EAC Bado Inakazi Kubwa kwa Wakazi wa Holili na Miji Mingine ya Mipakani
Na MtuwaSalira, EANA
HOLILI ni Mji mdogo wenye wakazi wapatao 7,400 ulipo Kaskazini ya Tanzania mkoani Kilimanjaro, ukiwa umepakana na wilaya ya Taveta katika nchi jirani ya Kenya. Miaka kumi iliyopita Holili ilikuwa kama mji mwingine wowote ule wa mpakani, ukiwa na kazi ya kupitisha mizigo na watu baina ya nchi hizo mbili. Lakini sasa kufuatia kufufuliwa upya kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kumeanza kujitokeza masuala kadhaa chanya katika mji huo. EAC ilifufuliwa rasmi Novemba 30, 1999, kufuatia kuvunjika kwa jumuiya ya kwanza mwaka 1977.
Wanachama wa mwanzo kabisa wa jumuiya hiyo ni Kenya, Uganda na Tanzania. Nchi za Rwanda na Burundi zilijiunga na jumuiya hiyo mwaka 2007 na kuongeza idadi ya wananchama kuwa tano. Maombi ya nchi ya Sudani Kusini kujiunga katika jumuiya hiyo yanafanyiwa kazi na iwapo yatakukubali, nchi hiyo ikuwa ya sita katika EAC.
Lengo kuu la EAC ni kupanua na kuboresha mtangamano baina ya watu wa Afrika Mashariki ili kuongeza kasi ya kujiletea maendeleo ya kiuchumi na maisha katika kanda hiyo.
Tofauti na jumuiya ya awali, ambayo ilisemekana ilikuwa na mizizi ya nguvu zake kutoka kwa viongozi wa juu wa jumuiya hiyo, hiyo ya sasa inalenga mahususi watu wa ngazi ya chini kabisa, yaani raia wa kawaida katika kanda hii ya Afrika Mashariki.
Ni miaka zaidi ya 10 sasa tangu jumuiya hiyo ifufuliwe upya na watu wanaoishi katika miji ya kipakani kama vile Holili, wako katika mstari wa mbele katika mwingiliano na majirani zao kijamii, kiuchumi na kisiasa. Lakini watu wa mipakani hao wana nini cha kusema kuhusu mtangamano huo? Je wakazi wa Holili na miji mingine ya mipakani katika kanda wanafahamu uwepo wa jumuiyo hiyo? Wananufaika chochote kutokana na kuwepo kwake?
Kwa msaada wa Shirika la Ujerumani la Fridrich-Ebert-Stiftung (FES) ofisi ya Tanzania, Shirika Huru la Habari la Afrika Mashariki (EANA) ilitaka kubaini majibu ya maswali hayo katika mpaka wa Holili na miji jirani ya Himo kwa Tanzania na Taveta kwa upande wa Kenya.
Watu wapatao 50 walihojiwa katika miji ya Holili na Himo kwa upande wa Tanzania na Taveta kwa upande wa Kenya. Waliohojiwa ni pamoja na maafisa uhamiaji na mamlaka ya mapato, viongozi wa serikali za mitaa wa maeneo hayo, wafanyabiashara ndogondogo wa jinsia zote, vijana, waendesha bodaboda, wamiliki wa maduka na wanunuzi na wauzaji wa nafaka.
Mji wa Himo
Himo ni mji mdogo kwa upande wa Tanzania uliopo karibu na mpaka wa Kenya, umbali wa kilometa zipatayo 10 kutoka mji wa mpakani wa Holili. Mji huo una watu wapatao 22,442 na kati yao 11,661 ni wanawake huku 10,781 wakiwa wanaume. Shughuli za kiuchumi katika eneo hilo ni pamoja na kuuza bidhaa zinazotokana na uzalishaji katika kilimo: Mboga, ndizi, viazi na nazi. Lakini pia kunashughuli za uzalishaji wa tofali unaotokana na udongo wa volkano, huduma za upakiaji na upakuaji mizigo na usfiri ikiwa ni pamoja na ule wa bodaboda. Shughuli nyingine ni uuzaji wa bidhaa za viwandani, mafuta na uuchuuzi wa vyakula mbalimbali.
Himo ni kituo kikubwa cha kuhifadhi na uuzaji wa mifugo na nafaka kama mahindi, mtama, mchele na maharage. Wauzaji wa mahindi katika Mji wa Himo wanasema wanaijua EAC lakini wanadai kwamba jumuiya hiyo haiwasaidii kukuza biashara zao.
