KIKOSI cha Zimbabwe kinawasili leo mchana (Novemba 18 mwaka huu) kuikabili Taifa Stars katika mechi ya Kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA)- FIFA Date itakayofanyika kesho (Novemba 19 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Msafara wa timu hiyo ukiwa na watu 30 utatua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) saa 8 kamili mchana kwa ndege ya Kenya Airways yenye mruko namba KQ 484 kupitia Nairobi.
Kocha wa timu hiyo Ian Gorowa atazungumza na waandishi wa habari mara baada ya timu hiyo kutua JNIA. Kiongozi wa msafara wa timu ya Zimbabwe ni John Phiri.
Wachezaji wanaounda kikosi hicho ni makipa; Frankson Busire, Maxwell Nyamupangedengu na Tapiwa Kapini. Mabeki ni Carrington Nyadombo, Felix Chindungwe, Innocent Mapuranga, Nkosana Siwela, Ocean Mushure na Patson Jaure.
Viungo ni Isaac Masami, Kundakwashe Mahachi, Milton Neube, Misheck Mburayi, Obey Mwenehari na Silas Dylan Songani. Washambuliaji ni Gerald Ndlovu, Lot Chiungwa, Nqobizitha Masuku, Simba Sithole na Themba Ndlovu.
Waamuzi wa mechi hiyo wanatoka Uganda wakati Kamishna atakuwa Leslie Liunda wa Dar es Salaam. Mwamuzi wa mezani ni Oden Mbaga pia wa Dar es Salaam.
Viingilio ni sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya bluu na kijani, sh. 30,000 kwa VIP A, sh. 20,000 kwa VIP B, sh. 15,000 kwa VIP C wakati viti vya rangi ya chungwa ni sh. 10,000.
Tiketi zinauzwa kwenye magari maalumu katika vituo vya; Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, mgahawa wa Steers uliopo Mtaa wa Ohio na Samora, Dar Live Mbagala, OilCom Ubungo, Uwanja wa Uhuru, na kituo cha mafuta Buguruni.
*Imeandaliwa na Boniface Wambura Mgoyo, Kaimu Katibu Mkuu
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)