JK Atuma Rambirambi Kifo cha Prof. Gabriel Mwaluko

Rais wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete

Rais wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete

RAIS Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Chuo Kikuu cha St Johnes kilichoko Dodoma kufuatia kifo cha Makamu Mkuu wa Chuo hicho Prof. Gabriel Mwaluko aliyefariki tarehe 11 Novemba, 2013 nchini India alipokuwa anapatiwa matibabu.

“Hakika Taifa limempoteza msomi, kiongozi na mzalendo wa kweli, ni pigo kubwa sio kwa Chuo Kikuu cha St. Johnes tu bali Taifa kwa ujumla” Rais amesema.

Rais amemuelezea Prof Mwaluko kama kiongozi mchapa kazi, muadilifu na mzalendo aliyezaliwa na kipaji cha uongozi ambacho amekitumia vyema kwa manufaa ya watoto wa Tanzania, taasisi mbalimbali ambazo amewahi kushika uongozi na Taifa kwa ujumla pia Jumuiya ya kimataifa.

Rais pia amemtumia rambirambi mjane, watoto na familia ya marehemu Prof. Mwaluko na kuwataka wawe na moyo wa subira na kumuombea marehemu mapumziko mema kwani ndiyo mipango ya Mwenyezi Mungu.

Prof. Mwaluko ameshika wadhifa wa Makamu Mkuu wa Chuo cha St. Johnes kilichoko Dodoma tangu Januari, 2012. Marehemu amezikwa kijijini kwao Chikuyu Wilayani Manyoni Mkoa wa Singida.