“EAC imeleta uhuru usio na kifani kwa wenzetu wa Kenya, ambao sasa wanaweza kununua mahindi moja kwa moja kutoka kwa wakulima hapa Tanzania na kusafirishwa kwenda Kenya. Hii inatishia uhai wa biashara yetu,” alisema mfanyabishara wa nafaka Modest Merkior.
Merkior alieleza kwamba awali, wafanyabiashara wa Kenya walikuwa wananunua mahindi na nafaka nyinghine katika soko la Himo lakini hivi sasa hali ni tofauti wananunua wenyewe moja kwa moja na hivyo kufanya wao kukosa cha kufanya.
Wafanyabishara wengine wanne wa mahindi na wamiliki wa ghala za mahindi mji mdogo wa Himo walikuwa na yao kuhusu wafanyabiashara wa Kenya. Samwel James, Chenono Herman, Dafa Abdi na Idrisa Mkwayu walisema serikali ya Tanzania haina budi kuweka sera ya upendeleo kwa wazawa ili kuwalinda na kile wanachokiita ‘kutotendewa haki sawa.’
“Uhuru huu kwa wafanyabiashara wa Kenya kuwasiliana moja kwa moja na wakulima katika maeneo mbalimbali ya Tanzania lazima udhibitiwe. Wanatakiwa waje Himo au maeneomengine yaliyotengwa kwa ajili ya kujinunulia mahindi. Huwezi mtanzania ukafanya hivi nchini Kenya,” James aliiambia EANA kwa uchungu.
Alisema iwapo zipo sababu za msingi kwa wageni kwenda maeneo ya pembezoni kununua mahindi na nafaka nyingine basi hawanabudi kufuatana na mtanzania. Amos Masiga, muuzaji wa mahindi na mmiliki wa ghala la kuhifadhia nafaka eneo hilo la Himo alisema tofauti na Kenya, wenye benki nchini Tanzania wamewatelekeza wafanyanishara wa nafaka kwa kutowauunga mkono kwenye biashara zao.
“Kwa nini benki kama vile NBC (Benki ya Taifa ya Biashara), Benki ya CRDB na nyingine zisitufuate kutuelimisha na kutupatia mikopo kwa ajili ya biashara zetu? Kwa nini wanajifungia maofisini badala ya kutoka nje kutufuata wateja? Ningekuwa na taasisi ya kifedha ya kunipatia mkopo bila shaka ningeboresha zaidi biashara yangu,” alisema Masiga.
Mji wa Holili
Wafanyabiashara katika mji wa Holili nao walikuwa na malalamiko yao dhidi ya chombo hicho cha kanda.” Jumuiya imeundwa kwa ajili ya kuwanufaisha matajiri na wenye nguvu. Hiki ndicho kinachosemwa na watu wanaoishi hapa mpakani. Raia wa kawaida kama sisi wanasumbuliwa mpakani na maafisa uhamiaji, polisi na mamlaka ya mapato kutokana na sababu kuanzia za kukosa hati halali ya kusafiria, kadi ya chanjo ya ugonjwa wa manjano na kodi kwa bidhaa zilizonunuliwa toka pande zote mbili,” alisema Paul Ngome dereva wa bodaboda wa Holili.
Ngome aliongeza kwamba jumuiya haina maana yoyote kwake na kwa raia wengine katika eneo hilo. Alitoa wito kwa wakuu wa EAC kuachana na hitaji la kadi ya chanjo ya ugonjwa wa manjano akisema kwamba raia wasisumbuliwe kwa vitu vidovidogo kama hivyo na waruhusiwe kuwa huru kuvuka mpaka.
Mawazo yake yaliungwa mkono na dereva mwingine wa bodaboda katika eneo hilo, Vincent Kibwana: “Sinufaiki chochote na mtangamano wa Afrika Mashariki.’’
Lakini maoni hayo yametofautina kabisa na yale yalitotolewa na Raymond Motesha, mfanyakazi wa zamani wa EAC na sasa anaishi Holili. Yeye hakuweza kuficha furaha yake. Alisema alionja matunda ya jumuiya ya zamani na kwamba anafurahia hatua ya kufufua umpya jumuiya hiyo.
