Baba mzazi wa Marehemu Peter (Pichani), Mzee Mangula, ambaye ni Makamu Mwenyeiti wa CCM Taifa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia Salamu za Rambirambi Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi, Mheshimiwa Philip Mangula kufuatia kifo cha Mtoto wake Peter Philip Mangula kilichotokea tarehe 26 Novemba, 2013 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) alikokuwa amepelekwa kwa matibabu akisumbuliwa na ugonjwa wa shinikizo la damu.
“Nimeshtushwa, nimesikitishwa na kuhuzunishwa sana kutokana na taarifa za kifo cha Mwanao Peter Philip Mangula aliyefariki dunia tarehe 26 Novemba, 2013 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili akipatiwa matibabu ya shinikizo la damu”, amesema kwa masikitiko Rais Kikwete katika Salamu zake.
Rais Kikwete ameongeza kusema kuwa “amesikitishwa zaidi na taarifa za kifo cha Peter Philip Mangula kwa kuzingatia kwamba ni katika kipindi kifupi kilichopita, Mheshimiwa Mangula alimpoteza Binti yake, Neema Nemela Mangula aliyefariki dunia kutokana na ajali ya gari, hivyo ni dhahiri kwamba kifo cha kijana wake huyu kimeongeza machungu na simanzi kwa familia ya Mheshimiwa Mangula na kimesababisha pengo kubwa kwa wanafamilia kwa ujumla”.
“Kutokana na taarifa hizo za kusikitisha, ninakutumia wewe Mheshimiwa Philip Mangula Salamu zangu za Rambirambi na pole nyingi kwako wewe binafsi na kwa familia yako yote kwa ujumla kwa kupotelewa na Peter Philip Mangula”.
“Ninamuomba Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema akujalie wewe na familia yako moyo wa uvumilivu na ujasiri ili muweze kuhimili machungu ya kuondokewa na kijana wenu kwa kutambua kwamba yote ni Mapenzi yake Mola”, amesema Rais Kikwete na kuongeza kuwa anamuomba Mola aipokee na kuipumzisha Mahala Pema Peponi Roho ya Marehemu Peter Philip Mangula, Amina.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
27 Novemba, 2013