Na Yohane Gervas, Rombo
TATIZO la ukosefu wa maji katika Kijiji cha Alen chini limechukua
sura mpya baada ya wananchi kuamua kufukua mabomba ya maji na kujiunganishia maji wenyewe.
Wakizungumza na Mtandao huu wananchi hao walisema wameamua kufikia hatua hiyo baada ya kubaini kuwa mafundi wa kampuni ya maji ya Kiliwater waliyafunga maji hayo yasielekee ukanda wa chini makusudi.
Mmoja wa wakazi wa Kijiji hicho, Dominiki Kavishe alisema wananchi wamefikia hatua hiyo baada ya kukosa ushirikiano kutoka kwa viongozi wa kijiji na mafundi wa kampuni husika. “…Kila mara wakiitwa wanagoma kuja kurekebisha tatizo hilo.” alisema Kavishe.
Alisema kwa sasa tatizo hilo limedumu kwa mwezi mmoja, huku idadi kubwa ya wananchi eneo hilo hawapati huduma ya maji, huku wakishangaa kuona wanalipishwa bili za maji kwa kulazimishwa na kutishiwa kuwa endapo hawatatoa fedha watang’olewa mabomba.
Alisema suala hilo limewasababishia usumbufu mkubwa kwani hulazimika kufuatilia huduma ya maji mbali na wasioweza kumudu huduma hiyo hulazimika kununua ndoo ya maji kwa shilingi 500.
Kero ya maji eneo hilo imewaathiri pia wanafunzi ambapo hulazimika kutumia muda mwingi kufuatilia maji badala ya kujisomea. Sara Adelard ni mwanafunzi wa kidato cha pili; alisema tatizo hilo limewaathiri vibaya wao kwani wanatumia muda wao mwingi kutafuta maji badala ya kusoma.
Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho, Bazil Kiwango alikiri kuwepo kwa kero ya maji na kudai kuwa suala hilo ni la kawaida kwa kipindi cha kiangazi.
Hata hivyo akizungumzia hali hiyo, Meneja wa Kampuni ya Kiliwater wa Wilaya ya Rombo, Prospa Kessy alikiri kuwepo kwa tatizo na kudai linatokana na tatizo la kiufundi ambapo katika moja ya mabomba ya kupitisha maji uliingia mzizi wa mti na kuziba maji yasipite.
Aliongeza kuwa tatizo hilo kwa sasa linafanyiwa kazi. Pamoja na hayo alikiri upungufu wa maji katika vyanzo tegemezi vya Mwaheni na Ndimila hasa kipindi cha kiangazi.