Na Hassan Abbas
MPANGO wa Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM) umemuomboleza Rais wa kwanza mzalendo wa Afrika Kusini, Mzee Nelson Mandela kwa kumtaja kuwa ni kiongozi wa mfano. Mandela (95) alifariki usiku wa Alhamisi iliyopita baada ya kupambana na maradhi na umri mkubwa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa juzi na makao makuu ya APRM yaliyoko mjini Midrand, Afrika Kusini, kifo cha Mandela ingawa kimeliachia Bara la Afrika huzuni kuu lakini Mzee Mandela anapaswa kushukuriwa kwa mambo makubwa aliyoyafanya kwa ajili ya binadamu.
“APRM ingependa kuwasilisha salamu zake za rambirambi kwa watu wa Afrika Kusini, familia, marafiki, wenzetu wengine katika Bara la Afrika na dunia kwa ujumla, kufuatia kifo cha Nelson Rholihlahla Mandela, Rais wa zamani wa Jamhuri ya Afrika Kusini,” ilisema taarifa hiyo.
APRM katika taarifa yake hiyo pia imesisitiza kuwa wakati Bara la Afrika na dunia vikiwa katika huzuni, Mpango huo unaungana na dunia katika kuomboleza na kuzikumbuka siku za maisha yake.
“Taasisi hii ya Afrika inaungana na dunia kuzitafakari harakati za Mandela na hasa uongozi wake madhubuti na usioyumba na kujitoa kwake katika kupigania maendeleo ya mwanadamu,” iliongeza taarifa hiyo.
APRM imetumia rambirambi hizo kusisitiza na kutambua mchango usio na kifani wa Mandela katika ukombozi wa Afrika Kusini. Taarifa inasema: “Tunamshukuru kwa harakati zake zisizo za ubinafsi za kuhakikisha Afrika Kusini na dunia kwa ujumla inakuwa huru.”
Enzi za uhai wake Mzee Mandela atakumbukwa kwa kupigania uhuru, kupiga vita ukandamizaji na ubaguzi wa rangi hadi alipofanikiwa kuushinda mfumo dhalimu wa kikaburu.
Pamoja na kwamba katika sehemu kubwa maisha yake tangu alipostaafu siasa Mzee Mandela alilazimika kupumzika zaidi kutokana na umri na maradhi bado mara kadha alishiriki katika jitihada mbalimbali za kuimarisha utawala bora Afrika ikiwemo kushiriki shughuli za APRM.
Mzee Mandela atakumbukwa mwaka 2007 kwa uamuzi wake wa kuambatana na mkewe, Graca Machel, kwenda nchini Kenya wakati wa tathmini ya APRM kuhusu utawala bora nchini humo.
Wakati Mama Graca alikuwa ndiye kiongozi wa jopo la wataalamu waliokwenda kuitahmini Kenya inavyotekeleza misingi ya APRM, Mzee Mandela aliona kuwa hiyo ni miongoni mwa fursa adimu na za kipekee kwake kushuhudia Afrika inavyopambana na changamoto zake za maendeleo.
Akiwa nchini Kenya katika ziara hiyo ya APRM, Mzee Mandela alinukuliwa akisisitiza kuwa angependa kabla ya kifo chake kuliona Bara imara zaidi la Afrika na linaloheshimu misingi adhimu ya utawala bora.