CHADEMA Yaendelea Kupukutika, Kigogo Mwingine Ajiuzulu Singida

Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Wilbrod Slaa

Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Wilbrod Slaa

Na Mwandishi Wetu, Singida

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Mkoa wa Singida amejuuzulu. Wilfred Kitundu aliyekuwa kiongozi wa juu mkoani hapa na mwenye kadi namba 300 ameamua kubwaga manyanga nafasi yake ya uenyekiti kwa kile kutoridhishwa na maamuzi ya Kamati Kuu ya chama hicho yaliyofanywa hivi karibuni ya kuwavua uongozi Zitto Kabwe, Dk Kitila Mkumbo na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba.

“Ninapenda kukuarifu kuwa nimeamua kujiuuzuru nafasi yangu ya uenyekiti wa mkoa ambayo nimekuwa nikiitumikia kwa kipindi kirefu sasa kama kielelezo cha kuamini na kudai demokrasia ya kweli ndani ya chama. Ikumbukwe kwamba mimi ndio mwanachama wa kwanza kujiunga na CHADEMA mkoa wa SINGIDA na ni mwanachama wa 300 kitaifa, hiyo ni heshima kubwa sana kwangu na sipo tayari kuipoteza kwa kukubali kuwa sehemu ya udharirishaji huu wa demokrasia uliopitiliza,” alisema Kitundu katika taarifa yake.
 
Kiongozi huyo aliongeza kuwa hakuridhishwa na uamuzi na vitendo vinavyoendelea ndani ya chadema kwa sasa na amevifananisha vitendo hivyo na ubakaji na udharirishaji wa demokrasia ya kweli inayohubiriwa na chama hicho mbele ya umma kila uchao.
 
“Kwa barua hii basi, nimeona bora mfahamu kuwa si vema mimi kuendelea kupingana na dhamira yangu inayonituma kuwa mwanademokrasia wa kweli. Ninatanguliza shukrani zangu za dhati kwa wanachadema wote wanaopinga upuuzi huu uliofanywa na kamati kuu ya chama.
 
Kusimamia haki, katiba na misingi ya chama ni wajibu wangu, hivyo kwa namna yoyote ile sitaweza kuwa tayari kufumba macho pindi ujinga wa namna hii unapoendelea kutekelezwa kwa uwoga wa uchaguzi.” Ilisema taarifa hiyo.