“EAC ni muhimu kwa sababu usumbufu ulikuwepo hapo awali haupo tena.Watu wanaweza kuvuka mpaka kwenda upande wotewote pasipo kubughudhiwa,” alieleza.
Kwa bahati mbaya alisema, watu wengi hawajui kuhusu uwepo wa jumuiya na faida zake. Alitoa wito kwa wenye mamlaka kuandaa kampeni ya kuhamasisha uelewa wa jumuiya kupitia vyombo vya habari ikiwa ni pamoja na radio, televisheni na magazeti. Akiwa kama mfanyakazi wa zamani wa EAC katika idara ya huduma ya chakula, iliikumbusha serikali ya Tanzania kukamilisha kuwalipa mafao yao akidai kwamba alishalipwa robo tu ya madai yake.
Frank Uroki ni miongoni mwa watu lukuki wanaofanya biashara ya kubadilisha fedha za kigeni kwenye lango kuu la kituo cha mpakani cha Holili. Alisema ana ufahamu kidogo sana juu ya EAC na pia hajui kwamba ina manufaa gani.’’ Maafisa wa serikali hawajali kuwaelimisha watu kuhusi masuala ya msingi kama vile ya kodi na mahusiano baina ya watu mipakani,’’ alieleza.
Uroki pia alitoa wito wa kufanyika kwa kampeni ya makusudi ya EAC kuweza kuwafikia watu katika ngazi za chini kabisa. Mfanyabiashara wa kuuza chakula Holili, Jacqueline Moke alisema amewahi kusikia kuhusu jumuiya lakini hajui anawezaje kunufaika nayo.
“Ningeifahamu vizuri zaidi kama kungetolewa mikopo kwa watu kama sisi,” alifafanua.
Alisema huwa anavuka kwenda Taveta (Kenya) mara nyingi kwa ajili ya kununua mahitaji bila kubughudhiwa hususan katika siku za soko.
Naye mmiliki wa duka la vifaa vya ofisini katika eneo hilo, Roze Wilfred alisema amekuwa akisikia juu ya jumuiya ya Afrika Mashariki lakini hajui manufaa yake.’’ Wafanyabishara na raia wengine hawanabudi kuelemishwa juu ya jumuiya,’’ alisisitiza.
Justus Muyombo, mwenyekiti wa kikunchi kinachojishughulisha na utengeneza wa matofali ya udongo wa volkano Holili alieleza kwamba alisikia taarifa kuhusu jumuiya kupita vyombo vya habari lakini hakuweza kuelezea zaidi ya hapo. Anakiri kwamba yeye huvuka mpakani kwenda Taveta bila kupata matatizo na kuongeza kwamba jumuiya ni muhimu kwa ajili ya ustawi wao. “Taarifa zaidi sipelekwe kwa wananchi ili waweze kuifahamu zaidi jumuiya,” alihitimisha.
Victor Ramadhani na Abdi Ramadhani wa Holili Check Point Group wanaojishgulisha na huduma ya upakiaji na upoakiaji miozigo mpakani hapo walisema wamewahi kusikia juu ya EAC lakini hawajui ina manufaa gani. Edward Urio, mwanachama kikundi cha Nguvu Kazi, alijikia kuwa na bahati ya kupata nafasi ya kufahamu zaidi mtangamano wa EAC.
“Nimebahatika kushiriki katika mikutano ya Ujirani Mwema iliyokuwa inafanyika Himo na Taveta ambayo mwanachi wa kawaida hakuweza kushiriki. Washiriki wengi walikuwa wanatoka katika idara za uhamiaji, polisi, mamlaka ya mapato, maafisa wanaoshugulikia upokeaji na usafirishaji mizigo na wafanyabiashara wacheche waliochaguliwa.Mwenendo huu hauna budi kubadilishwa kwa kufanya mikutano ya hadhara ili watu wengi zaidi waweze kushiriki,’’ alieleza.
Naye Ali Msangi, mfanyabishara wa rejareja Holili alisema bado yuko gizani kuweza kuelewa ni nini hasa jumuiya inafanya. “Tuna wasiwasi kwamba EAC ni mtangamano wa viongozi peke yao.”
