CRDB Yatoa Semina ya Ujasiliamali kwa Akinamama

Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, Dk. Charles Kimei

Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, Dk. Charles Kimei

Anthony Komanya, Shinyanga
 
WAFANYABIASHARA wanawake wamekumbushwa kuitumia fursa ya uwepo wa Kitengo cha Kusaidia wafanyabiashara wadogo katika Benki ya CRDB kujisajiri kuwa Wateja na hatimaye kuweza kuchukua mikopo ili kukuza mitaji yao.

Maneja wa Banki ya CRDB Tawi la Shinyanga, Saidi Pamui alitoa changamoto hiyo wakati akiwakaribisha mamia mengi ya wanawake wajasiriamali wadogo na wa kati kushiriki semina ya Wajasiliamali juu ya Elimu ya Huduma ya taasisi za kifedha kwa wajasiriamali wanawake yaliyofanyika mjini Shinyanga juzi.
 
Akizungumza katika semina hiyo ya siku moja leo Meneja wa tawi hilo alisema kuwa wameamua kuendesha mafunzo hayo kutokana wengi wa akina mama wa mjini hapa wamekuwa hawajui jinsi ya kupata mitaji ya kuendesha biashara na hivyo kushindwa kuinuka kiuchumi

Alitaja baadhi ya fursa kwa wanawake zinazoweza kupatikana kupitia kitengo hicho kuwa pamoja na uwezekano wa kuchukua mikopo ya kufanyia biashara, na mikopo ya uwekezaji kwa ajili ya shughuli maalumu za kiuchumi.

Akaunti nyingine kwa wakinamama wajasiriamali ni ile inayofahamika kama ‘Akaunti ya Malkia’, ambayo ni kwa wanawake tu.

Katika akaunti hii mteja (mwanamke) hujiwekea akiba kidogo kidogo kwa muda maalumu na  kwa malengo maalumu kisha kuzifanyia kazi muda ufikapo ili kutimiza malengo aliyojiwekea.
 
“Tumeamua kutoa semina hii ya ujasiliamali kwa akina mama wa mjini hapa ilikuwapa elimu ya kupata mitaji ya kuendesha biashara zao na kuinuka kiuchumi ikiwa ni pamoja na kuondoa tamaduni ya mfumo dume ambayo hurudisha nyuma maendeleo ya nchi”, alisisitiza Pamui.
 
Hata hivyo meneja huyo aliwataka wakina mama wanaofanya Biashara ndogondogo kuunda vikundi vya ujasiliamali ambavyo vitawasaidia kupata mikopo kwa urahisi hali ambayo itawasaidia kukuza biashara zao na kuinuka kiuchumi.

“Kinachotakiwa ni wakinamama kuwa na mawasiliano ya karibu na Benki ya CRDB, na kuzungumza na watumishi kwa ajili ya kupata maelekezo”, aliendelea kusisitiza.

Kwa upande wake Afisa Mikopo wa CRDB Claudina William, akitoa mada kwa wajasiriamali hao wanawake, alitaja baadhi ya masharti ya kuwa mteja wa CRDB ni kufungua akaunti baada ya kuleta kitambulisho, picha mbili za passport, na leseni ya biashara ya mhusika.
 
Aidha kwa upande wake mgeni Rasmi kwenye semina hiyo Mariamu Rufunga(mke wa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga) aliwataka wakina mama wanapochukua mikopo hiyo waitumie katika shughuli za maendeleo na siyo kwa matumizi mengine yasiyo na tija.
 
Alisema Baadhi ya kina mama wamekuwa wakichukua mikopo na kushindwa kuitumia kwa matumizi yaliyo kusudiwa ya kimaendeleo na hivyo kushidwa kumudu kurejesha mkopo huo na matokeo yake kufirisiwa kwa kunyang’anywa mali alizoweka Dhamana

Kwa upande wao baadhi ya washiriki walitaja changamoto ya kutokuwa na dhamana ambazo mara nyingi huhitajika katika kuchukua mikopo kwenye asasi za kifedha, kama vile hati za umiliki ardhi, nyumba na mali kutokana na wanaume ndiyo wenye majina yao kwenye mali hizo. Katika kujibu hoja hiyo, Meneja Pamui aliwasihi wakinamama kutokusita kufika kwenye tawi la benki kwa ajili ya mawasiliano,

“Njoo, tukae, tuzungumzie mstakabali huo tupate jibu”, alisisitiza.

Hata hivyo ndani ya semina hiyo kuliambatana na ufunguzi wa akaunti za Biashara kwa akina mama wajasiliamali ambao wengi wao walikuwa hawajafungua akaunti hizo.