Mkurugenzi Mtendaji wa Shirikisho la Viwanda Nchini (CTI) Bi Christine Kilindu (Mwisho Kulia) akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hali ya viwanda nchini na mchango wa sekta hiyo katika kupambana na tatizo la ajira katika kilele cha Siku ya Viwanda Afrika, (Kati Kati) ni Kaimu Katibu Mkuu Odilo Otieno (Kushoto) Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Viwanda (UNIDO) Emmanuel Kalenzi .
MKURUGENZI Mtendaji wa Shirikisho la Viwanda Nchini (CTI) Bi Christine Kilindu amesema moja ya vikwazo katika ukuaji wa sekta ya viwanda na biashara ni uwepo wa wadhibiti wengi (Regulators) na tozo ya ushuru wa asilimia 0.2 ni kizingiti kwa maendeleo ya viwanda Tanzania. Moblog inaripoti.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam katika kuadhimisha siku ya Viwanda Afrika ukumbi wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko, amesema moja ya mambo ambayo yanawakwaza wawekezaji na wafanyabiashara ni uwepo wa wadhibiti wengi katika sekta ya viwanda.
“Sisi hatujakataa kudhibitiwa ila tulikwenda kumuona Katibu Mkuu Kiongozi Ikulu na tulimweleza juu ya matatizo ya kuwa na wadhibiti wengi na kila mtu ana taka asilimia zake (percent) hiki ni kikwazo katika ukuaji wa sekta ya viwanda hapa nchini,” amesema Bi Kilindu
Amesema kwamba pamoja na hayo lakini kwa siku za hivi karibuni hali ya kutegemaa kwa nishati ya umeme kumefanya sekta ya viwanda kupiga hatua kubwa kwani kwa sasa wanachangia asilimia 10 ya ajira na asilimia 20 ya bidhaa zinazouzwa nje ya nchi.
Kilindu amesema shirikisho la viwanda linaunga mkono kwa dhati kabisa dhana ya ujasiriamali katika kusukuma gurudumu la maendeleo pamoja na kuanza kufundisha elimu ya ujasiriamali mashuleni kuanzia shule ya msingi mpaka sekondari.
Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Viwanda toka Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko Bi Elli Pallangyo akizungumzia ukuaji wa viwanda kwa miaka ya hivi karibuni ambapo amesema jumla ya viwanda 700 vimeanzishwa nchini.
“Tunataka elimu ya ujasiriamali katika shule za msingi na sekondari ili vijana wetu waanze kufundishwa kuhusu ujasiriamali na waondokane na dhana ya kuajiriwa na waweze kujiajiri,” aliongeza
Naye Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Viwanda (UNIDO) Emmanuel Kalenzi amesema katika siku ya Viwanda Afrika ni muhimu kwa nchi na wadau wote wa maendeleo duniani ksuhirikiana katika kukuza hali ya ujasiriamali miongoni mwa jamii.
Amesema kuwa sekta ya viwanda ni mhimili mkubwa katika kutokomeza tatizo la ajira kwa vijana kupambana na umaskini na ni chachu ya ukuaji wa uchumi na pato la taifa.
Kalenzi alilisitiza kuwa shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Viwanda limejikita katika kufanya utafiti na kuhamasisha uwekezaji wenye tija kwenye sekta ya viwanda lakini viwanda vyenye kutoa ajira rasmi na inayoheshimika.
“Ongezeko la watu wasio kuwa na ajira Afrika ni ushahidi tosha kwamba bara la Afrika linatakiwa kujikita zaidi katika kuanzisha viwanda vipya na vinavyotoa ajira kwa sababu asilimia 63 ya watu walioajira Afrika wako katika ajira hatarishi,” amesema Kalenzi
Kwa Upande wake Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko Odilo Majengo amesema kwamba viwanda vya uzalishaji ambavyo vipo nchini Tanzania vinaweza kuinua uchumi wa taifa na kukuza pato la nchi.
“Kesho ni kilele cha siku ya viwanda Afrika na ni muhimu kwa watanzania wote kushiriki katika maonyesho hayo yanayoendelea katika viwanja vya saba saba ukumbi wa PTA kwani wafanyabiashara wengi wataonyesha bidhaa zao,” amesema Majengo
Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Viwanda toka Wizarani, Bi Elli Pallangyo amesema kwa kipindi cha miaka mitano mpaka sasa taifa limeweza kupata viwanda vipya 700 na pato la taifa kupitia vianda kufikia asilimia 9.
