Ngeleja, Katibu wake ‘matatani’, wabunge wagomea bajeti yake


Waziri Ngeleja akizungumza bungeni.

Dodoma,
IDADI kubwa ya wabunge wakiwemo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wameikataa bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini, na Serikali kuomba ikajipange upya kabla ya kuiwasilisha tena bajeti hiyo bungeni.

Mbali na Waziri Mkuu Pinda kuiondoa bajeti hiyo jana bungeni Dodoma, Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, David Jairo wapo matatani kutokana na tuhuma za kuchangisha fedha na hazijulikabi zemetumikaje.

Wabunge kwa pamoja sasa wamechachamaa na wanataka kujua sh. bilioni moja zilizochangishwa na Wizara hiyo zimetumikaje, kwa kuwa maelezo yake wakati zikichangishwa yanatatanisha.

Wamemtaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kumwagiza Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG), akague mara moja namna fedha hizo zilivyotumika.Akizungumza kuchangia bajeti la wizara hiyo, Mbunge wa Kilindi, Beatrice Shellukindo (CCM), jana alisema watendaji katika wizara hiyo ndiyo wanamuangusha Waziri William Ngeleja.

Alisema watendaji hao ndiyo wanaosababisha matatizo ya mgawo wa umeme kutomalizika.

“Ingawa niliombwa sana nisichangie hotuba hii, lakini nalazimika kuchangia kutokana na ukweli kwamba Watanzania wanataka umeme, Ngeleja ulikuwa waziri mzuri miaka ya nyuma, ulikuwa ukisoma bajeti kwa ‘confidence’.

Lakini katika hotuba yako hii ulikuwa unasoma kwa wasiwasi mkubwa, hii ni kutokana na mambo mengi kutokamilika, imejaa ahadi tupu.

Miradi uliyotusomea hapa inaanza 2015 sasa je, hapa katikati tunafanya nini? Watendaji wenu ndiyo wanawaangusha,” alisema Shellukindo.

Wakati akiendelea kuzungumza, Shellukindo alisema “hapa nina barua inazitaka taasisi 21 zilizochini ya wizara kuchangia sh. milioni 50, 000, 000 kila moja, gharama za kukamilisha maandalizi na uwasilishaji wa hotuba ya bajeti ya Wizara ya mwaka 2011/12 bungeni Dodoma”

“Barua hii imesainiwa na David Jairo, Katibu Mkuu wa Wizara, fedha hizi ziliagizwa kuwekwa katika akaunti namba 5051000068 NMB tawi la Dodoma, nimejaribu kufuatilia fedha hizi zimeshatolewa.

Leo nakusudia kuwasilisha hoja, naomba wabunge mniunge mkono bajeti irudishwe, na sitaunga mkono hoja mpaka mpaka niambiwe fedha hizi zimetumikaje. Barua hii nitaiwasilisha mezani Mheshimiwa Spika,” alisema.

Mbunge wa Simanjiro, Christopher ole Sendeka (CCM), alisema anaungana na Shellukindo katika hoja yake na kwamba na yeye amepelekewa barua hiyo.

“Tunamuomba Waziri Mkuu, amwagize CAG afanye ukaguzi leo hii fedha hizi zinalenga nini na kama kweli zipo kwenye akaunti hiyo.

Barua hiyo ninayo inazitaka taasisi 21 zichangie sh. milioni 50, 000, 000 kila moja, sasa tunataka kujua fedha hizi ambazo ni sawa na sh. bilioni moja zimeelekezwa wapi, hii ndiyo inatufanya tuamini maneno kwamba Wizara imeihonga kamati,” alisema ole Sendeka.
Mbunge huyo akiendelea kuchangia alilitaka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kuzingatia ratiba ya mgawo wa umeme na kwamba mgawo usiozingatia ratiba unahatarisha usalama wa wachimbaji katika mgodi wa Mererani.

Pia alihoji iwapo kama kweli Serikali inaguswa na tatizo lililopo la mgawo, kwanini isitenge fedha kwa ajili ya kununulia majenereta, lakini yenyewe imeng’ang’ania mitambo ya kukodi.

“Mwaka 2008 katika ripoti ya Dk. Harrison Mwakyembe (CCM), alipendekeza tuachane na mitambo ya kukodi, hivyo tufuate ushauri huo tusiwe na vichwa vigumu. Kuhusu mradi wa MW 60 kwa ajili ya kuzalisha umeme unaotarajiwa kujengwa Mwanza ni ufisadi mwingine utafanyaje kazi wakati hakuna gesi ya kutosha? hivyo sitaunga mkono hoja hii mpaka nitakapopata majibu ya kutosha,” alisema.

Barua hiyo ilisomeka kama ifuatavyo; Yahusu kuchangia gharama kukamilisha na kuwasilisha maandalizi na uwasilishaji wa hotuba ya bajeti ya wizara ya mwaka 2011/2012 bungeni Dodoma.

Wizara imefanikisha maandalizi ya Mpango na Bajeti kwa mwaka 2011/2012 na imekwisha pitishwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini. Katika kukamilisha mchakato huo, Hotuba ya Bajeti inatarajiwa kuwasilishwa bungeni Julai 15 na 18, 2011.

Kama ilivyo kawaida wakati wa kuwasilisha Hotuba ya Bajeti Dodoma, maofisa mbalimbali wa Wizara na Taasisi zilizochini yake huambatana na viongozi waandamizi kwa ajili ya kutoa ufafanuzi wa masuala yanayojitokeza wakati wa mjadala wa hotuba hiyo.

Ili kufanikisha mawasiliano ya hotuba hiyo ya bajeti unaombwa kuchangia jumla ya sh. 50,000,000 fedha hizo zitumwe Geological survey of Tanzania (GST), kwenye akaunti namba 5051000068 NMB tawi la Dodoma.

Baada ya kutuma fedha hizo Wizara ipewe taarifa kupitia ofisi ya DP kwa uratibu, na imesainiwa na David Jairo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini.