Serikali Yatia Saini Ujenzi wa Barabara wa Bilioni 538

“Napenda kuwatahadharisha nyie makandarasi mlioko hapa kama kuna yeyote kati yenu hataweza kufanya kazi kwa ubora na wakati basi asisaini mkataba huu”, alisema Dkt Magufuli

“Napenda kuwatahadharisha nyie makandarasi mlioko hapa kama kuna yeyote kati yenu hataweza kufanya kazi kwa ubora na wakati basi asisaini mkataba huu”, alisema Dkt Magufuli

Na Eliphace Marwa (Maelezo)
SERIKALI imetia saini mikataba mitatu ya ujenzi wa barabara yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni Tsh.538 za Kitanzania kwa ushirikiano toka Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) na Shirika la Maendeleo la Japan (JICA) mapema hii
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa sherehe za kutia saini mikataba hiyo,Mtendaji Mkuu wa TANROADS Mhandisi Patrck Mfugale alisema kati ya fedha hizo ADB wanachagia asilimia 65.80 , JICA asilimia 29.2 ambazo wametoa mkopo na Serikali inachangia asilimia tano.
“Mikataba iliyotiliwa saini hii leo ni pamoja na ujenzi wa sehemu ya Mayamaya hadi Mela yenye urefu wa kilomita 99.35 inayojengwa na Kampuni ya China Henan International Cooperation Group Co. Ltd (CHICO) kwa gharama ya zaidi bilioni mia moja kwa muda wa miezi thelasini na sita,” alisema Mfugale.

Alizitaja barabara nyingine ni Mela hadi Bonga yenye urefu wa kilomita 88.8 inayojengwa na Kampuni ya China Railway Seventh Group kwa gharama ya zaidi Sh. bilioni 88 , ambapo muda wa utekelezaji ni miezi thelasini na sita.

Mkataba wa mwisho ni wa ujenzi wa barabara ya Mangaka hadi Mtambaswala yenye urefu wa kilomita 65.5 itakayojengwa na Kampuni ya Sichuan Road and Bridge (Group) Corporation kwa gharama ya zaidi ya Sh.bilioni 59 na muda wa utekelezaji ni miezi ishirini na nne.

“Napenda kuwapongeza Benki ya Maendeleo ya Afrika pamoja na Shirika la Maendeleo la Japan kwa ushirikiano wao kwani sio mara ya kwanza kutupatia mkopo kwa ajili ya ujenzi wa barabara zetu na tunaahidi kuzisimamia ili ziwe katika ubora unaotakiwa”, alisema Mfugale.

Aidha naye Waziri mwenye dhamana ya ujenzi Dkt. John Magufuli alishukuru ADB na JICA kwa mkopo huo na kutoa angalizo kwa wakandarasi wasio makini na kazi zao kukaa chonjo kwani sasa hakuna huruma kwao tena.

“Napenda kuwatahadharisha nyie makandarasi mlioko hapa kama kuna yeyote kati yenu hataweza kufanya kazi kwa ubora na wakati basi asisaini mkataba huu”, alisema Dkt Magufuli.

Nao wawakilishi toka ADB na JICA walimshukuru Waziri Magufuli kwa usimamizi imara wa miradi mbalimbali ujenzi inayoendelea kote nchini.

Hii si mara ya kwanza kwa ADB na JICA kutoa mkopo kwa ajili ya ujenzi wa barabara kwani Machi mwaka , 2010 walitoa mkopo kwa ajili ya ujenzi wa barabara za Iringa mpaka Dodoma yenye urefu wa kilomita 260 na barabara ya Namtumbo mpaka Tunduru yenye urefu wa kilomita 193.