Bi Pallangyo aliongeza sekta ya viwanda kwa miaka hivi karibuni imepiga hatua kubwa za kimaendeleo na kuchangia kwa kiasi kikubwa pato la taifa na mauzo nje ya nchi.
Wakati huo huo pamoja na serikali kutamba kwa uanzishwaji wa viwanda vipya lakini Kuna baadhi ya viwanda vilivyokuwa vikifanya kazi miaka ya nyuma hasa katika serikali ya awamu ya kwanza na ya pili, lakini sasa havipo tena baada ya watu waliokabidhiwa kushindwa kuviendeleza.
Baadhi ya viwanda hivyo ni kama kiwanda cha nguo cha Urafiki Garments kilichopo ubungo, Tanzania Dairies limited ambacho kilikuwa cha maziwa, Ubungo Spining mill, pamoja na cha Zana za kilimo (UFI) ambacho kilikuwa maalum kwa ajili ya kutengeneza zana za kilimo. Vingine ni Tanzania Sewing Thread na Poly Sacks. Viwanda hivyo hivi sasa havifanyi kazi.
Viwanda hivyo vilikuwa vinafanya kazi katika awamu ya kwanza ya Mwalimu Julius Nyerere, lakini sasa vimekufa kutokana na uzembe na kuridisha nyuma sekta ya viwanda nchini.
Hivi Karibuni, Waziri wa Viwanda na Biashara Dk Abdallah Kigoda, alitoa ripoti inayoonyesha jinsi hali ya viwanda ilivyo barani Afrika.
Ripoti hiyo ilijikita zaidi kwa nchi ya Tanzania ikionyesha jinsi viwanda vyake vilivyodorora.
Kigoda anaelezea kwamba ripoti hiyo imejikita zaidi kutatua matatizo mbalimbali ambayo yameikumba sekta ya viwanda.Anasema wanajipanga jinsi ya kutatua matatizo yaliopo kwenye sekta hiyo ili kufufua viwanda na kuleta maendeleo nchini.
Dk Kigoda anasema Serkali itaweka mazingira bora kwa ajili ya kuvutia wawekezaji, kuboresha na kulegeza masharti kwa wawekezaji, kuboresha miundo mbinu, na kupambana pamoja na urasimu.
Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Viwanda (UNIDO) Bw. Emmanuel kalenzi akihojiwa na mwandishi wa MOblog.
“Ripoti hii imejikita zaidi jinsi ya kutatua matatizo mbalimbali zinazoikumba sekta ya viwanda nchini, naamini kwa kufanya hivi sekta ya viwanda itainuka upya,” anasema Kigoda.
Dk Kigoda:Tufufue viwanda vyetu
Kutokana na hali hiyo Serikali na sekta binafsi zinatakiwa kuungana ili kufufua uchumi kupitia viwanda na siyo kutegemea kilimo tu kama uti wa mgongo wa taifa.
“Mageuzi ya fikra zetu yanahitajika kuitazama upya sekta ya viwanda na kuacha kusema kwamba kilimo pekee ndio uti wa mgongo wa taifa letu kwani hata nchi zilizoendelea zinathamini viwanda pia,” anasema Kigoda.
Waziri huyo anafafanua kwamba vitendo vinahitajika zaidi kufufua sekta ya viwanda.
“Lazima tuondokane na nadharia na kujikita kwenye vitendo ili Wizara ya Viwanda na biashara ipanue soko la ndani na nje, lakini hili litafanikiwa baada serikali na sekta binafsi kuungana pamoja,”amesema Kigoda.
Anabainisha kwamba tatizo kubwa linaloikumba sekta ya viwanda nchini ni ukosefu wa mitaji na tatizo la kupatikana kwa soko la uhakika la kuuza bidhaa za viwandani.
Anafafanua kwamba matatizo hayo yanasababisha kudorora kwa biashara katika nchi za Afrika.
“Ukosefu wa mtaji kwa wafanyabiashara ni changamoto kuu inayowafanya washindwe kuwekeza kwenye viwanda, hadi kufikia biashara katika nchi.
Kutokana na kuwapo kwa tatizo hilo biashara imedorora kwa sababu imekuwa ikifanyika kwa asilimia 10 tu ukulinganisha na nchi nyingine duniani.
Viwanda vinatumia mitambo duni
Katika hatua nyingine wizara husika kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Viwanda (UNIDO), imeandaa ripoti ambayo imechambuliwa kiundani kuhusu maendeleo ya viwanda Tanzania ili kuonyesha matatizo yanayokabili viwanda nchini.
Chanzo: Moblog