Na Mtuwa Salira, EANA, Arusha
HOLILI ni mji mdogo wenye wakazi wapatao 7,400 ulipo Kaskazini ya Tanzania mkoani Kilimanjaro, ukiwa umepakana na wilaya ya Taveta katika nchi jirani ya Kenya. Miaka kumi iliyopita Holili ilikuwa kama mji mwingine wowote ule wa mpakani, ukiwa na kazi ya kupitisha mizigo na watu baina ya nchi hizo mbili. Lakini sasa kufuatia kufufuliwa upya kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kumeanza kujitokeza masuala kadhaa chanya katika mji huo. EAC ilifufuliwa rasmi Novemba 30, 1999, kufuatia kuvunjika kwa jumuiya ya kwanza mwaka 1977.
Wanachama wa mwanzo kabisa wa jumuiya hiyo ni Kenya, Uganda na Tanzania. Nchi za Rwanda na Burundi zilijiunga na jumuiya hiyo mwaka 2007 na kuongeza idadi ya wananchama kuwa tano. Maombi ya nchi ya Sudani Kusini kujiunga katika jumuiya hiyo yanafanyiwa kazi na iwapo yatakukubali, nchi hiyo ikuwa ya sita katika EAC. Lengo kuu la EAC ni kupanua na kuboresha mtangamano baina ya watu wa Afrika Mashariki ili kuongeza kasi ya kujiletea maendeleo ya kiuchumi na maisha katika kanda hiyo.
Tofauti na jumuiya ya awali, ambayo ilisemekana ilikuwa na mizizi ya nguvu zake kutoka kwa viongozi wa juu wa jumuiya hiyo, hiyo ya sasa inalenga mahususi watu wa ngazi ya chini kabisa, yaani raia wa kawaida katika kanda hii ya Afrika Mashariki.
Ni miaka zaidi ya 10 sasa tangu jumuiya hiyo ifufuliwe upya na watu wanaoishi katika miji ya kipakani kama vile Holili, wako katika mstari wa mbele katika mwingiliano na majirani zao kijamii, kiuchumi na kisiasa. Lakini watu wa mipakani hao wana nini cha kusema kuhusu mtangamano huo? Je wakazi wa Holili na miji mingine ya mipakani katika kanda wanafahamu uwepo wa jumuiyo hiyo? Wananufaika chochote kutokana na kuwepo kwake?
Kwa msaada wa Shirika la Ujerumani la Fridrich-Ebert-Stiftung (FES) ofisi ya Tanzania, Shirika Huru la Habari la Afrika Mashariki (EANA) ilitaka kubaini majibu ya maswali hayo katika mpaka wa Holili na miji jirani ya Himo kwa Tanzania na Taveta kwa upande wa Kenya.
Watu wapatao 50 walihojiwa katika miji ya Holili na Himo kwa upande wa Tanzania na Taveta kwa upande wa Kenya. Waliohojiwa ni pamoja na maafisa uhamiaji na mamlaka ya mapato, viongozi wa serikali za mitaa wa maeneo hayo, wafanyabiashara ndogondogo wa jinsia zote, vijana, waendesha bodaboda, wamiliki wa maduka na wanunuzi na wauzaji wa nafaka.
Mji wa Himo
Himo ni mji mdogo kwa upande wa Tanzania uliopo karibu na mpaka wa Kenya,umbali wa kilometa zipatayo 10 kutoka mji wa mpakani wa Holili. Mji huo una watu wapatao 22,442 na kati yao 11,661 ni wanawake huku 10,781 wakiwa wanaume. Shughuli za kiuchumi katika eneo hilo ni pamoja na kuuza bidhaa zinazotokana na uzalishaji katika kilimo: Mboga, ndizi, viazi na nazi. Lakini pia kunashughuli za uzalishaji wa tofali unaotokana na udongo wa volkano, huduma za upakiaji na upakuaji mizigo na usfiri ikiwa ni pamoja na ule wa bodaboda. Shughuli nyingine ni uuzaji wa bidhaa za viwandani, mafuta na uuchuuzi wa vyakula mbalimbali.
Himo ni kituo kikubwa cha kuhifadhi na uuzaji wa mifugo na nafaka kama mahindi, mtama, mchele na maharage. Wauzaji wa mahindi katika mji wa Himo wanasema wanaijua EAC lakini wanadai kwamba jumuiya hiyo haiwasaidii kukuza biashara zao.
