vya kimataifa kwa ajili ya kujadiliwa na kutolewa mapendekezo ya utekelezaji.
Ndugu Wananchi;
Napenda niwahakikishieni kuwa Serikali inaendelea kupitia mikataba ambayo bado haijafanywa kuwa sehemu ya sheria za nchi, ili nayo iweze kuingizwa kwa kadri inavyofaa kwa maslahi ya wananchi wetu na maendeleo ya nchi yetu.
Katika kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa kinara wa kujali Haki za Binadamu, Serikali imeanzisha taasisi mbalimbali zinazoshughulikia masuala ya kulinda na kukuza haki nchini. Taasisi hizo ni pamoja na:- Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora; Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi; Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU); Bunge na Mahakama. Vyombo hivi vilianzishwa kwa mujibu wa sheria na tutazidi kuvipa ushirikiano kadri inavyowezekana ili viendelee kufanya kazi zake vizuri na kukidhi matarajio yake kwa umma.
Serikali pia imejenga mazingira mazuri na kuruhusu taasisi zisizo za kiserikali kuanzishwa kwa lengo la kusaidia juhudi zake za kuimarisha Haki za Binadamu hapa nchini. Hadi sasa, Tanzania ina takribani mashirika 5,000 yasiyo ya kiserikali yanayojihusisha na utetezi wa Haki za Binadamu. Mashirika haya yanatambuliwa kwa mujibu wa mikataba mbalimbali ya kimataifa na sheria za nchi. Baadhi ya mashirika hayo ni pamoja na; LHRC, NOLA, PINGOs, TPCF, TAWLA, ZLSC, WLAC, SIKIKA, SAHRINGON, TGNP, HAKIELIMU na HAKI-ARDHI. Mashirika haya yamekuwa yakitoa mchango mkubwa katika kutetea na kulinda Haki za Binadamu hapa nchini.
Serikali pia imetengeneza Mpango Mkakati wa Kitaifa wa Haki za Binadamu ambao utazinduliwa leo kwa lengo la kuhakikisha kila sekta inajumuisha masuala ya Haki za Binadamu kwenye mipango kazi yake na utekelezaji wake.
Ndugu Wananchi;
Mabibi na Mabwana;
Eneo lingine muhimu ambalo Serikali inajivunia katika harakati zake za kujenga misingi imara ya Haki za Binadamu hapa nchini, ni haki ya kupata elimu ambapo hadi sasa, zaidi ya asilimia 98 ya watoto wenye umri wa kwenda shule, wanaandikishwa na kupata elimu ya msingi inayotolewa bure. Hivi sasa kila kata nchini ina shule ya msingi na sekondari, kata zingine zina shule zaidi ya moja. Haya ni mafanikio makubwa katika utekelezaji wa Haki za msingi za Binadamu.
Ndugu Wananchi;
Maadhimisho haya yanatoa fursa nzuri kwetu sote kujiuliza; tumefanya nini katika kipindi cha mwaka mzima na changamoto zinazokabili suala zima la Haki za Binadamu. Tukumbuke kuwa utekelezaji wa Haki za Binadamu na Maadili ni mchakato, hivyo siku zote ni lazima tuendelee kuboresha haki hizo, kama vile ambavyo haki hizo pia huibuka na kuongezeka kila mara.
Napenda pia kuwahakikishieni kwamba Serikali yenu inajitahidi kuhakikisha kuwa wananchi wote hasa wale wa kawaida, wanapata msaada wa kisheria kwa kuchukua hatua mbalimbali zikiwemo:- Kuanzisha mchakato wa kuwa na Sekretarieti ya Huduma za Kisheria; Kuboresha Mahakama za Mwanzo; Kuanzisha Shule ya Taaluma ya Sheria na Kuongeza idadi ya majaji wa Mahakama za Rufaa kutoka wanane mwaka 2005 hadi kufikia 14 mwaka 2012 , na wale wa Mahakama Kuu, kutoka 24 hadi 54.