Mji wa Taveta
Taveta ni mji wa mpakani kwa upande wa Kenya ulipo umbali wa kilometa 5 kutoka mpaka wa Holili. Mji huo una idadi ya watu 9,632 wakiwemo wanawake 4,851 na wanaume 4,781. Shughuki za kiuchumi katika mji huo zinafanana na zile zilizopo katika miji miwili ya awali ya Himo na Holili. Wafanyabiashara wadogo katika mji huo huuza bidhaa zinazotokana na kilimo kama vile mboga, ndizi na viazi. Pia kuna shughuli za kutoa huduma ya kupakia na kupakua mizigo na shughuli za usafirishaji ikiwa ni pamoja na bodaboda. Yapo pia maduka ya rejareja, uchuuzi wa chakula na ubadilishaji wa fedha za kigeni. Sambamba na shughuli hizo pia ipo biashara ya bidhaa kutoka viwandani kama vile vifaa ya matumizi ya nyumbani, chupa za chai,chumvi, mafuta ya kupikia, vifungashio, dawa za meno, sabuni, pipi, malighafi za ujenzi, saruji na vifaa vya kufanyia usafi wa mazingira.
Mfanyabiashara ndogondogo wa Taveta, Priva Mwabile alisema alifahumu uwepo wa jumuiya ya Afrika Mashariki kupitia mkutano mmoja aliohudhuria. Alisema anahitaji kujieleza sana mbele ya polisi na maafisa uhamiaji kila inapombidi kuvuka mpaka kwenda Tanzania. Alitoa wito kwa jumuiya kufanya juhudi za kuelimisha umma kuhusu malengo ya jumuiya hiyo. Pia alisema kwamba ipo haja ya kuweka huduma zinazofanana kwa pande zote mbili za mpakani ili mambo yaende vizuri zaidi.
Juma Machila kama alivyo Mwabile alisema inaifahamu jumuiya kupitia mikutano ya Ujirani Mwema. Alisema kabla ya mikutano hiyo kulikuwapo matatizo lukuki ya kiutendaji-hususan ni katika suala zima la kuvusha watu na mizigo mpakani. Hali sasa ni bora zaidi.
Machila ameitaka EAC kuondoa vikwazo vyote. “Kama inawezekana basi tuwe na kitambulisho cha aina moja cha EAC. Jumuiya ni nzuri kwetu kwani imekuwa ikiimarisha mtangamano na biashara mpakani. Jumuiya ni muhimu sana.”
Mfanyabiashara mdogo mwingine, Nzuki Daniel hakuacha kutoa maoni yake: ”EAC haina budi kufanya kampeni ya kuhamasisha wananchi katika nchi zote tano wananchama, hususan karibu na mipakani kuhusu faida inazoweza kuwapatia raia wa Afrika Mashariki.”
Naye Daniel Nduku, Mganga wa Jadi wa Kenya alisema anafahamu kuwa EAC ilikuwa inarejea umpya taratibu lakini aliongeza kwamba inahitajika juhudi zaidi. Alisema si rahisi kwake kufanyabiashara katika mji wa karibu wa Himo, nchini Tanzania kutokana na vikwazo vya masula ya uhamiaji ambayo amesema siyo ya muhimu.
Mfanyabiashra wa ndizi, Dezi Munene alisema aliwahi kusikia juu ya EAC lakini anahitaji taarifa zaidi. ”Watu wanahitajika kupewa semina juu ya jambo hili.”
Kwa upande wake, Mary Munene, mmiliki wa duka la rejareja Taveta alisema amewahi kusikia habari za jumuiya lakini hakufaya ufuatiliaji wowote kupata taarifa zaidi. Bila kutoa ufafanuzi alisema jumuiya ni muhimu kwa mtangamano wa watu.
Viongozi mpakani wanasemaje?
Frederick Kiondo, Afisa Uhamiaji Kiongozi katika Kituo cha Holili upande wa Tanzania ambaye kishahamishiwa kituo kingine cha kazi, alisema raia kutoa pande zote mbili wamekuwa wakifurahia huduma za uhamiaji walizokuwa wanapata kwa kuzingatia sheria zinazotawala mambo ya uhamiaji katika kuvuka mpaka ambazo alisema bado zipo zinafanyakazi. Alifafanua kwamba ingawaje EAC imefufuliwa upya, sheria bado inatamka kwamba raia wanaweza kuvuka mpaka kwenda nchi nyingine kwa sababu yoyote ile baada ya kutoa hati halali ya uhamiaji kama vile hati ya kusafiria na kibali cha ruhusa.
