RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amezitaka nchi tajiri na zilizoendelea duniani kutimiza ahadi zao za kutoa fedha kusaidia nchi masikini zinazoendelea kuchukua hatua za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.
Amesema kuwa rekodi zinaonyesha kuwa nchi tajiri na zilizoendelea hazijatoa fedha zozote mpya kwa ajili ya kugharimia hatua za kupambana na athari za mabadiliko ya tabia nchi katika miaka mitatu iliyopita, kama ilivyokubaliwa, na badala yake nchi tajiri zimekuwa zinatoa fedha ambazo ziliahidiwa siku nyingi.
Aidha, Rais Kikwete ametaka kuwepo kwa uwazi kuhusu jinsi ahadi hizo zinavyotimizwa na jinsi fedha inavyogawanywa duniani kwa sababu mpaka sasa kuna ukosefu mkubwa wa uwazi katika jambo hilo.
Rais Kikwete amesema, Novemba 20, 2013, wakati aliposhirikiana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mheshimiwa Ban Ki Moon kufungua Mjadala wa Mawaziri kuhusu Jinsi ya Kugharimia Hatua za Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabia Nchi ikiwa ni sehemu ya Mkutano wa Kimataifa wa Mabadiliko ya Tabia Nchi (COP19/CMP9) unaoendelea mjini Warsaw, Poland.
Akishiriki katika ufunguzi wa Mjadala huo kwenye Uwanja wa Taifa wa Poland ambako Mkutano wa Tabia Nchi unafanyika, Rais Kikwete amewaambia wajumbe kuwa jitihada za nchi zinazoendelea kukabiliana na athari za mabadiliko ya taiba nchi zinakwamishwa na ukosefu wa fedha zilizoahidiwa na nchi zilizoendelea.
“Kama mnavyokumbuka, mwaka 2010 mjini Cancun, Mexico, Jumuia ya Kimataifa ilielewa hali ya nchi zinazoendelea na kukubali kugharimia hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi. Yalikuwa ni makubaliano yaliyotoa kipaumbele kwa nchi masikini zaidi duniani (LDC’s), yaani Mataifa Madogo ya Visiwa na Afrika,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Ahadi ya pesa mpya na ya nyongeza ya kiasi cha dola za Marekani bilioni 30 ilileta matumaini mapya katika mazingira ya kukatisha tamaa kwa nchi walengwa. Lakini sasa tunashuhudia kuwa mambo hayakwenda kama ilivyokubaliwa. Kwanza, kiasi kikubwa kilichotolewa hakikuwa fedha mpya wala za nyongeza, kama ilivyokubaliwa mjini Cancun.”
Rais Kikwete amesema kuwa nchi chache ambazo zimetimiza ahadi yao zimefanya hivyo siyo kwa kutoa fedha mpya wala za nyongeza isipokuwa kwa kutoa fedha za Misaada ya Maendeleo (ODA) zilizokuwa zimeahidiwa huko nyuma.
“Isitoshe, sehemu kubwa ya fedha hizo zilitolewa kwa nchi zenye kipato cha kati. Hii ilikuwa tofauti na makubaliano kuwa fedha zingeelekezwa kwa mahitaji ya nchi masikini zaidi kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.”
Rais pia ametaka uwazi zaidi katika kutolewa kwa fedha hizo. “Hali ya ukosefu wa uwazi inasababisha ugumu wa kujua kama ahadi zimetimizwa ama hazijatimizwa, na kama zimetimizwa ni kwa namna gani. Isitoshe, hakuna uratibu wa utoaji wa fedha na mchakato wa kuweza kupata fedha hizo ni mrefu na mgumu. Ukosefu wa utabiri huo unasababisha ugumu wa kuamua faida za fedha za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Njooni niwapeni mfano wa Tanzania ili kuthibitisha ninayoyasema. Tathimini yetu ya karibuni inaonesha kuwa nchi yetu imepokea dola za Marekani milioni 20 kwa ajili ya kuunga mkono masuala ya tabia nchi. Lakini rekodi za wafadhili zinaonyesha kuwa kiasi kilichotolewa kwa Tanzania ni kikubwa mno – dola milioni 200. Ni jambo la kushangaza sana kuwa tumeweza kurekodi asilimia 10 ya kiasi kilichopokelewa.”
Amesisitiza Rais Kikwete: “Haya, kwa maoni yangu, ndiyo baadhi ya mambo ya msingi ambayo yanahitaji hatua za haraka za Jumuia ya Kimataifa. Fedha kwa ajili ya mabadiliko ya tabia nchi zinatakiwa kunufaisha watu wote.”