“EAC imeleta uhuru usio na kifani kwa wenzetu wa Kenya, ambao sasa wanaweza kununua mahindi moja kwa moja kutoka kwa wakulima hapa Tanzania na kusafirishwa kwenda Kenya. Hii inatishia uhai wa biashara yetu,” alisema mfanyabishara wa nafaka Modest Merkior.
Merkior alieleza kwamba awali, wafanyabiashara wa Kenya walikuwa wananunua mahindi na nafaka nyinghine katika soko la Himo lakini hivi sasa hali ni tofauti wananunua wenyewe moja kwa moja na hivyo kufanya wao kukosa cha kufanya.
Wafanyabishara wengine wanne wa mahindi na wamiliki wa ghala za mahindi mji mdogo wa Himo walikuwa na yao kuhusu wafanyabiashara wa Kenya. Samwel James, Chenono Herman, Dafa Abdi na Idrisa Mkwayu walisema serikali ya Tanzania haina budi kuweka sera ya upendeleo kwa wazawa ili kuwalinda na kile wanachokiita “kutotendewa haki sawa.”
“Uhuru huu kwa wafanyabiashara wa Kenya kuwasiliana moja kwa moja na wakulima katika maeneo mbalimbali ya Tanzania lazima udhibitiwe. Wanatakiwa waje Himo au maeneomengine yaliyotengwa kwa ajili ya kujinunulia mahindi. Huwezi mtanzania ukafanya hivi nchini Kenya,’’ James aliiambia EANA kwa uchungu.
Alisema iwapo zipo sababu za msingi kwa wageni kwenda maeneo ya pembezoni kununua mahindi na nafaka nyingine basi hawanabudi kufuatana na mtanzania. Amos Masiga, muuzaji wa mahindi na mmiliki wa ghala la kuhifadhia nafaka eneo hilo la Himo alisema tofauti na Kenya, wenye benki nchini Tanzania wamewatelekeza wafanyanishara wa nafaka kwa kutowauunga mkono kwenye biashara zao.
“Kwa nini benki kama vile NBC (Benki ya Taifa ya Biashara),Benki ya CRDB na nyingine zisitufuate kutuelimisha na kutupatia mikopo kwa ajili ya biashara zetu? Kwa nini wanajifungia maofisini badala ya kutoka nje kutufuata wateja? Ningekuwa na taasisi ya kifedha ya kunipatia mkopo bila shaka ningeboresha zaidi biashara yangu,’’ alisema Masiga.
Mji wa Holili
Wafanyabiashara katika mji wa Holili nao walikuwa na malalamiko yao dhidi ya chombo hicho cha kanda.” Jumuiya imeundwa kwa ajili ya kuwanufaisha matajiri na wenye nguvu. Hiki ndicho kinachosemwa na watu wanaoishi hapa mpakani. Raia wa kawaida kama sisi wanasumbuliwa mpakani na maafisa uhamiaji, polisi na mamlaka ya mapato kutokana na sababu kuanzia za kukosa hati halali ya kusafiria, kadi ya chanjo ya ugonjwa wa manjano na kodi kwa bidhaa zilizonunuliwa toka pande zote mbili,” alisema Paul Ngome dereva wa bodaboda wa Holili.
Ngome aliongeza kwamba jumuiya haina maana yoyote kwake na kwa raia wengine katika eneo hilo.Alitoa wito kwa wakuu wa EAC kuachana na hitaji la kadi ya chanjo ya ugonjwa wa manjano akisema kwamba raia wasisumbuliwe kwa vitu vidovidogo kama hivyo na waruhusiwe kuwa huru kuvuka mpaka.
Mawazo yake yaliungwa mkono na dereva mwingine wa bodaboda katika eneo hilo, Vincent Kibwana:’’Sinufaiki chochote na mtangamano wa Afrika Mashariki.’’
Lakini maoni hayo yametofautina kabisa na yale yalitotolewa na Raymond Motesha, mfanyakazi wa zamani wa EAC na sasa anaishi Holili.Yeye hakuweza kuficha furaha yake.Alisema alionja matunda ya jumuiya ya zamani na kwamba anafurahia hatua ya kufufua umpya jumuiya hiyo.
“EAC ni muhimu kwa sababu usumbufu ulikuwepo hapo awali haupo tena.Watu wanaweza kuvuka mpaka kwenda upande wotewote pasipo kubughudhiwa,” alieleza.