Ndugu Wananchi;
Pamoja na juhudi kubwa za Serikali kuboresha mazingira ya upatikanaji na utoaji wa Haki za Binadamu nchini, matukio ya ukiukaji wa haki hizo yameendelea kuongezeka. Taarifa za vyombo mbalimbali vya habari na ripoti za kitafiti, zimeonesha na kuthibitisha uwepo wa matukio kadhaa ya ukiukwaji wa haki za binadamu nchini.Baadhi ya matukio hayo ni kama yale ya Ghasia zinazohusiana na vurugu za makundi; Mahabusu kuwekwa rumande muda mrefu kabla ya kesi kusikilizwa; Unyanyasaji dhidi ya wanawake na watu wenye ulemavu wa ngozi; Unyanyasaji wa watoto (ikiwemo ukeketaji, ukatili wa kijinsia, ndoa za utotoni, mauaji kwa wanaozaliwa na ulemavu, utekaji nyara, ajira mbaya nk.) Nawahakikishieni kwamba Serikali imejipanga vema kukabiliana na kutokomeza uovu huo pasi kumwonea huruma mtu yeyote anayejihusisha na maovu hayo.
Tukumbuke kuwa watoto wanachukua nusu ya idadi ya Watanzania wote. Tunajua kwamba mafanikio katika utekelezaji wa haki mbalimbali za mtoto, ni muhimu kwa ukuaji na maendeleo ya nchi yetu hususan katika kufanikisha Malengo ya Milenia. Ni wajibu wetu sote kuhakikisha kwamba haki ya mtoto inalindwa sio tu kutokana na kwamba tunaiwakilisha Serikali bali kama wazazi, majirani na jamii kwa ujumla.
Leo hii pia, tunajivunia kuzindua Mkakati wa Miaka Mitano wa Kuendeleza Mageuzi ya Haki ya Mtoto 2013-2017. Tunazindua mkakati huu sambamba na Utekelezaji waMpango Mkakati wa Kitaifa wa Haki za Binadamu kuonesha dhamira ya dhati ya Serikali kulinda, kuendeleza na kuhamasisha haki za watoto .
Mkakati huu wa Haki ya Mtoto unaainisha hatua zinazopaswa kuchukuliwa na mawizara idara, mawakala na CSOs kwa miaka mitano kuhakikisha watoto wote ambao haki zao zimekiukwa, wanapata haki na kwamba mtoto yeyote anayekwenda mbele ya vyombo vya sheria, aidha awe muhanga, shahidi au aliyeonewa, anapata haki halali inayozingatia hadhi na utu wake kwa wakati.
Ndugu Wananchi;
Nitumie fursa hii pia kuwaasa Watanzania wenzangu kuanzisha kampeni maalum za kukuza maadili katika ngazi mbalimbali zikiwemo zile za utumishi wa umma, taasisi za dini, taasisi za elimu na katika nyanja zote za maisha ya kila siku. Suala hili likifanyika vizuri, naamini sote kwa pamoja, tutakuwa tumetimiza wajibu wetu wa malezi bora kwa watoto na vijana wetu hali itakayosaidia kupunguza maovu mengi ndani ya jamii.
Ndugu Wananchi;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Kabla sijahitimisha hotuba yangu, napenda kusisitiza kuwa usimamizi wa Haki za Binadamu na ujenzi wa Maadili mema ndani ya jamii yetu, ni jukumu la kila mmoja wetu. Kila mmoja wetu kwa namna moja au nyingine anawajibu wa kulinda, kuheshimu na kudumisha Haki za Binadamu. Nawahakikishieni kwamba Serikali ya Awamu ya Nne inatilia maanani sana suala la Haki za Binadamu, Utawala Bora na Maadili. Tukishikamana katika hili naamini tutashinda kwani “ Umoja ni nguvu”
Nawaasa kujiepusha na mambo yote yanayochangia kwa njia moja ama nyingine, kuvunja na kukiuka misingi ya Haki za Binadamu na Maadili mema. Kueni raia wema na chukieni maovu.
Baada ya kusema hayo, kwa heshima na taadhima natamka kuwa; Maadhimisho ya Sita ya Kitaifa ya Siku ya Haki za Binadamu na Maadili, yamefunguliwa rasmi.
Ahsanteni sana kwa kunisikiliza.