Takwimu Yaifagilia Tanzania Maendeleo ya Kiuchumi

Mkurugenzi wa Takwimu za Jamii na sensa ya Watu na Makazi Bw. Ephraimu Kwesigabo akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam kuhusu hali ya kuendelea kudhibitiwa kwa mfumuko wa bei nchini.

Mkurugenzi wa Takwimu za Jamii na sensa ya Watu na Makazi Bw. Ephraimu Kwesigabo akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam kuhusu hali ya kuendelea kudhibitiwa kwa mfumuko wa bei nchini.


Na Aron Msigwa – MAELEZO, Dar es Salaam

OFISI ya Taifa ya Takwimu imesema kuwa Tanzania inapiga hatua nzuri katika maendeleo ya uchumi kutokana na hali ya mfumuko wa bei nchini kuendelea kudhibitiwa hali inayoleta unafuu wa maisha kwa mlaji. Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam Mkurugenzi wa Takwimu za Jamii na sensa ya Watu na Makazi Bw. Ephraimu Kwesigabo amesema kuwa mfumuko wa bei wa Taifa kwa Mwezi Novemba 2013 umepungua hadi kufikia asilimia 6.2 kutoka 6.3 za mwezi Oktoba 2013 kutokana na kupungua kwa bei za bidhaa na huduma.

Amesema kuwa hali hiyo imesababishwa na kupungua kwa mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na bidhaa zisizo za vyakula kwa mwezi Novemba ikilinganishwa na mwezi Oktoba na kuongeza kuwa kumekua na ongezeko dogo la mfumuko wa bei wa bidhaa za nyumbani na migahawani hadi kufikia asilimia 7.6 kutoka 7.3 za mwezi Oktoba.

Kwa upande wa bidhaa zisizo za vyakula Kwesigabo ameeleza kuwa kasi ya ongezeko la bei imepungua hadi asilimia 5.7 kwa Mwezi Novemba 2013 kutoka asilimia 6.1 za mwezi Oktoba. Aidha amefafanua kuwa taarifa za matokeo ya mfumuko wa bei unaopimwa kwa kipimo cha mwezi unaonyesha kubaki kuwa asilimia 0.6 kama ilivyokuwa mwezi Oktoba huku fahirisi za bei zikiongezeka hadi kufikia 142.23 mwezi Novemba kutoka 141.39 za mwezi Oktoba

Amezitaja baadhi ya bidhaa za vyakula zilizochangia kwa kuongezeka kwa fahirisi za bei kuwa ni pamoja na mahindi kwa asilimia 2.4, vitafunwa ailimia 4.0, unga wa Muhogo kwa silimia 2.5, nyama kwa asilimia 1.1, kuku kwa asilimia 3.7, samaki waliokaushwa kwa mafuta kwa asilimia 5.2, nazi asilimia 5.7. Bidhaa nyingine ni pamoja na dagaa kwa asilimia 2.5, mbogamboga kwa asilimia 3.0, nyanya asilimia 6.0, Maharage 4.5, karoti kwa asilimia 5.8 na viazi mviringo asilimia 4.6.

Ameongeza kuwa mwenendo wa bei za bidhaa za vyakula hasa mchele kwa mwezi Novemba 2013 umeonyesha kupungua kwa asilimia 26.0 ikilinganishwa na mwezi Novemba mwaka 2012, bidhaa nyingine zilizopungua ni mahindi kwa asilimia 9.4, unga wa mahindi 5.7, viazi mviringo 7.6 na karanga kwa asilimia 9.7.

Kuhusu mchango wa bidhaa zisizo za chakula zilizochangia kupungua kwa mfumuko wa bei kwa kipimo cha mwezi Novemba 2013 ni pamoja na mitandao kwa asilimia 4.7, radio asilimia 4.3 na vifaa vya kielectroniki kama luninga kwa asilimia 2.7.

Hata hivyo kufuatia hali hiyo ya mfumuko wa bei Bw. Kwesigabo ameeleza kuwa uwezo wa shilingi 100 ya Tanzania katika kununua bidhaa na huduma za jamii kwa mwezi Novemba umeonyesha kuwa imara kwa kufikia shilingi 70 na senti 31.

“Napenda niwahakikishie kuwa fahirisi za bei za Taifa zimeonyesha kuwa na mwelekeo imara kwa kipindi chote, kwa hiyo uwezo wa shilingi 100 ya Tanzania katika kununua bidhaa na huduma umeonyesha kuwa na mwelekeo imara kwa kufikia shilingi 70 na senti 31 ” amesema.

Kuhusu ulinganifu mfumuko wa bei wa Tanzania na baadhi ya nchi za Afrika Mashariki amesema kuwa una mwelekeo unaofanana na kueleza kuwa mfumuko wa bei nchini Kenya umefikia asilimia 7.36 kwa mwezi Novemba kutoka asilimia 7.36 za mwezi Oktoba, huku nchini wa Uganda Ukifikia asilimia 6.8 kwa mwezi Novemba kutoka asilimia 8.1 za mwezi Oktoba.