Picha anuai juu ni Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiwa na Rais wa Sri Lanka Mhe. Mahinda Rajapaksa alipomtembelea kwa mazungumzo kwenye jengo la Temple Trees jijijini Colombo leo Novemba 14, 2013 kabla ya ufunguzi rasmi wa mkutano wa wakuu wa nchi za jumuiya ya madola mwaka huu (CHOGM 2013). Picha na Ikulu.
Rais Kikwete akutana na Rais Rajapaksa wa Sri Lanka
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, Novemba 14, 2013, amekuwa mmoja wa viongozi wa kwanza na wachache kukutana kwa mazungumzo na Rais Mahinda Rajapaksa wa Sri Lanka katika Makazi Rasmi ya Rais wa nchi hiyo ya Temple Trees mjini Colombo, mji mkuu wa nchi hiyo.
Rais Kikwete akifuatana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mheshimiwa Bernard Membe na Balozi wa Tanzania nchini Sri Lanka, John Kijazi amezungumza na Mheshimiwa Rajapaska kwa kiasi cha dakika 35.
Rais Kikwete amekuwa miongoni mwa viongozi watatu ambao wamekutana na Rais Rajapaksa leo miongoni mwa viongozi wengi ambao kesho wanaanza Mkutano wa Wakuu wa Serikali wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Madola (CHOGM).
Viongozi wengine wa Nchi na Serikali waliokutana na Rais Rajapaksa, ambaye ni mwenyeji wa Mkutano wa Jumuiya ya Madola, ni Waziri Mkuu wa Malaysia, Datuk Seri Najib Tunku Razak na Waziri Mkuu wa Pakistan, Muhammad Nawaz Sharif.
Katika mazungumzo kati ya Rais Kikwete na Rais Rajapaksa, viongozi hao wawili wamejadili masuala yanayohusu uhusiano kati ya Tanzania na Sri Lanka na masuala ya kimataifa ukiwamo mkutano wa Jumuiya ya Madola wenyewe unaoanza kesho, Ijumaa, Novemba 14, 2013.
Rais Kikwete amemshukuru Rais Rajapaksa kwa kutuma wataalam wa zao la nazi ambao karibuni walikuja Tanzania kuangalia na kushauri kuhusu ugonjwa wa minazi ambao unashambulia zao hilo nchini. Wataalam hao tayari wamerejea Sri Lanka kufanya utafiti na vipimo vya kisayansi matokeo ya uchunguzi wao.
“Mheshimiwa Rais umeahidi na umetimiza. Kama ulivyoahidi wakati wa ziara yako katika Tanzania, wataalam wamekuja na sasa tunasubiri matokeo ya uchunguzi wao na ushauri wao,” Rais Kikwete amemwambia Rais Rajapaksa.
Rais Kikwete pia amemshukuru Rais Rajapaksa kwa kushawishi makampuni ya Sri Lanka kuwekeza katika shughuli za viwanda vya nguo na miradi midogo ya kuzalisha umeme.
Rais Kikwete pia amemshukuru Rais Rajapaksa kwa mwaliko wake wa kushiriki mkutano wa Jumuiya ya Madola na pia akampongeza kwa kuandaa vizuri mikutano ya mwanzo ya Jumuiya hiyo iliyotangulia Mkutano wa Wakuu wa Serikali wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Madola (CHOGM).
“Naomba radhi pia kuwa sikuweza kufika mapema ili kufanya ziara rasmi kama tulivyokuwa tumekubaliana ulipotutembelea nyumbani. Wewe unajua mambo ya uongozi, shughuli zimekuwa nyingi kidogo kuliko kawaida,” amesema Rais Kikwete.
Naye Mheshimiwa Rajapaksa amemshukuru Rais Kikwete kwa kusaidia kuongeza hamasa ya viongozi wa Afrika kushiriki katika Mkutano wa mwaka huu wa Jumuiya ya Madola.
“Aidha, tunakushukuru wewe binafsi kwa kusafiri safari ndefu kuja kuhudhuria mkutano huu. Asante sana”.
Rais Kikwete na Mama Salma Kikwete wamewasili nchini Sri Lanka asubuhi ya leo kutokea nyumbani tayari kuhushuria Mkutano huo wa Jumuiya ya Madola.