Alieleza kwamba sheria za uhamiaji zinakataza kwa mgeni kuajiriwa,kufanya biashara na kusoma nchini Tanzania bila kibali. Wakati wa siku za soko Taveta kwa upande wa Kenya na Himo kwa Tanzania alisema watu huwa huru kuvuka mpaka kwenda upande wowote mradi wazingatie mamboya masingi yanayotakiwa.
“Tutakuwa na uhuru kamili katika masuala ya uhamiaji tutakafika hatua ya kuwa na Shirikisho la Afrika Mashariki kwa sababu wakati huo tutakuwa nchi moja,” Kiondo alifafanua.
Alisema kwamba kwa sasa elimu na uhamasishaji kuhusu mambo ya EAC inahitajika zaidi kwa watu wanaoishi mpakani. Vyombo vya habari kama vile radio, televisheni na magazeti vinaweza kutumika ipasavyo kwa lengo hilo, aliongeza.
Diwani wa Kata ya Holili, Onesmo Myombo alisema anafahamu uwepo wa EAC lakini anakerwa na bughudha wanayopata watu wa kawaida kwa pande zote mbili wanapovuka mpaka. Anasema wanasumbuliwa na polisi, idara za uhamiaji na mamlaka za mapato wanapovuka mpaka kwa ajili ya shughuli zao. Usumbufu huo alisema unawagusa zaidi watu wasiokuwa na vibaki halali vya kusafiria na wale ambao hawana leseni hususan ni kwa madereva wa bodaboda. Watanzania wengi anadai wamekamatwa na hata kuhukumiwa vifungo Taveta kwa kukosa hati hizo. Licha ya tatizo hilo watu huwa huru kwenda upande wowote wa mpaka kwa ajili ya shughuli.
Diwani huyo alidokeza pia kwamba upo uelewa mdogo juu ya shuhguli na mipango ya EAC kwa wananchi wa kawaida na hivyo kutoa wito wa kufanyika kwa juhudi za makusudi za kuwahamasisha watu juu ya umuhimu wa mtangamano wa kanda.
Naye Elinamu Malle, Afisa Mtendaji Kata ya Himo, alisema watu wengi wanaufahamu wa jumla kuhusu EAC na wamekuwa wakifanya biashara na wenzao katika bidhaa zinazotokana na kilimo hususan ni nafaka kama vile mahindi, mchele na maharage. Lakini pia alisema wanafanya biashara katika bidhaa zinazozalishwa viwandani kama vile mafuta na vifaa vya ujenzi.
“Tofauti na miaka ya nyuma ambapo biashara nyingi zilifanyika kwa kupitia njia za panya, siku hizi biashara nyingi zinapitia katika mpaka wa Hoili. Ukusanyaji wa ushuru umeongezeko zaidi na kisha matunda yake kushika hadi kwa ngazi ya kijiji, wilaya na mamlaka ya mapato,” alieleza kwa ufasaha.
Afisa Uhamiaji wa Kenya katika kituo cha Holili, Lucas Malimali alisema jumuiya imesadia vilivyo kuboresha uhusinao baina ya watu wa mataifa hayo mawili katika mpaka huo.” Tunao marafiki na jamaa zetu ambao wanapata huduma za matibabu katika hospitali za Tanzania kama vile Marangu na KCMC. Pasipo Jumuyia tusingepata huduma hii muhimu.”
Naye Mkuu wa Wilaya ya Taveta nchini Kenya, Nkaduda Hiribae alisema, “Kama unafika Taveta siku ya soko huwezi kutofautisha kati ya Mkenya na Mtanzania. Wanazungumza masuala ya biashara kwa Kiswahili kwa maelewano makubwa. Wagonjwa wetu wanapata huduma za matibabu kwenye zahanati na hospitali za Tanzania zilizokaribu. Watu hapa wanajua EAC ipo kwa sababu gani.”
Lakini pia amekiri kwamba yapo matatizo kadhaa hutokea. “Baadhi ya watu wanaweza kutiwa mbaroni au wanapoulizwa vibali vya uhamiaji wataanza kulalamika. Lakini kwa ujumla tunafurahia uhusiano mzuri uliopo na jirani zetu watanzania. Watu wetu hupata matibabu katika hospitali ya Marangu ma watanzania huleta mifugo yao eneo la Kitobo, upande wa Kenya kwa ajili ya huduma ya maji. Lakini binadamu ni wagumu. Baadhi kamwe hawaridhiki.Kila mara wanataka kupata zaidi,” alihitimisha Hiribae.