Na Rungwe Jr.
Ndugu zangu, Juma hili Mh. Rostam Aziz hatimaye ‘amejivua gamba’. Kama tulivyosikia na kusoma hotuba ya Mh. Aziz mwenyewe wakati anawaaga wana Igunga, haukuwa uwamuzi rahisi kwake. Pamoja na hayo, huu ni uwamuzi wa busara na hatua ya msingi kwa chama chake cha Mapinduzi, kwani angalau kimeonyesha usikivu katika yale yanayopigiwa kelele. Moja ya yale yanayopigiwa kelele na wadau mbalimbali ni hatma ya wale wanaotajwa kwenye tuhuma za ufisadi, ambazo zimegubika taifa letu.
Katika hotuba yake ya kuwaaga wana Igunga, Aziz alisema “Tatu, nilishangazwa na kushitushwa na ujasiri ambao umekuwa ukioneshwa na baadhi ya viongozi wetu wapya wa Sekretarieti wanaolitaja jina langu na kulihusisha na kile wanachokiita ufisadi ambao hata ukweli wa kimazingira na kihistoria ukiachilia mbali ushahidi wa wazi umeshathibitisha kwamba ni porojo za kisiasa zilizotokana na makovu na matarajio ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 na ule ujao wa 2015.” Nukuu hii inaonyesha dhahiri kwamba kulikuwa na shinikizo ndani ya chama kumtaka Aziz ajiuzuru na kujiuzuru kwake angalau kumeonyesha masikio ya CCM. CCM itaonyesha usikivu zaidi endapo itahakikishwa wale wanaotajwa sambamba na Aziz pia ‘wanajivua gamba’ na hatua zaidi zinachukuliwa dhidi yao!
Imekuwa ni kawaida kwa nchi zilizoendelea kama Marekani na nyinginezo, viongozi wake kuwajibika mara moja pindi wanapokuwa wamekabiliwa na tuhuma nzito za mmomonyoko wa maadili dhidi yao. Wengi wamepoteza nafasi zao za uwakilishi sio tu kwa tuhuma za ufisadi, bali hata zile za ngono. Kwa mfano hivi karibuni Mwakilishi Athony Weiner wa New York alijiuzuru nafasi yake hiyo baada ya kubainika amesambaza picha zake za ‘kingono’ mtandaoni. Watanzania ipo siku na sisi tutafika huko tu, kwani viongozi ni ‘viyoo vya jamii’ hivyo basi, hawana budi kuwa watu safi katika nyanja zote.
Sipo hapa kumuhukumu Mh.Aziz, kwani kama alivyosema mwenyewe “Wazee wangu, nyinyi ni mashahidi kwamba, mbali ya mimi mwenyewe kujitokeza kupitia vyombo vya habari na kueleza wazi kwamba sijapata kujihusisha katika vitendo vyovyote vya ukiukwaji wa maadili ya uongozi au vya rushwa, hakuna ushahidi wowote uliotolewa unaonihusisha na kashfa yoyote miongoni mwa zile zilizotajwa.” Ni kweli kwamba bado hakuna ushahidi unaothibitisha kwamba Mh. Aziz ametenda yale anayotuhumiwa, lakini huu sasa ni wakati muafaka wa kukamilisha ushahidi (Kama upo) na kumfikisha Mh. Aziz mahakani kujibu tuhuma zinazomkabili.
Uwajibikaji hautakiwi uishie kwenye kujiuzuru tu! Tunataka hatuwa zaidi ya hapo zichukuliwe kwa kumpa nafasi Mh. Aziz kujibu tuhuma zinazomkabili mahakamani.
Mungu Ibariki Tanzania.