Mapigano Mapya Yazuka Libya Watu 40 Wauawa

Mapigano Mapya Yazuka Libya Watu 40 Wauawa

MAPIGANO mapya yamezuka mjini Tripoli Libya Novemba 16, 2013 wakati idadi ya watu waliouawa katika mapigano wakati wa maandamano ya kupinga wanamgambo ikipanda na kufikia watu 43. Zaidi ya watu 450 wamejeruhiwa wakati maandamano siku ya ijumaa yalipozusha mapigano katika mji huo mkuu baina ya makundi ya wanamgambo ambayo yaliendelea usiku kucha, amesema waziri wa sheria Salah al-Marghani.

Waziri mkuu Ali Zeidan, ambaye alitekwa nyara kwa muda na wanamgambo mwezi uliopita katika tukio ambalo linaelezea hali inayoongezeka ya kutokuwa na uthabiti, ametoa wito wa “kuvumiliana na kusitishwa kwa mapigano,”akionya kuwa ” muda unaokuja na siku zijazo zitakuwa muhimu katika historia ya nchi ya Libya”.

Usiku wa Jumamosi, maofisa wa mji wa Tripoli wametangaza, “mgomo wa nchi nzima wa siku tatu katika sekta ya umma na binafsi kuanzia Jumapili” ikiwa ni jibu kutokana na ghasia hizo. Nchi hiyo imeshuhudia ongezeko la hali isiyo tulivu wakati waasi wa zamani ambao walisaidia kuuangusha kutoka madarakani utawala wa Muammar Gaddafi uliodumu miongo kadha mwaka 2011, walipuuzia madai ya serikali ya kutaka waweke silaha zao chini.

Ghasia hizo mpya zilizuka wakati waandamanaji wakiwa wamebeba bendera nyeupe walioingia mitaani katika maeneo ya majengo ya kifahari ambayo yanatumika kama kituo cha kikosi cha Misrata, kinachoundwa na wapiganaji waliokomaa kwa vita kutoka mji wa magharibi wa Misrata, na wakidai kuwa wanamgambo hao waondoke mjini humo. Watu wenye silaha walifyatua risasi kutoka ndani ya nyumba hizo katika eneo la Gharghour, na kuuwa waandamanaji kadha na kusababisha wanamgambo wa makundi mengine kushambulia kituo hicho cha wanamgambo wa Misrata, na kuchoma sehemu ya eneo hilo.

Mji wa pwani wa Misrata, ulioko kilomita 200 mashariki ya mji ya Tripoli, umeshuhudia mapigano makubwa kabisa kuwahi kutokea tangu vuguvugu la maandamano ya umma ya mwaka 2011. Kikosi cha Misrata kilishambulia kambi ya jeshi mapema Novemba 16, na kuzusha duru nyingine ya mapambano ambapo mtu mmoja ameuwawa na wengine wanane wamejeruhiwa, kwa mujibu wa kanali Mosbah al-Harna, kamanda wa kikosi kingine ambacho kwa kawaida kiko chini ya mamlaka ya wizara ya ulinzi.

Harna amesema wanamgambo wa kikosi cha Misrata baadaye walipora kituo hicho cha jeshi, wakichukua magari, silaha na risasi. Wapiganaji wengi zaidi kutoka Misrata walijaribu kuingia mjini Tripoli kutoka upande wa mashariki, na kuzusha mapigano na wanamgambo hasimu kabla ya mlolongo wa wanamgambo hao wa ziada kurejea nyuma kwa kilometa kadha.

Kikosi cha “Ngao ya Libya” ambacho ni kikosi kingine cha waasi wa zamani ambacho kilikuwa chini ya udhibiti wa serikali, baadaye kilitangaza kuwa kinalidhibiti eneo la Gharghour wakati wapiganaji wa Misrata wakijitoa katika eneo hilo. Kikosi cha Ngao ya libya katika eneo lenye matatizo la mji wa mashariki wa Benghazi nacho kilikuwa lengo la maandamano mwezi Juni ambayo pia yalisababisha umwagikaji wa damu, ambapo watu zaidi ya 30 walipoteza maisha.

Barabara kuelekea mji wa Tripoli kutoka upande wa mashariki imefungwa, amesema mwandishi mmoja wa shirika la habari la AFP, na mji huo sasa uko shwari hadi jana jumamosi, lakini shughuli nyingi za kibiashara na maduka zimefungwa.
-DW